TUME YA MABADILIKO YA KATIBA NA UKUSANYAJI WA
MAONI YAWANANCHI MIKOANI.
Na Festo Mukerebe
Mimi sio mchambuzi wa mambo ya siasa. Lakini hilo halijawahi kunizuia kutoa maoni yangu binafsi kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisiasa yanayojitokeza nchini mwetu. Na wala sijali hata kuitwa mwandishi ‘kanjanja’. Ni sawa tu hata nikiitwa hivyo, maana ni kweli kwamba mimi sijawahi kusomea popote taaluma ya uandishi wa habari.
Sensa ya Watu na Makazi, 2012, imemalizika. Sasa tunarejea katika mada za maisha na mambo tuliyoanza kuyazoea kabla ya ujio wa zoezi hilo la Sensa, ambalo hututembelea mara moja katika kila muongo. Mada inayochemka zaidi ndani ya jamii yetu kwa sasa, na ambayo inaelekea tutadumu nayo kwa muda mrefu ujao, ni Mabadiliko ya Katiba. Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeingia katika awamu ya pili ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi, ikiwa imemaliza kutembelea mikoa minane, bara na visiwani.
Katika makala hii, nashawishika kuiangalia kidogo kauli ya hivi karibuni ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba, kauli ambayo tayari imedakwa na wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari.
Kupitia tahariri za vyombo hivyo, tumehabarishwa kuhusu dosari iliyojitokeza katika awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi, kwa mtazamo wa Mwenyekiti wa Tume. Mimi nilitarajia zitajwe dosari nyingi zaidi. Lakini haikuwa hivyo. Kwa kutajwa dosari moja tu, nashawishika kuamini kwamba hadi hatua hii, zoezi hilo linakwenda vizuri. Heko kwa Tume ya Warioba!
Dosari iliyotajwa, na kwa maoni yangu kukuzwa sana, inahusu wanasiasa na vyama vya siasa kuonekana ‘wanaingilia’ mchakato wa zoezi, kwa kuwazungukia wananchi na ‘kuwapandikizia’ maoni yenye mwelekeo wa kujijenga kisiasa. Inaelezwa kwamba kusudi la wanasiasa hao (au vyama vyao), ni kujenga taswira, mwisho wa siku, kwamba maoni ‘waliyopandikiza’ ndiyo maoni halali ya wananchi walio wengi.
Mwenyekiti Warioba na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari, wameushitukia na kuulaani kwa nguvu mkakati huo wanaouona ni ‘mchafu’. Wameonyesha kukishangaa kitendo hicho, hasa kwa mantiki kwamba wanasiasa, vyombo vya habari na wananchi katika makundi yao mbalimbali, wametengewa fursa za kukutana na Tume kwa wakati muafaka ili kutoa maoni yanayosadifu misimamo yao na ya makundi ya kijamii na kisiasa wanayoyaongoza au kuyawakilisha. Ya nini, basi, kupenya ndani ya jamii na kuhamasisha misimamo fulani?
Nitamshangaa mtu yeyote ambaye mantiki ya hoja hii, itampiga chenga. Halikadhalika, nitamshangaa mtu atakayemshangaa Mwenyekiti Warioba kwa kukemea kitendo hicho.
Lakini kadiri ninavyoitafakari zaidi hoja hii, ndivyo ninavyojikuta nashangaa kidogo kwa nini tupoteze nishati kubwa kiasi hiki katika huku kulikemea jambo hili. Ni jambo linalojulikana kwamba katika jamii yoyote ile, viwango vya uelewa wa jambo lolote hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Baadhi ya watu hulielewa kidogo jambo. Wengine hutokea kulielewa kwa kiwango cha wastani tu. Lakini wengine, aghalabu walio wengi, huchelewa kulijua jambo hilo, na huenda haitatokea wakalimaizi jambo hilo katika maisha yao yote, hata kama wanaliunga mkono kabisa. Lakini wapo watu, hata wawe wachache namna gani, ambao hulielewa na kulidadavua vizuri jambo kwa undani kushinda watu wengine.
Kwa maoni yangu mimi, tofauti hizi za kiasili katika jamii, ndiyo msingi na sababu ya binadamu kuhitaji kuishi katika jamii. Na hapa ndipo taaluma na falsafa ya elimu jamii (sociology) hutufundisha kwamba binadamu huhitaji jamii, na kinyume chake- ili pale anapopungukiwa, anajaziwa na wenzake wanaomzunguka. Mwalimu Nyerere aliwahi kutoa hotuba kuhusu hoja hii: man needs society.
Katika kijiji cha kiasili, kwa mfano, utakuta watu wenye ujuzi na maarifa yanayotofautiana. Atakuwapo fundi seremala, mfinyanzi na mhunzi. Atakuwapo kinyozi na msusi wa nywele za kina mama. Atakuwapo ngariba na mpiga ramli. Atakuwapo manju wa ngoma na mvuvi wa samaki. Atakuwapo fundi ujenzi wa nyumba za kiasili. Atakuwapo mwindaji na mlenga shabaha mwenye uwezo wa kusaidia kuongoza misako ya wanyama waharibifu porini. Lakini watakuwapo pia watawala na wazee wenye hekima na busara kwa ajili ya kuiongoza jamii na kusuluhisha migogoro yake.
Orodha inaweza kuwa ni ndefu sana. Hoja hapa ni kwamba taaluma hizi zinapounganika, husaidia kuunda synergy madhubuti ambayo huzalisha nishati ya kuisukuma mbele jamii nzima ya kijiji hicho.
Masuala ya Katiba ni mambo yanayoangukia zaidi katika taaluma na sayansi ya siasa. Na haiwezekani watu wote katika jamii wakawa magwiji katika mambo ya siasa, au taaluma yoyote ile, kwa wakati ule ule. Watu wachache wenye uelewa mkubwa na mpana wa masuala ya siasa, ndio watategemewa kuiongoza jamii nzima katika mwelekeo na mchakato huo. Pengine watakuwa ni watu waliojaaliwa kwenda shule na kupata elimu ya kiwango cha kutosha, kuliko wenzao wengi. Au watakuwa wamejihusisha kwa vitendo katika uongozi na utawala.
Katika synergy ya kijamii, sisi tutahitaji wachache hawa watuongoze katika jambo hili la maoni kuhusu Katiba Mpya. Mbona tunataka kusahau kwamba Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere, akiwa amerejea kutoka masomoni Ulaya, miaka ya 1950, aliongoza harakati zetu za TANU kusaka uhuru hadi ukapatikana mwaka 1961? Si alikuwa kijana mdogo tu enzi zile, lakini mwenye upeo na visheni ya kuona mbali, akiwa anatuzidi kwa mbali sisi wananchi kabwela?
Na wala sio kwamba alituweka pembeni sisi Watanganyika, kwa kisingizio cha upeo wetu duni au kwa hofu - kama hizi tunazotahadharishwa nazo - kwamba atakuwa ‘anatubambikizia’ maoni na mitazamo yake binafsi. Wala hakudiriki kuifanya kazi ya mapambano peke yake. Na kama angalifanya hivyo na kupuuza kutushirikisha na kutuunganisha tukawa kitu kimoja, walahi asingalifanikiwa kutimiza azma yake ya ukombozi kama alivyofanya. Na mimi nimewahi kumsikia Mwalimu mwenyewe akilikiri jambo hili katika hotuba yake ya kuwaaga wazee wa Dar es Salaam, wakati alipoamua kung’atuka madarakani, mwaka 1985.
Katika hotuba ile, Mwalimu alieleza jinsi miaka hiyo wazee wa Dar es Salaam na sehemu nyingine nchini walivyokuwa wakisuasua na kutilia mashaka hatma ya harakati za uhuru. Ni baada ya kuwahakikishia uhalali wa harakati hizo katika ulimwengu wa siasa kimataifa wakati huo, alipofanikiwa kurejesha imani na ujasiri wao, baada ya miongo ya kukata tamaa, kufuatia kumbukumbu ya matokeo ya vita vya Maji Maji, kwa maisha ya wazee wao walioshiriki vita hivyo, mwishoni mwa karne ya 19. Nani aliyeshuhudia vitanzi vile, na bado akajitia kimbelembele katika mapambano?
Tangu kipindi kirefu cha utawala wa chama kimoja, Watanzania wamejifunza kuchunga na kudhibiti ndimi zao, hasa wawapo hadharani. Ni rahisi kujua sababu za ukimya huo, kama tunavyozijua sababu za ‘wazee wa Nyerere’ kusuasua katika harakati za mapambano ya uhuru.
Lakini kama alivyokuwa Nyerere mwenyewe, wapo Watanzania wachache waliojaaliwa mioyo ya ujasiri na wapo tayari wakati wowote kusimama mbele ya hadhara na kutoa maoni na mawazo yao kwa uwazi na ukweli, bila hofu ya matokeo hasi ya wao kufanya hivyo. Lakini yapo pia makundi ya kina mama na vijana, hasa vijijini, ambao kwa sababu za tamaduni za jamii zao, sio rahisi kusimama hadharani kutamba na maoni yao, japo wanayo mengi tu na yenye manufaa, kiasi cha kustahili kuingia katika Katiba Mpya.
Aidha, tusisahau kwamba, licha ya kuwa tumejitawala miaka mingi sasa, elimu ya kawaida huko vijijini, bado ni changamoto. Na wapo bado watu ambao hutegemea watu wengine wazungumze au kutoa maoni kwa niaba yao na wao wabaki kupiga makofi na kushangilia kwa vigelegele, ikiwa ni uthibitisho wao kwamba wanaafikiana na kukubaliana na maoni yaliyotolewa. Tukubali, tukatae, jamii zetu nyingi, hasa vijijini, bado ziko hivyo. Na wala tusitarajie kwamba ujio waTume ya Warioba utakuwa umeleta muujiza wa mabadiliko katika hali hiyo. Hakuna.
Mimi ninao uelewa wa kuridhisha wa jamii hizi za vijijini. Labda nilithibitishe jambo hili kwa maelezo mafupi ya kisa cha kweli. Nilikuwa nimewasili nyumbani kwa likizo; na katika kujuliana hali na mmoja wa jamaa zangu, akaniacha sina mbavu kwa tambo zake za ‘mafanikio makubwa’ mwaka ule. Kwa kipimo chake cha uelewa, alikuwa amevunja rekodi katika kilimo cha mahindi msimu ule. Nilipodadisi kuhusu mafanikio hayo makubwa, nikaambiwa kwamba katika shamba lake la ekari mbili, alikuwa hakukosa madebe kumi ya mahindi, kwa uchache .
Siku chache awali, mimi na wenzangu katika kituo nilichowahi kufanyia kazi, tulikuwa tumetembelea mradi wa shamba moja la mahindi, la shirika la World Vision. Katika risala ya wasimamizi wa mradi ule, tulikuwa tumeambiwa kwamba wao huzalisha magunia 30 ya kg 100@; kwa maana ya jumla ya madebe 180 kwa ekari moja. Wapi na wapi na uzalishaji wa ‘mafanikio makubwa’ wa jamaa yangu kwenye kipande cha ekari zake mbili za ardhi? Jamaa yangu wa ‘mafanikio makubwa’, hakuwa mwepesi kuielewa simulizi yangu ya World Vision. Ama kweli, akana katakyala, kati mawe achumba.
Katika hili, nakubaliana na Dk. Kitila Mkumbo kama alivyoandika katika Gazeti la Raia Mwema, hivi karibuni (Agosti 29-Septemba 4, 2012):
“Moja ya nguzo ya mafanikio kwa mtu binafsi au taasisi yoyote ni kutokuridhika. Ukiwa mtu wa kuridhika kirahisi kwa mafanikio mepesi huwezi kwenda mbali. Mfano mzuri ni mwanafunzi darasani. Ili mwanafunzi atoke hapo alipo ni muhimu aweke dhamira kwamba uwezo wake ni mkubwa kuliko aliokwisha kuuonyesha. Kama akiridhika na alama au namba anazozipata leo basi atabaki hapo hapo alipo ama ataporomoka zaidi.
Moja ya mambo yanayotukwamisha kupiga hatua kama taifa ni wepesi wetu, kama jamii, wa kuridhika kirahisi na mafanikio mepesi, na wakati mwingine pasipo na mafanikio yoyote”.
Mara mbili hivi, mnamo miaka ya 1980, nilitembelea kikazi jamii ya wawindaji na wabangaizaji ya Wahadzabe, huko Yaeda Chini, Bonde la Ufa, Arusha. Nilikuta watu hao wakihusisha magonjwa ya degedege, malaria n.k., na aina ya nyumba za banda walizokuwa wamejengewa na Serikali! Aidha, hawakuwa na habari kwamba nchi yetu iliwahi kupigana vita na Uganda. Wengine walituuliza habari za Nyerere, wakiwa hawana habari yoyote kwamba hatunaye duniani miaka mingi sasa!
Ninao uwezo wa kutoa mifano mingi zaidi ya hali ya jamii zetu na mapungufu ambayo watu wetu wenye elimu haba, hususan vijijini, wanaweza kuwa nayo katika nyanja mbalimbali za maisha. Sijui kama ni busara kwetu sisi, kwao au kwa yeyote yule, kukomalia hoja kwamba watu hao watoe maoni yao moja kwa moja bila msaada wa wenzao wenye uelewa mpana zaidi.
Nionavyo mimi, jambo muhimu zaidi ni kuhakikisha wananchi wameshirikishwa kikamilifu na kuelimishwa vya kutosha kuhusu kitu kinachoendelea katika mchakato mzima wa zoezi la kukusanya maoni yao. Na hapo sioni muhali vyama vya siasa, NGO na makundi mengine ya kizalendo kushiriki kusaidia kuifanya kazi ya uelimishaji na uhamasishaji wa wananchi.
Kwa nini inajengwa taswira ya kushinikiza kwamba wazo haliwezi kuwa chanya na lenye manufaa kwetu kama halikutolewa na watu husika wenyewe? Mbona tuliwahi kunufaika na harakati za uhuru na Azimio la Arusha, wakati ni mawazo ya watu wachache, the elites, yaliyoletwa kwetu, nasi tukayatohoa na hata kutembea kwa miguu masafa marefu kuyaunga mkono (Azimio la Arusha)?
Mbona hatukusubiri hadi jamii zetu zilitolee maoni Azimio la Arusha au Muungano, kwa mfano, ndipo liwe jema na lenye manufaa kwa nchi yetu? Wakati huo, mbona mazoezi mengine, kama vile Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, yamepata ukinzani mkali kutoka kwa makundi kadhaa ya kijamii nchini, wakati Watanzania wenyewe ni wale wale, wa enzi za ukoloni, uhuru na Azimio la Arusha? Kweli jambo hilo halitufundishi vya kutosha kwamba Watanzania wanazo busara za kutosha kutambua jambo lililo jema kwao na kuliunga mkono, hata kama limetokana na watu wachache?
Si ndiyo ile dhana ya synergy ya kijamii kazini, kama tuliyoidadavua hapo awali? Lakini mbona pia hatujiulizi kwa nini wakati fulani mwanzoni mwa mchakato wa kusaka Katiba Mpya, watawala wetu walituelekeza kuzitambua bila mjadala na kuziacha zilivyo (intact) zile zilizoitwa ‘tunu za Taifa’ letu? Au hilo halihusiani na ubambikizaji wa maoni kwa wananchi? Mbona ni yale yale? Au labda ni yale ya ‘mkuki kwa nguruwe, kwa binadamu mchungu’!
Lakini lipo jingine moja analotukumbusha Ahmed Rajab, mwanasafu wa Gazeti la Raia Mwema. Anaandika, na nanukuu: “…inasemekana kwamba Tume itatoa mapendekezo yake kwa kuzingatia nguvu za hoja zinazotolewa kuunga mkono rai fulani.
Haitotoa mapendekezo kwa kuzingatia rai fulani inaungwa mkono na wingi gani wa wananchi. Kipimo kitakuwa nguvu za hoja za kulitetea pendekezo fulani na wala si wingi wa idadi ya watu wenye kuliunga mkono pendekezo hilo.”
Sasa ni nani hadi hapo, asiyeona haja na umuhimu wa wachace, the elites, wenye upeo na uwezo wa kujenga hoja, kutuelimisha na kutuhamasisha tujenge hoja zenye mashiko sisi wenyewe; la sivyo, watusaidie wao kuzungumza na kudadavua mambo haya, kwa niaba ya sisi wengine - ilmradi tunajihusisha nao kama ‘wenzetu’ katika mapambano?
Kwa mwenendo huu wa kuendekeza (kwa kiwango hiki) hofu na woga wa baadhi ya watawala wetu na hata baadhi ya wahariri, sina hakika kama tutafika mbali.
No comments:
Post a Comment