Tuesday, October 23, 2012

VYAMA VYA UPINZANI VIJIEPUSHE KUSHEREHEKEA USHINDI
USIOPATIKANA BADO

                                         Na Festo Mukerebe
Mwandishi mmoja wa Afrika ya Magharibi, Ayi Kwei Armah, alikiita kitabu chake cha kifalsafa: The Beautiful Ones Are Not Yet Born. Kadiri ya mantiki ya kitabu hicho na mwenendo wa matukio ya enzi zetu hizi, ni wazi kwamba, Mwandishi huyo hakukosea hata chembe.
Mimi sikuwahi kukipenda Chama cha Mapinduzi, japo katika miaka yake ya awali, nilikuwa na Kadi ya uanachama. Hata hivyo, sijawahi kumbaini kiongozi bora kama muasisi wa chama hicho, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere.
Kama ningalibanwa kuthibitisha ukweli wa mapenzi yangu kwa Mwalimu, wala nisingalihitaji kwenda mbali sana. Watu walio karibu na mimi watakuwa wamebaini siku nyingi  kwamba ni nadra sana niwapo mapumzikoni nyumbani kwangu siku ipite bila kufungulia redio yangu  kukisikiliza kipindi cha Wosia wa Baba, ambacho hudhaminiwa na Shirika la Taifa la Mbuga za Wanyama nchini (TANAPA) na kurushwa na Kituo cha Televisheni cha TBC kati ya saa 2.15- 2.30 usiku, isipokuwa siku za Jumapili. Nakihusudu kupindukia kipindi hicho kwa sababu ya hotuba zake zisizochosha wala kuchusha.
Aidha, kwa miaka mingi pia, asilimia kubwa ya vitabu nilivyojitahidi kununua kwa ajili ya maktaba yangu ya nyumbani (home library), ni vile vinavyohusiana moja kwa moja na kazi za Mwalimu kitaifa na kimataifa, baada ya uhuru na hata baada ya kung’atuka kwake uongozi wa chama na serikali.
 Ni rai yangu ya dhati kwamba kama ipo tunu kubwa ambayo Watanzania tutakujajuta kuikosa katika maisha yetu ya sasa na ya vizazi vingi vijavyo, tunu hiyo ni hotuba zake, zile rasmi na hata zile ambazo Waingereza huziita impromptu, kwa maana ya zile zisizoandaliwa awali.
Ama kweli, Mwalimu alikuwa amejaliwa kipaji kisichomithilika cha kuzungumza na kuhutubia.  Ningalikuwa na mamlaka tosha, ningalielekeza kipindi cha Wosia wa Baba sio tu kirushwe kila siku , bali kipewe muda usiopungua saa nzima. Robo saa ya sasa haikidhi hamu ya baadhi yetu ambao tumetokea kuwa na mzio chanya  (positive addiction) na hotuba zenye mvuto mkubwa za gwiji hilo la siasa duniani.
Hivi ni kwa kiasi gani sisi Watanzania tunavihitaji vipindi vya muziki wanaouita wa ‘kizazi kipya’ na vingine kama ‘Bango’(matukio ya watu binafsi) na ‘Chereko’ (nadhiri za uongo na viapo vya kudanganyana ‘wapendanao’) ambavyo vinatufanya watu wazima tuonekane mazezeta mbele ya TV zetu, tukitumia muda wetu mwingi kukodolea program zisizokuwa na tija kwa maisha yetu?
    
Mwanzoni mwa makala hii, nimesema kwamba sijapata kukipenda Chama Cha Mapinduzi, hata kama ndicho chama alichopata kukiongoza Mwalimu. Nilimpenda Mwalimu bila kukipenda CCM. Hiyo ni kwa sababu kwa kila hatua, mimi huwa naiuliza nafsi yangu kama C.C.M. na serikali yake kweli ilikuwa inakidhi matakwa na utashi wangu katika maisha. Nyakati za Uchaguzi Mkuu, mimi hutazamia kila Mtanzania aihoji nafsi yake swali hilo kabla hajaamua kukipigia kura chama hicho. Sina hakika kama huwa wanafanya hivyo!
Hivi karibuni, niliandika makala moja kueleza kwa nini nilikua  sijisikii kushiriki zoezi la Sensa ya Idadi ya Watu na Makazi ya mwaka huu, 2012. Ili nisihusishwe na Waislamu wenye imani kali, nililazimika kueleza sababu zangu za kughairi zoezi lile (japo wakati wa Sensa yenyewe ulipowadia, nilijikongoja kushiriki kikamilifu). Moja ya sababu hizo, ilikuwa ni kushindwa kuona matunda ya kushiriki kwangu katika Sensa nyingi zilizotangulia (1957, 1967, 1978 na 2002).
Nilihoji kwa nini njia ya miguu niliyotembea peku mwaka 1961 (zaidi ya miaka 50 iliyopita) kwenda kuanza maisha ya shule, imeendelea kubaki ile ile hadi leo; mbona shule yenyewe (Kashumbililo Shule ya Msingi) haijabadilika sana hadi leo (licha ya kupandishwa hadhi kutoka darasa 4 hadi darasa la 7); mbona zahanati ya Kata yetu, Izigo, niliyoshiriki kwaya ya shule yangu kuifungua  mwaka 1964, haijabadilika hadi sasa (kwa maana ya miundo-mbinu na ubora wa huduma zake, n.k.? Sasa nishiriki Sensa nyingine ili iweje?
Najikuta nikishindwa kukipambanua Chama Cha Mapinduzi na mapungufu yote hayo (na mengine mengi ambayo nafasi ya makala hii haitoshi kuyataja). Kwangu mimi, mapungufu hayo ni kielelezo tosha cha kushindwa kwa Chama hicho kumuenzi ipasavyo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Hata kushindwa kwa serikali kukitengea muda wa kuridhisha kipindi cha Wosia wa Baba kuwa hewani  kupitia  chaneli yake ya Taifa, TBC, ni udhaifu mwingine ulio dhahiri.
Pengine jambo rahisi kama hilo linashindikana kufanyiwa kazi kwa sababu Hotuba zenyewe za Mwalimu kwa mantiki yake zinausuta uongozi na mwenendo mzima wa Chama hicho, haijalishi kwamba ni yeye mwenyewe aliyekiasisi na kukipa uhai wake. Kwani si aliwahi kukiri kwamba Chama hicho hakikuwa mama yake mzazi kiasi kwamba asiweze kufarakana nacho, ikibidi kufanya hivyo?
Watu wengi wenye uelekeo kama wa kwangu, mintarafu siasa za Tanzania, wananiaminisha kwamba wanatazamia mwaka 2015 tutashuhudia mwisho wa Chama Cha Mapinduzi kama Chama Tawala katika siasa za Tanzania. Na mimi binafsi ningalitamani iwe hivyo. Lakini kwa bahati mbaya, wishes are not horses.
Ni kweli  kwamba Chama Cha Mapinduzi hakitakuwa chama tawala cha kwanza barani Afrika kupoteza usukani. Yaliwahi kukitokea UNIP cha Zambia, cha KANU nchini Kenya na cha MCP nchini Malawi. Aidha, bado tunafuatilia mambo yanayoendelea kutokea kwa vyama tawala vya nchi zilizofanikiwa kuung’oa utawala wa nchi zao kasikazini mwa Bara la Afrika, ikiwa ni pamoja na Algeria, Tunisia, Misiri na Libya. Kwa hiyo, ni kweli kwamba mabadiliko kama hayo ni mambo yanayowezekana kabisa kutokea kwa chama kingine chochote, haijalishi ni kikongwe kiasi gani.
Lakini yatakuwa ni makosa na kujidanganya kufikiri kwamba jambo kama hilo litakuwa ni rahisi kutokea kwa Chama Cha Mapinduzi. Kwa nini? Kwa sababu vyama ambavyo vimeendelea kuwa madarakani barani Afrika, vilikwishashituka na kukaa chonjo, tofautina kina UNIP vilivyoshitukizwa na mabadiliko. Kwa vyovyote vile, vyama vikongwe madarakani  kama Chama Cha Mapinduzi, ZANU- PF, haviko tayari kufuata nyayo ya vyama tangulizi vya UNIP, KANU, MCP na vinginevyo vilivyoanguka mweleka wa mende. Vyama hivi vitang’ang’ania madarakani kama papasi afanyavyo juu ya kiwele cha ng’ombe, liwalo na liwe!.
Kwetu Tanzania, hali inaweza hata kuwa ngumu zaidi, kwani wapo baadhi ya Watanzania ambao hadi sasa hawajafanikiwa kukipambanua Chama Cha Mapinduzi na Mwalimu Nyerere pamoja na Sera  yake ya Ujamaa na Kujitegemea, siasa iliyotukuka nchini kwa miongo kadhaa kabla ya kifo chake mwaka 1999. Mifano michache yaweza kutolewa kulithibitisha jambo hili.
Wakati Tanzania ilipolazimika kutohoa mfumo wa vyama vingi, Mwalimu Nyerere, kwa upeo wake mkubwa, aliwapa changamoto wahafidhina wa siasa za chama kimoja ambao hawakuwa tayari kwa mabadiliko, kujizatiti kwa sababu za miaka ya Tisini (na sio zile za miaka ya Sitini zilizopitwa na wakati), la sivyo wakubali kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Kwa vile wahafidhina hawakuwa na sababu zenye mantiki wala uwezo wa kukabiliana na changamoto ya Mwalimu Nyerere, walijaribu kuibua hisia za vitisho na hofu kwamba vyama vingi vingezua mitafaruku katika jamii ambayo ingaliitumbukiza nchi katika lindi la mauaji ya kimbari, kama yale ya nchi jirani za Ruanda na Burundi. Kina mama na wazee waliogopeshwa sana kwa sinema zilizoonyesha wanawake wajawazito wakitumbuliwa matumbo yao na mimba zao kunyotolewa kwa ukatili na mateso ya kinyama!
Ni katika mazingira hayo kwa jumla, ndimo hatimaye mfumo wa siasa ya vyama vingi ulijikuta unazaliwa nchini Tanzania. Na kwa bahati mbaya, kizazi kilichotishwa na kutishika na wahafidhina waliopinga kuanzishwa kwa mfumo huo, bado kinadumu na huenda sumu ya mawazo yake, itachukua miaka mingi zaidi kufifia na kutoweka kabisa.
Niliwahi kushuhudia mara kadhaa kijiji cha nyumbani kwetu (jina la kijiji kapuni) kikitisika kwa mihemko ya kusherehekea ushindi wa Diwani wa Kata aliyepita kwa tiketi ya Chama Chama Mapinduzi. Mzee yule (jina linahifadhiwa), alikuwa tayari amedumu katika wadhifa ule kwa zaidi ya mihula mitatu, yenye jumla ya miaka isiyopungua thelathini! Baadhi yetu tuliendelea kujiuliza ni kwa rekodi gani mzee yule alikuwa ameendelea kupigiwa kura za ushindi katika Kata yetu!
Katika dadisi zangu binafsi, hatimaye nilifanikiwa kugundua kwa nini.  Wazee wengi wa vijiji vya kwetu na, hasa kina mama, walitegemea zaidi mauzo ya gongo (enkonyagi) kwa maisha yao ya kila siku. Lakini kwa vile kwa sheria za nchi yetu pombe hiyo ni haramu, shughuli hiyo iliwatia hofu ya kushukiwa na mkono wa nguvu za dola.
Kwa bahati, Diwani ‘wao’ alielekea kuwakingia kifua dhidi ya hatua za kisheria pale askari polisi au mgambo walipovamia vijijini, kwa taarifa au vinginevyo. Ni kwa msingi huo sasa, wazee walikuwa hawaambiliki wakati wa kupiga kura, kwani kiongozi huyo alikuwa ni tumaini na mtetezi wao wakati wa misako ya gongo, kodi na uhalifu mwingine mdogo mdogo vijijini.
Katika dadisi zangu nyakati za uchaguzi wa vyama vingi, nimewahi kuwasikia kina mama wakihoji ni chama gani zaidi ya CCM ambacho wangalikipigia kura. Mmoja wao (jina kapuni) aliuliza: “ Hivi kweli bila CCM watu tunaweza kuishi?”
Ndiyo maana mimi binafsi sishangai tena kumuona kiongozi wa CCM akidumu katika nafasi ya uongozi kwa miaka chungu nzima hata kama hana jambo la maana la kuonyesha kama matunda ya uongozi wake. Kwani nimegundua kwamba  kiongozi anayewania kuchaguliwa tena na tena sio lazima apimwe kwa misingi ya mambo chanya aliyowahi kufanikisha utekelezaji wake mnamo vipindi vya awali vya  uongozi wake. Wahalifu watatu au wanne aliowasaidia wasikabiliane na mkono wa nguvu ya dola, ni mtaji wa kutosha kumuwezesha kujikusanyia kura za ushindi katika kijiji kimoja au kingine.
Nimewahi kufadhaishwa sana na matokeo ya kinyang’anyiro cha uchaguzi katika kijiji kimoja cha kwetu (jina linahifadhiwa) ambapo askari polisi mmoja mstaafu (jina kapuni) alikuwa anagombea fursa ya uongozi kwa tiketi ya chama cha upinzani. Wengi wetu ambao tuliwahi kuwa karibu na mstaafu huyo na kutambua upeo na uwezo wake, tulimuona kama lulu ambayo kijiji chetu kilikuwa kimejaliwa kuipata katika safu ya uongozi kwa ngazi hiyo.
Hatukuamini taarifa zilizotufikia baadaye kwamba askari polisi mstaafu yule alikuwa amegaragazwa vibaya na  kijana (asiyekuwa na jina kisiasa kijijini) aliyegombea kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi. Kisa? Mosi, eti askari polisi wana roho mbaya (‘ebipolisi bigil’ omwoyo gubi’); na pili, vyovyote vile mtu kama huyu angalitokea kuwa kipingamizi kikubwa kwa shughuli zao za kiuhalifu zisisizoendana na utawala wa sheria.
Kwa nini ninayaandika yote haya? Nayaandika kuwataadharisha viongozi na wakereketwa wa vyama vya Upinzani ambao wanaelekea kukumbwa na kiwewe cha imani kwamba 2015 ni mwaka wa Watanzania kushuhudia kaburi la Chama Cha Mapinduzi. Pamoja na baadhi yetu kufurahika na mtazamo huo, bado mimi naziona hizo kama ndoto za Alinacha! Na kamwe sipendi kufananishwa na mbwa mwitu ambaye alimnyemelea binadamu kwa masafa marefu hadi mlangoni kwake kwa matarajio ya kuokota mikono yake aliyoiona iko mbioni kukongoroka na kudondoka chini wakati wowote!
Hivi karibuni, wakati wa uchaguzi wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi, Mwenyekiti wa chama hicho tawala, Jakaya Mrisho Kikwete, alisikika akiwasuta na kuwakebehi Watanzania wasiokitakia CCM mema na uhai baada ya Uchaguzi Mkuu 2015, kwamba watakufa wao wenyewe na kukiacha chama hicho kikiendelea kudunda kwenye uongozi wa nchi kwa miaka mingi zaidi ijayo. Kwa hakika siifurahii kauli hiyo, lakini sipendi kuipuuza hata kidogo; kwa sababu nawafahamu vizuri Watanzania. Naona na Kikwete anawafahamu vilivyo watu wake.
Kwa baadhi yetu, ni jambo lililo dhahiri kwamba Chama Cha Mapinduzi kimejifikisha katika hatua ya udhaifu mkubwa tangu kuasisiwa kwake miaka 60 iliyopita. Na kwa vyovyote vile, hakuna namna ya kulinganisha nguvu zake leo na wakati wa miaka ya themanini, kwa mfano.
Tuchukue tukio la ‘kuchafuka kwa hali ya hewa’ kama kielelezo na kigezo cha tofauti za Chama hiki kwa nyakati hizo. Mwaka 1984, Chama Cha Mapinduzi, chini ya uongozi madhubuti wa Mwalimu Nyerere, kilidiriki kumtimua uongozi Makamu wa Kwanza wa Rais, Alhaj Aboud Jumbe. Kiongozi huyo aliondoka kwenda Dodoma akiwa ni mtu wa pili tu nchini nyuma ya Nyerere kwa madaraka, nguvu na mamlaka, lakini alirejea Zanzibar akiwa raia wa kawaida tu. Na wala hatukumsikia Rais Nyerere kumshikia bastola au chombo chochote cha moto kama tunavyoshuhudia viongozi ndani ya utawala wa CCM (kina Ismael Aden Rage, Kigwangala, n.k.) wakifanyiana hivi leo. Misimamo ya kisiasa ya Mwalimu Nyerere ilikuwa ni makombora ya nyuklia ya kung’oa na kusambaratisha milima.
Miaka miwili iliyopita, Chama Cha Mapinduzi kilitikisika vibaya kutokana na ufisadi mkubwa uliodhihirika ndani ya uongozi wake na  kutishia kuisambaratisha kabisa haiba yake machoni mwa Watanzania.
Kutokana na uchunguzi wake, Chama Cha Mapinduzi kilibaini na kukiri kwamba angalau vigogo wake watatu walikuwa vinara wa ufisadi ule hatarishi: Waziri Mkuu wa Zamani aliyejiuzuru kwa kashfa ya Rushwa ya Richmond, Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Zamani, Andrew Chenge na Mbunge wa Igunga aliyepata kuwa Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi, Rostam Aziz. Hatukupata kushuhudia vishindo vya kutimuana vya enzi za Mwalimu.
Badala yake, tulitangaziwa mradi wa Chama wa kuwatokomeza mafisadi wale, kama mkakati wake wa kujisafisha mbele ya umma. Lakinini kitu gani kimetokea hadi leo?
Ukiondoa Rostam Aziz aliyetangaza kushindwa kuendesha ‘siasa za maji taka’ na hivyo kuamua kwa hiari yake kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi, tumewashuhudia wenzake wakizidi kuchanja mbuga kwa kuendelea kushikilia nyadhifa zao zote, kama sio kuongezewa nyingine nyingi tu,  kama vile hakuna jambo lolote lililopata kutokea katika maisha yao ya kisiasa!
Lugha inayotawala anga za siasa nchini mwetu hivi sasa ni kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Haimshangazi mtu yeyote kusikia kigogo mkuu wa kashfa za Richmond akitajwa kuongoza mbio za kuwania Urais wa Tanzania katika Uchaguzi huo. Nina hakika kwamba kigogo huyo anaingia katika kinyang’anyiro hicho kwa matumaini ya kuibuka  mshindi. Nami nitakuwa Mtanzania wa mwisho kushangaa kumuona mtu huyo anaibuka na Urais wa nchi yetu! Kwa nini? Kwa sababu ninawafahamu Watanzania, ambao kura zao ndiyo nyenzo itakayomuinua kwenye kiti cha enzi cha Ikulu miaka hii michache ijayo. Mbona kapeta katika kinyang’anyiro cha uchaguzi uliopita mwaka huu wa Halmashauri Kuu ya Taifa?
Ndiyo maana kila nikimkumbuka Mzee Aboud Jumbe na Rostam Aziz, nashindwa kuelewa ni nini wanakiwaza popote walipo! Ilikuwaje wakakubali kusalimu amri kwa urahisi namna ile wakati ushindi wao ulikuwa mbioni unakuja? Labda isemwavyo ni kweli kuwa unapokaribia kukata tamaa, ndipo ukombozi wako unapokuwa kona ya mwisho kutua mbele yako!
Ninapenda kuhitimisha kwa kuwaasa wapenda mageuzi wa Tanzania kujiepusha na kiwewe cha matumaini bandia ya kifo cha Chama Cha Mapinduzi na matarajio yao ya kunyakua madaraka katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Hii sio Zambia wala Kenya ambako vyama vya UNIP na KANU vilikubali kupigwa teke kwa urahisi, kama ilivyowatokea Mzee Aboud Jumbe na Rostam Aziz wetu.
Yafaa wanamageuzi wa Tanzania wakatambua kwamba wakati wa kusherehekea mabadiliko nchini mwetu bado uko mbali sana. Na si ajabu kuwa Mwandishi wa vitabu wa Afrika Magharibi, Ayi Kwei Armah, alikuwa anatuandikia sisi Watanzania, alipokiita kitabu chake: The Beautiful Ones Are Not Yet Born.         

MDAHALO WA NELSON WA CHANYA NA HASI YA MATUMIZI YA SIMU ZA KIGANJANI NA UZOEFU WANGU KATIKA KILIMO NA BIASHARA YA ZAO LA NYANYA ENZI ZA MAREHEMU BABA YANGU BUKOBA

                                 Na  Festo  Mukerebe
Tarehe 21 Septemba, 2012 ilikuwa ni siku ya Jumamosi. Ilikuwa ni mara yangu ya pili au ya tatu kubaini mwanangu Nelson akiondoka nyumbani asubuhi na kurejea jioni. Kwa vile hiyo haikuwa ni kawaida yake tangu miaka ya awali, kuhudhuria masomo shuleni siku za Jumamosi, nilikuwa nimekwishahojiana naye kuhusu mabadiliko hayo. Naye alikuwa tayari amenipatia maelezo ya kuridhisha mintarafu mabadiliko hayo.
Hata hivyo, siku tajwa hapo juu, nilirudia kumhoji kuhusu jambo hilo hilo. Naye akanieleza kwamba kwa siku hiyo, yeye na wanafunzi wenzake wa Kidato cha Tatu na Nne, walikuwa wamealikwa kushuhudia (na kushiriki?) mdahalo wa Kidato cha Tano na Sita shuleni kwao – mdahalo uliohusu faida na hasara za kumiliki simu za mkononi. Bila shaka hoja hiyo iliwahusu na kuwalenga wanafunzi wenyewe.
Nilihisi kutaka kujua jinsi wachangiaji wa mjadala ule walivyodadavua na kujenga hoja na misimamo yao. Kwa bahati mbaya, hapa sikuambulia maelezo ya kukidhi. Maana Nelson aliishia kukumbuka mchangiaji mmoja tu aliyedai kwamba simu zina matokeo ya kuwatia umasikini wamiliki wake, kutokana na ununuzi wa kila mara wa vocha za muda wa kuwa hewani.
Maelezo hayo kiduchu yaliniongezea kiu ya kutaka kujua zaidi. Lakini kwa vile Nelson hakuelekea kuwa na cha maana zaidi kutosheleza kiu yangu, nilijikuta mimi mwenyewe sasa nashindwa kudhibiti hamu yangu ya  kuchangia mdahalo nisioalikwa, Nelson akiwa ndiyo hadhira yangu ya pekee!
Uchu wangu ulinipeleka takriban mwaka 1965. Kadiri ya kumbukumbu zangu, ambazo zimekataa kufutika kichwani hadi sasa, ni kipindi hicho Marehemu Baba yangu, kwa kushirikiana na wanaume wengine wachache kijijini kwetu, Kimbugu - Bulwani, waliasisi kilimo cha mboga mboga, hususan nyanya na kabeji – kilimo ambacho kilileta mabadiliko makubwa katika uchumi na maisha ya wanaume wale wa shoka walioshiriki kilimo kile na (sisi) familia zao.
Kwa kusema hayo, sina maana kwamba wazee wale walitajirika sana kutokana na mabadiliko hayo. Lakini naweza kusema kwa kujiamini kabisa kwamba kuanzia wakati huo, maisha ya familia zetu hayakurejea nyuma.
Mwaka ule wa 1965, kwa mfano, Baba aliweza kuboresha makazi yetu kwa kufanikiwa kujenga nyumba aina ya banda yenye kuezekwa kwa bati, badala ya tetei aliyoijenga miaka mimi nazaliwa, 1952 - 1953. Nakumbuka jinsi nilivyoshirikiana naye kusomba nguzo, mabati na maji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ile ya banda (wengi hawaelekei kulijua hilo), ambayo bado ipo hadi hii leo.
Mwaka 1966, Baba aliinyanyua juu hadhi ya familia yetu kwa kuanza kufuga ng’ombe wachache aliowamiliki mwenyewe kutokana na mapato ya biashara ya nyanya. Nakumbuka jinsi nilivyoshirikiana naye kuwaswaga ndama wawili (na wengine walioongezeka baadaye) kuwaleta nyumbani. Ndugu na jamaa zangu wengi hawaelekei kulitambua jambo hilo la kihistoria. (Au labda wanalipuuza tu kwa nia mbaya!)  
Idadi ya ng’ombe wa Baba iliongezeka taratibu sana kwa sababu ya maradhi ambayo hayakuepukika kutokana na uhaba wa taaluma stahiki katika nyanja ya ufugaji na huduma zinazohusika nayo. Wakati anaitwa kutangulia mbele ya haki, Baba yangu hakuweza kuvuka idadi ya ng’ombe 15 ambao wote waliishia mikononi mwa survivors wachache mafisadi  . Lakini ni ukweli usiopingika kwamba ng’ombe hao walimjengea hadhi kubwa (yeye na hata sisi) katika jamii, na kutupa  sisi ‘wasomi’, uhakika wa kusonga mbele shuleni.
                Lakini, kilimo cha nyanya ndicho pengine kilichotujenga zaidi kuliko kitu kingine chochote katika maisha. Huwa napenda kuamini kwamba kama kilimo hicho kingalitendeka mnamo mazingira ya miaka tuliyo nayo, basi Baba yangu asingalifariki au tukiwa masikini. Na hili hasa ndilo linaloniunganisha na mdahalo wa Nelson kuhusu hasi na chanya ya simu za kiganjani shuleni kwake.
Tangu nikiwa darasa la Tano, mwaka 1965, ‘tulilima na kulimaga… tulipanda na kupandaga’. Misitu mikubwa ya kiasili kama Nkomelo, Kyakatoto, Lubezi, Kyente, Kamusholelwa na mingineyo, iliangamia kwa mapanga, mashoka na majembe ya familia za wazee waliokuwa serious farmers (Baba yangu, Mzee Frederick Kalumuna, Mzee Paulo Bitambi, Mzee Mwamudu Hassan Kagengele, Mzee Bayubi, Mzee Celestin Lubunu, Kijana Abubakar Mwamudu na wengine wachache ambao nimewasahau). Sina hakika na hukumu ya wanaharakati wa hifadhi ya mazingira! Lakini katika hili, siwatarajii waibuke na nishani kwa ajili yetu!
Mchakato wa kilimo kile ulianza na wazee kukagua msitu unaolengwa kushughulikiwa na kufikia muafaka na wamiliki wake. Baada ya hapo, mapanga na mashoka makali yalinolewa na kufanya kazi, kabla ya familia zetu hazijapinda migongo kuutifua udongo wenye rutuba nyingi na pengine usiopata kulimwa tangu enzi za kale. Ndipo mbegu za money maker, drum head na nyinginezo ziliposihiwa katika vitalu na miche kupandwa. (Kwa bahati mbaya, sikuwahi kuona mistari inazingatiwa!). Hatua hiyo ilifuatiwa na umwagiliaji kwa kutumia keni, vidumu, karai, sufuria, vibuyu na vyombo vingine vilivyoweza kupatikana katika kaya zetu. Ilikuwa ni lazima mashamba (emisiri) yawe jirani kabisa na vyanzo vya maji (chemichemi, mito na ziwa) ili kuwezesha kazi hiyo (iliyofanyika majira ya kihangazi) kufanyika kwa ufanisi.
Mchakato wa umwagiliaji na palizi (mbili) ulifuatiwa na kazi ngumu kadhaa. Moja ya kazi hizo ilifanyika usiku, ikihusu ulinzi dhidi ya wanyama waharibifu, hasa viboko. Kazi hii ilifanywa na wazee na vijana waliokuwa na umri mkubwa. Kazi yingine ilikuwa ni kuchuma na kusomba nyanya hadi nyumbani. Pengine hii ndiyo kazi iliyotutoa jasho jingi zaidi kuliko kazi nyinginezo. Kwa maana, kama ilivyokwishadokezwa, nyumbani kwetu (pakiwa mwanzoni mwa plateau ya kwanza kutoka Ziwa Viktoria) panatenganishwa na ukanda wa pwani na safu ya  mlima mkali ambao ilibidi tuupande tukiwa na matenga mazito ya nyanya vichwani mwetu. Kwa kawaida, kazi ya kuvuna na kusomba nyanya hizo kutoka ufukweni mwa Ziwa Viktoria, ilifanyika mara mbili kwa siku.
Na hata hadi hapo, kazi ilikuwa bado ni mbichi kabisa. Maana baada ya siku kama mbili hivi, ililazimu tupakie upya nyanya hizo katika matenga na kuyabeba matenga hayo hadi barabarani Kibahoni, ambapo tuliyasetiri msituni kwa usalama. Alfajiri kesho yake, tulidamka mapema na kuyapanga barabarani, kusubiri usafiri wa mabasi yaendayo Bukoba Mjini kwa mauzo.
Kabla sijatokomea Kahororo mwaka 1968 kwa elimu ya Sekondari, niliweza kusafirisha nyanya za Baba mara mbili au tatu hivi, hivyo kuwa na uzoefu na uelewa wa kutosha kuhusu yaliyojiri baada ya basi tulilosafiria kuwasili stendi ya mabasi mjini Bukoba.
Tuliweza kuipima hali ya soko mara baada ya kuwasili stendi na kuanza kuyateremsha matenga yetu. Iwapo ulilakiwa kwa kuzongwa na umati wa wafanyabiashara ya nyanya kutoka soko kuu la mji, basi ulikuwa na kila sababu ya kuwa na faraja kwamba kulikuwa na uhaba mkubwa wa zao hilo huko sokoni na hivyo kwamba bei kwa siku hiyo ilikuwa ni nzuri. Kwa mujibu wa Marehemu Baba yangu, sasa uliweza kuiwasha sigara yako na kuivuta kwa matumaini na madaha, ukiwaachia wafanyabiashara kazi ya kushughulika na uteremshaji wa matenga.
Lakini endapo ulijikuta ukiandamwa na watoza ushuru wa halmashauri ya mji tu, basi ulilazimika kubwaga moyo kwamba siku ile soko lilikuwa tayari limefurika nyanya, hali ambayo ilikuwa na athari ya kushusha bei ya zao hilo siku hiyo. Na siku kama hiyo, wafanya biashara walicheza mchezo mchafu. Bila huruma yoyote kwa wakulima waliosafirisha mazao yao kwa gharama kubwa, walibana kutoa bei hadi jioni wakati mabasi yanaanza kurejea vijijini. Ndipo katika kiwewe cha kuachwa na mabasi hayo, wakulima hawakuwa na jinsi yoyote ile bali kuuza mazao yao kwa bei ya kutupa! (Sikuona waliokuwa na ndugu au jamaa wa kufikia mjini Bukoba).
Kinasimuliwa kisa cha mzee Celestin Lubunu ( huyu aliwahi kupigana vita ya pili ya dunia, akiwa askari katika jeshi la kikoloni la Waingereza nchini, King’s African Rifles, ambaye hakuwa tayari kuzikubali kirahisi nyanyaso za wafanya biashara wa sokoni. Tofauti na baadhi ya wakulima wenzake waliolazimika kuzimwaga jalalani nyanya zao zilizokosa soko, Mzee Celestin alifanya hivyo baada ya kuzipondaponda na kuzichanganya na uchafu. Alikuwa amegundua kwamba baada yawaokuondoka, wafanya biashara wajanja walikuwa wanachakura majalala na kuziokota nyanya zilizotupwa humo, na kisha kuziosha kwa maji,  ili kesho yake wazifanyie biashara safi kama kawaida, bila kugharamika nazo kwa lolote!
Endapo mawasiliano ya simu za mkononi yangalikuwa tayari yamevumbuliwa enzi hizo, madhila yote hayo yasingeliwakuta kina Baba na wakulima wenzake masikini. Wangaliweza kuitathmini hali ya soko kila siku kabla ya kusumbuka na usafirishaji wa ‘mzigo’ mzito, hadi hali ya soko itulie au itoe bei yenye tija zaidi. Vyovyote vile, wangaligharamika kidogo kwa kununua vocha za muda wa maongezi hewani. Lakini manufaa ya kufanya hivyo, yangalikuwa makubwa sana kuliko hasara waliyoipata kutokana na ukosefu wa mawasiliano hayo.
Hadi wanaaga dunia, nina hakika kwamba baadhi ya wale wazee, kama sio wote, wangalikuwa wakimiliki hata vyombo vya moto kama vile pick-up au malori na outboard engines kwa ajili ya kusafirisha matenga ya nyanya na magunia ya kabeji hadi masoko makubwa zaidi ya miji ya mbali kama Mwanza, Shinyanga na Tabora. Si ni dhahiri kwamba kwao umasikini ungalikuwa bye bye? And why not?      


MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NA MATISHIO YAKE YA KUKIFUTA CHADEMA KATIKA DAFTARI LAKE.

                            Na  Festo  Mukerebe

Pengine kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, Watanzania hivi karibuni tulishuhudia mauaji ya mwandishi wa habari za luninga wa Channel Ten, David Mwangosi, huko Nyololo, Mufindi, Iringa. Inasadikiwa kwamba Mwangosi alikuwa amekwenda katika Kijiji cha Nyololo kufuatilia taarifa za kukamatwa kwa mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe, ambaye alikuwa ametiwa mbaroni na jeshi la polisi huko huko Mkoani Iringa.
Mzizi na chanzo cha tukio hilo ni sherehe za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) za uzinduzi wa ofisi ya tawi lake jipya, ambazo chama tawala, C.C.M., kilikerwa kuona jinsi zilivyovutia waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari kuziwekea kumbukumbu.
Hukumu ya kifo cha Mwangosi, ilitolewa na askari mmoja wa cheo cha chini katika jeshi la polisi, aliyeamua kumaliza udhia kwa kumlipua kwa bomu Mwangosi sehemu ya tumbo lake. Kitendo hicho kilifanyika baada ya kushirikiana na askari polisi wengine, wasiopungua saba (kwa mujibu wa picha zilizochukuliwa wakati tukio hilo likiwa linaendelea) kumzonga Mwangosi na kudhibiti harakati zake za kuchukua picha za hali halisi ya mambo ilivyokuwa katika eneo lile, huku Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Mchael Kamuhanda, akisemekana kuwapo kushuhudia (na kuamuru?) mauaji hayo!
Sio madhumuni yangu kulijadili kwa undani tukio hili, kwani naamini kwamba tayari liko Mahakamani. Isitoshe, tumezoea kuzuiwa kuyajadili matukio kama hayo kwa mantiki na msingi kwamba yamefikishwa Mahakamani. Kila kukicha,  tunaambiwa kuwa kufanya hivyo, ni kinyume kabisa cha matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!
Kwani ni mara ngapi mwaka huu tumeshuhudia marufuku hii ikitamkwa kwa ukali na msisitizo mkubwa na serikali, hususan Bungeni? Migomo ya Madaktari na Walimu ilizuiliwa kabisa hata kuzungumzwa tu katika vikao vya Bunge la Bajeti, kwa maelezo ya kuwa kwake tayari mbele ya Mahakama. Tumeambiwa mara nyingi kwamba, Mahakama, kama mmoja wa Mihimili yetu ya dola,  si ruhusa kwa Mihimili miwili mingine ya Bunge na Serikali, kuingilia mambo yake!
Shida iliyonisukuma kuandika makala hii, haina uhusiano wa moja kwa moja na mantiki ya kanuni hiyo. Jambo linalosumbua kichwa changu ni kauli na vitisho  vya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji John Tendwa, kwamba hatasita kukifuta katika Daftari lake, Chama chochote cha siasa, ambacho mkutano wake wa kisiasa utapelekea kutokea kwa mauaji.
Kimsingi, naunga mkono msimamo mkali wa Msajili, kwani matukio ya mauaji katika nchi yetu yameongezeka kwa kasi mnamo miaka ya karibuni; na kwa vyovyote vile, hali hiyo ya upotevu wa uhai wa raia wa nchi hii wasiokuwa na hatia, haiwezi kuendelea kuvumiliwa zaidi.
Wasiwasi wangu ni ubavu wa Msajili kuitekeleza kwa ufanisi na bila upendeleo wowote, azma yake hiyo ya kujitutumua. Hadi sasa, mauaji mengi yamefanywa na jeshi la polisi, likiwa katika harakati za kudhibiti maandamano na mikutano ya Vyama vya Upinzani, hususan CHADEMA na CUF. Binafsi sijawahi kusikia jeshi la polisi likipambana na Chama Tawala, CCM, wakati wa mikutano na maandamano yaliyoandaliwa na Chama hicho.
Nitaikubali shingo upande hoja kwamba Chama Cha Mapinduzi, C.C.M., ni chama chenye maadili na nidhamu ya hali ya juu sana, kiasi kwamba chenyewe kamwe hakivunji au kukiuka kanuni na taratibu za mikutano na maandamano, kama zilivyowekwa na mamlaka husika.
Lakini napata taabu zaidi kuamini nidhamu hiyo, hasa ninapofuatilia mwenendo wa baadhi ya wanasiasa waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi, wanapokuwa wakichangia mijadala Bungeni au kuhutubia mikutano ya kampeni za chaguzi ndogo majimboni. Sikusudii hapa kuwataja kwa majina viongozi hao. Lakini Watanzania wengi wana macho na bongo nzuri. Fumbo mfumbie mjinga!
Sambamba na hali hiyo, najiuliza kama atakuwapo mwamuzi asiyefungamana na upande wowote, atakayepitisha hukumu ya haki ya nani  mwenye kutimiza vigezo vyote vya nidhamu inayokubalika kuhusiana na uendeshaji wa mikutano na maandamano yenye ushindani mkali wa kisiasa, kuelekea 2015.
Hivi kweli wanaweza kuwa ni watendaji wateule wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, sampuli ya Jaji Tendwa? Na kama watendaji hawa wataamua, kwa maslahi ya ajira zao nono, kukibeba Chama cha mrengo wao, na kuvikata ndimi na kauli vyama vyenye upinzani mkubwa kwao, ni nani atasimama kuvisemea na kuvitetea hivyo vyama vya upinzani? Kweli vitakuwa salama? Ah wapi!
Nina hakika kwamba C.C.M. kikiamua kuasisi ghasia  fujo na machafuko katika mikutano na maandamano ya vyama wasivyovipenda, Msajili hatasita kuitekeleza azma yake kwa kukifuta chama husika. Huenda sasa anajenga mazingira ya kufanya hivyo mbele ya safari.
Lakini endapo CHADEMA nacho, kwa mfano, kikianzisha fujo za aina hiyo kwenye mikutano au maandamano ya Chama Cha Mapinduzi, hivi kweli tuamini kwamba Jaji Tendwa  atakuwa na satwa, utashi na ubavu wa kukifuta Chama hicho Tawala katika Daftari lake? Thubutu! Akale wapi?
Ushauri wangu wa bure kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, ni kwamba awe muangalifu na makini sana katika utekelezaji wa matishio yake. Asipofanya hivyo, asishangae kujikuta anapelekea nchi yetu kuingia katika machafuko na vita ya wenyewe kwa wenyewe, kama tulivyoshuhudia katika mataifa mengine ya Afrika, hususan Misri, Libya na Tunisia. Kwa maana mimi sioni jinsi vyama vya upinzani vyente ufuasi mkubwa katika umma wa nchi yetu, vitakavyokuwa tayari kufutiwa usajili wake kirahisi na kwa mbinu za ujanja ujanja; na bado vikubali kukaa kimya mithili ya kondoo anayepelekwa machinjioni. Lazima vitapambana tu. Chonde chonde Msajili wetu, atuepushe na zahma hiyo!  
Lakini lipo jambo jingine linalohusiana na hili, linalonitia mashaka makubwa. Baada ya matukio ya mauaji ya kisiasa yaliyotekelezwa na Jeshi la Polisi huko Morogoro na Iringa mwaka huu, achilia mbali matukio ya mengine kama hayo huko Arusha, Tarime, Songea, Igunga, Aru Meru, n.k., Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, amesikika akimshangaa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP, Saidi Mwema, kwa kuchelewa kumkamata na kumtia ndani mara moja, Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa.
Kisa nini, ati? Eti Dk. Slaa aliwahi kumtumia Kamanda Mwema ujumbe mfupi wa simu akitahadharisha kuhusu kuibuka na kuenea kwa wimbi hatarishi la mauaji ya kisiasa nchini. Sasa kwa vile mauaji ya mwandishi wa habari Mwangosi, yalitokea siku chache baada ya ujumbe huo, basi Dk. Slaa alikuwa ni injinia mkuu wa mauaji hayo! Na hivyo, alistahili kutiwa kitanzi! Ebo! Hivi kweli Waziri Nchimbi hajawahi kusikia au kuelewa mantiki ya msemo wa wahenga kwamba: “Tarishi hauawi”.
Vinginevyo, Waziri asingaliweza kuyahusisha kirahisi mambo hayo mawili tofauti - mauaji ya Mwangosi na ujumbe wa Dk. Slaa kwa IGP. Mbona Waziri haonyeshi hata dalili tu ya kupepesa kope kwa kuwaona Kamanda Kamuhanda na askari aliyemfumua kwa ukatili wa kutisha mwandishi Mwangosi wakiendelea kupeta mitaani, wakiwa huru kazini mwao, utadhani marehemu Mwangosi hakuwa ‘mtu kitu’. Sijui tutaendelea hadi lini kujiuliza kama askari muuaji alikuwa anatekeleza amri ya Kamanda wake, au aliamua tu kwa ridhaa yake mwenyewe kumpoka uhai mwandishi wa habari. Na tusubiri miezi ijayo taarifa za hizo tume lukuki zilizoundwa na waheshimiwa kutuambia kulikoni!
Kwa mbali, mimi naweza kumuona Waziri Nchimbi akijaribu kulinusuru jeshi lake la polisi, kama sio kujinusuru yeye mwenyewe, akiwa bosi mkuu wa jeshi hilo nchini; lakini  tafakuri ndogo tu inanituma nimuone Waziri akigonga mwamba kwa kishindo katika kadhia hii.
Kwa kuhitimisha makala hii, mimi ningelidhani kwamba wakati ulikuwa unatishia kukipita Chama Cha Mapinduzi, makada wake wababe (kina Mwigulu Nchemba, Livingstone Lusinde, John Tendwa na wengineo kama Ismael Aden Rage mwenye kudiriki kutembea na silaha ya moto kiunoni hadharani). Kama kweli wanakitakia maisha mema Chama chao, CCM,  baada ya 2015, wangelishaurika kurudi haraka kwenye drawing boards za mikakati.
Ni kwa manufaa ya makada na washabiki wa Chama cha Mapinduzi kutambua kwamba shida kuu ya Watanzania, ni maisha bora ya kweli. Haijalishi hata wakiletewa na shetani maisha hayo

MOVEMENT FOR CHANGE, M4C, VUA GAMBA VAA GWANDA, MABADILIKO MANNE CHANYA, OPERESHENI SANGARA; VISION FOR CHANGE, MCHAKAMCHAKA HADI 2015;  MISSION FOR CHANGE;  ARI ZAIDI, NGUVU ZAIDI NA KASI ZAIDI, MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA;… WATANZANIA TUNA KAZI KUELEKEA 2015.

                                    Na  Festo Mukerebe

Mwaka 1960, Waziri Mkuu wa Uingereza (Macmillan?), alizungumzia kile alichokielezea kama ‘Kimbunga cha Mabadiliko Barani Afrika’ (“The wind of change”, alisema “is blowing across Africa”. Makoloni kama India yalikuwa tayari yamefanikiwa kujipatia uhuru (1948); na mengine, yakiwemo ya Afrika, yalikuwa hayako tayari kuendelea kutawaliwa na kudhibitiwa na mataifa ya Ulaya. Kuanzia wakati huo, Mabadiliko makubwa yalikuwa hayawezi kuepukika tena.
Mwaka 2008, mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Democrat, mweusi Barak Obama, aliitumia kwa mafanikio makubwa Kauli-mbiu (au slogan) ya Mabadiliko,Change, kuingia Ikulu, huku akiwahamasisha Wamarekani kuamini katika uwezo wake wa kuinasua nchi hiyo kutokana na madhila mbalimbali waliyoletewa na utawala ‘mbaya’ wa Rais wa tiketi ya chama cha Republican aliyemtangulia, George Bush. “Yes we can”, aliwahakikishia na kuwashawishi wapiga kura hadi kuamua kumsabilia uongozi wa taifa hilo kubwa ulimwenguni. Baada ya karne nyingi za udhalimu na ukandamizaji, enzi za dharau kwa mtu mweusi, zilikuwa hatimaye zimefikia tamati na kutokomea.
Miaka ya karibuni, Tanzania imeshuhudia kimbunga cha Kauli-mbiu za Mabadiliko katika medani za siasa za chaguzi za vyama vingi . Tulianza kuzisikia Kauli-mbiu hizi wakati wa kampeni za Urais za kipindi cha kwanza cha Awamu ya Nne, ambapo Chama Cha Mapinduzi (C.C.M.) kiliibuka na “Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya” (ANGUKA) na “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania”.
Kutokana na ufanisi kiduchu uliopatikana katika miaka mitano ya kipindi cha kwanza cha utawala wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kauli-mbinu hizo hizo zilifanyiwa  ukarabati kusudi wananchi waendelee kuamini  kwamba C.C.M bado kinaweza!. Kauli-mbiu ya “ANGUKA”, kwa mfano, ikakolezwa kwa nyongeza ya neno ‘ZAIDI’- “ Ari Zaidi, Nguvu Zaidi na Kasi Zaidi”. Tatizo la C.C.M. hapa ni kutambua, bila kuwa na la maana la kufanya, kwamba mahasimu wake wanakisuta kwa kukiita “Chama cha ANGUKA ZAIDI”!
Siku za hivi karibuni, vyama vingine vya siasa navyo vimezinduka na kuona kuwa haiba zake hazikamiliki bila kubuni na kusanifu kauli-mbiu zenye ushindani katika soko la mvuto na haiba kwa Watanzania wanaoandaliwa kwa kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wamekuja na “Vuguvugu la Mabadiliko”, maarufu kama “Movement for Change”. Wakati mwingine, kauli-mbiu hii inatiwa kionjo kwa kuitwa “Mabadiliko Manne Chanya” au “M4C”.
Chama cha Wananchi (CUF), hakikukubali kuachwa nyuma katika mkumbo huu mpya wa Mabadiliko. Kichekwe? Chenyewe kimeibuka na Kauli-mbiu za “Vision for Change” na “Mchakamchaka Hadi 2015”. Sina hakika zilikoishia Kauli-mbiu zake za awali za “Ngangari” na “Haki Sawa Kwa Wote”.
Nacho SAU kinasemekana kuwa mbioni, si muda mrefu ujao, kuzindua kauli-mbiu ya “Mission for Change”.
Kwa rekodi iliyofikiwa hadi sasa, hapana shaka kwamba orodha ya Kauli-mbiu hizi itakuwa ndefu zaidi kadiri siku zinavyokatika kuelekea kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu, mwaka 2015.
Binafsi, sina tatizo na harakati hizi za ushindanishi wa Kauli-mbiu za vyama katika mbio za kujinadi na kujigamba mbele ya Watanzania, ambao muda si Miaka mingi  ijayo, watakuwa wakimiliki tena nguvu ya turufu (veto) kuhusu mustakabali wa utawala wa nchi yetu, fursa ambayo huwajia mara moja katika kila miaka mitano, kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu.
Shida yangu ni mantiki ya msemo wa Kiswahili usemao: “ Miluzi mingi huwapoteza mbwa”. Maana sina hakika na uwezo wa Watanzania tulio wengi kuzipembua na kuzipambanua kwa “ukweli na uwazi” kauli - mbiu zote hizi, achilia mbali na kuzihusisha na hali halisi ya utendaji wa vyama vyetu, ili tuweze hatimaye kufanya maamuzi chanya, hekima na busara (informed decisions), come 2015, for our own fate and betterment. Mungu Ibariki Tanzania.

OKUHA:  THE CULTURE OF GIVING AMONG THE HAYA
OF NORTH - WESTERN TANZANIA

                     Na  Festo  Mukerebe

Mnamo miaka ya 1980, niliandika makala ya Kiingereza yenye somo hilo hapo juu. Hivi karibuni, wakati naandika makala kuhusu baadhi ya mila na desturi za Wahaya zinazohitaji mtazamo mpya katika zama tulizo nazo leo, nimeikumbuka sana makala ile ya Kiingereza. Lakini kutokana na kutokukumbuka wapi nilizihifadhi nakala za makala ile, nikabaki kutumaini kuiona siku moja ili niweze kuisoma tena na, hali ikiruhusu, niweze kuifanyia rejea (Revisit) na kuipanua kwa kuipa mtazamo wangu wa kipindi tulicho nacho sasa.
Hata hivyo, wakati nasubiri ‘kuivumbua’ upya makala hiyo, nimejisikia kuandika, japo kidogo tu, kuhusu utamaduni wa ‘upaji’ miongoni mwa Wahaya Mkoani Kagera.
Siwezi kudai kuifanyia utafiti wa kina sana dhana hiyo ya ‘upaji’ ambayo ndiyo okuha, miongoni mwa Wahaya. Lakini hilo haliwezi kuwa sababu toshelezi ya kunizuia kuijadili kwa kutumia uzoefu wangu wa miaka mingi kiasi kama mwanajamii husika.
Umuhimu wa okuha, hauhitaji kupigiwa kinubi wala baragumu. Upana wake, kama msamiati, unatosha kutuonyesha jinsi okuha kulivyokuwa ni tunu inayothaminiwa sana katika utamaduni wa Wahaya. Kwa hakika, okuha ni dhana ambayo haina mshindani katika ‘kamusi ya Kihaya’ kwa wingi wa maana zake mbalimbali, ambazo baadhi yake zinaendelea kusikika zikitumiwa hadi leo.
Pamoja na kutokuwa gwiji wa lugha ya Kihaya, mimi binafsi nimeweza kukusanya maana zisizopungua dazeni kuhusiana na maana hizo. Kwa kuzitaja tu, maana hizo ni pamoja na okutangilila, okutwela, okukulata, okulongola, okuganuza, okugabila, okugaba, okubegela, okushalila, okuzilima, okubisila, okuhonga, okutekela, okulozya, okubegana, okueleza, na hata okuhao. Inawezekana kuwa yapo maneno mengine ya Kihaya yenye msamiati mpana kama hilo la okuha, lakini ninaamini kwamba yatakuwa ni machache sana.
Mbali na vitenzi nilivyoweza kuviorodhesha hapo juu na kuvihusisha na ‘kutoa’ tunu fulani zipelekwe au kuhamishiwa kwa mtu, ukoo, tabaka au watu wengine, vipo vitenzi ambavyo, japo sio kwa ukaribu wa kiwango cha uwazi, vinaweza kunyumbuliwa na kujenga taswira isiyokuwa mbali na dhana ya upaji. Kwa mfano, okulela maana yake ni kulea. Ni wazi kwamba muktadha wa neno hilo unaonekana zaidi katika mwelekeo wa upaji, okuha.
Hii ni kwa sababu kulea au kuhudumia, ni kitendo kinachohusiana kwa karibu na kutjiolea muda,  raslimali na mapenzi kwa mtu mwingine aliye na hali ya kupungikiwa au kutindikiwa na amali fulani katika maisha yake. Mwisho wa siku, kusema kweli, kulea ni kumpa mtu kitu ambacho kukikosa kwake kitu hicho kungelimsababishia mlengwa unyonge na mapungufu kiafya au kumpotezea maisha kabisa.  Hebu tulithibitishe jambo hili kwa mifano michache zaidi.
·         Okukulata:

Enzi za jadi, wakati bado mfumo wa kitabaka wa ukabaila (feudalism) bado unatawala katika jamii ya Wahaya, raia wa hadhi ya chini, yaani abailu (watwana), walilazimika kuwasilisha kwa watawala wao, sehemu ya mavuno ya kilimo na mazao ya mifugo. Mila hiyo ya kujinyenyekeza au kujipendekeza, ilijulikana kama okukulata. Kwa maana hiyo, sehemu ya mali iliyopatikana kwa jasho la watwana ilihamishwa bila shurti dhahiri na kupelekwa kwa mtawala, kwa matarajio kwamba mtawala naye angaliweza kumtunukia (kumulongola, kumugabila au kumutunga) shamba au mifugo mtwana aliyewasilisha.
Japokuwa hali hiyo inaonyesha  dhana ya ‘unequal exchange’ au ‘labour exploitation’ ilivyofanya kazi kuneemesha tabaka la mabwana, bado tunaona jinsi pande mbili zilivyopeana raslimali na kubadilishana tunu nyinginezo chini ya mfumo wa utawala wa kitabaka uliokuwepo.
  
·         Okuzilima:
Okuzilima ni kitendo kilichohusisha sherehe ya kijamii, ambacho kwacho  familia ya wazazi wa bibi harusi ilikusanya kwa njia ya michango (okutweza) na kupeleka mali (kuzilima), hasa mikungu ya ndizi (ebitoke) na vibuyu vya pombe (amalwa), kwa familia ambako binti yao ameolewa (chini ya mwavuli wa kumzawadia binti yao). Ni wazi kwamba mila hii  ilikuza na kuimarisha mahusiano mema na maelewano ya upendo baina ya familia mbili zilizooleana.
Aidha, mila hii pia ilisaidia kujenga mshikamano katika jamii pana ya  kijiji au ukoo, kwani watu wote walialikwa na kupata fursa ya kushiriki mchakato wa sherehe kwa michango yao ya hali na mali. Kuchangia huko ndiko okutwela, wakati kuchangisha au kuhamasisha michango ni  okutweza.
Kwa mfano watu waliweza kuchangia mikungu ya ndizi(ebitoke n’enkundi) ili kukidhi mahitaji ya zawadi, na chakula na pombe kwa ajili ya washiriki. ‘Siku ya Siku’, watu wengine, hasa vijana, walialikwa na kushirikishwa katika misafara ya kubeba zawadi husika. Misafara hiyo ilipambwa na kukolezwa kwa  shamrashamra ya sherehe za ngoma na nyimbo (ebizina). Siku hizi, fedha zinatumika zaidi katika kufanikisha mchakato wa mila hii.

·         Okubega:
Okubega au okubegela ni mila iliyotekelezwa na Wahaya katika ngazi ya kaya, hususan wakati wanafamilia wanajipatia mlo wao. Vitendo vya okubega viliimarisha upendo katika kaya na kuwatia hamasa wanakaya walioonyesha nidhamu, uadilifu, utiifu na utendaji bora wa majukumu.
Japokuwa hapakuwepo na mipaka maalumu kuhusu nani ampe nani zawadi ya kitoweo (omukubi) kama ishara ya shukrani au pongezi kwa tabia nzuri, adabu na utendaji uliotukuka, ni watu wa rika andamizi zaidi ndani ya kaya (hasa bibi), walioidhibiti zaidi mila hii ya okubega.
Kwa kawaida, kitoweo  (samaki, nyama au maziwa) kiligawiwa katika utaratibu wa hatua kadhaa. Katika hatua ya awali, bibi (mgawaji wa mafungu ya kitoweo) alimgawia kila mwanakaya fungu lake stahiki, kulingana na rika au hadhi yake ndani ya kaya.  Kadiri mlo ulivyoendelea, alifanya mgawo mwingine mdogo. Kwa kawaida, mgawo  huu nao uliwahusisha karibu watu wote wa kaya waliojumuika pamoja kwa chakula.
Lakini kulikuwapo na hatua nyingine zaidi, iliyohusu ugawaji wa fungu maalum ambalo bibi alikuwa amelitenga kando kwa madhumuni ya kuligawa kama tuzo kwa kuzingatia vigezo na sifa maalum. Mara nyingi, utoaji wa mgao huu wa ziada uliandamana na maneno ya  kukaripia, kusifia, kuhimiza, kufundisha, kuonya, kuadabisha, kuhamasisha na kuelekeza.

·         Okulongola:
Okulongola, ni kitendo cha hiari alichokifanya mtu kwa kusudi la kumuonyesha mwenzake jinsi alivyoridhishwa na kitendo kingine ambacho yeye mwenyewe alipata kutendewa huko nyuma. Waingereza hukiita kitendo kama hicho reciprocity. Sisi hatuwezi kukosea kukiita Nipe - Nikupe. Ni kitendo cha kurudisha fadhila.
Mfano mzuri hapa, ni mila nyingine ya Kihaya, ambayo kwayo mwanamke hutoka na kwenda porini (wakati wa msimu wa musenene) na kukamata senene kwa ajili ya mumewe. Baada ya kuwaandaa wale senene na kuwawasilisha kwa mumewe kwa wakati muafaka, hutazamiwa mume naye aonyeshe kufurahi na kuridhishwa na juhudi za mkewe, kwa kumnunulia mkewe zawadi maalum, hususan doti ya kitenge au khanga. Akifanya hivyo, anakuwa ametekeleza mila ya okulongola. Mambo yalikuwa vivyo hivyo kwa maswahiba walioshibana.

·         Okutangilila
Katikanchi ya Wahaya’ (Buhaya), pengine hakuna mila ambayo imeenea na kuzingatiwa zaidi kuliko Okutangilila. Huwezi kuingia katika mji wa Muhaya ukatoka bila kutangililwa, yaani kulakiwa kwa kahawa au pombe, kama ishara ya ukarimu na upendo. Hata awe masikini kiasi gani, Muhaya atafanya juhudi kubwa kuhakikisha anaweka nyumbani kwake akiba ya kahawa (emwani) za kutafuna kwa ajili ya wageni wanaoweza kumfikia hata bila taarifa; haijalishi wageni hao wanatoka masafa ya mbali au karibu.
Kaya masikini iliyotembelewa na mgeni inaweza kutindikiwa na huduma nyingine yoyote, ikiwa ni pamoja na kitoweo, kiasi cha mgeni huyo kulazimika kula chakula ‘maluma’, jambo ambalo ni fedheha ya kutosha kwa mwenyeji, lakini kahawa ya mgeni kutafuna itapatikana tu, japo iwe nusu ya kibaba. Miaka hii, pombe, hasa gongo (enkonyagi), inatumika zaidi kukidhi haja, lakini mila inakuwa timilifu ikihusisha pia kahawa za kutafuna.

·         Okubisila
Okubisila ni mila ya kujiandaa kwa mapokezi ya wageni mashuhuri, hata wale ambao hawakutaarifu mapema kuhusu ujio wao. Maandalizi hayo yanahusiana moja kwa moja na kahawa za kutafuna pamoja na pombe, kama ilivyoelezwa hapo juu, chini ya kipengele cha okutangilila.
Lakini katika mazingira ya magonjwa haribifu ya migomba (kama ‘mnyauko’) na  kupungua sana miaka hii kwa zao kuu la ndizi kama chakula, Muhaya atabangaiza kuishi kwa kula mazao ya nafaka na mizizi (mihogo, viazi, magimbi, n.k- vyakula vya misimu (emyaka) visivyokuwa na hadhi kubwa kama ndizi, au vyakula vya kununua madukani (unga wa mahindi na mchele), ili mradi tu ahakikishe hakosi mikungu michache ya ndizi shambani mwake kwa ajili ya mgeni anayeweza kujitokeza wakati wowote.
‘Vyakula’ vinavyopatikana kwa msimu kama senene, huhifadhiwa maalum kwa ajili ya kukidhi mila hii. Na hakuna kitendo chochote cha heshima kubwa zaidi anachoweza kufanyiwa mgeni, kuliko kukarimiwa kwa senene. Labda tutoe mfano mmoja kuthibitisha thamani ya senene kwa Wahaya. Mwanamke ambaye mumewe amefungwa jela kwa miaka kadhaa, atafanya kosa linaloweza kuhatarisha ndoa yake asipochukuwa tahadhari ya kujiandaa kuwasilisha malimbikizo ya senene aliowahifadhi mnamo misimu iliyomkuta mumewe akiwa kifungoni!
Na kama tulivyoona awali, akifanya hivyo, atastahili ‘kulongolwa’ na huyo mumewe aliyerejea kutoka jela.

·         Okuhonga
Katika maana yake ya kiasili, Okuhonga katika jamii ya Wahaya, hakukuhusiana na kutoa rushwa, kufanya vitendo vya kifisadi au kununua mapenzi ya mwanamke. Enzi kabla ya ujio wa Wazungu walioleta na kutupandikizia imani na taratibu zao za kumuabudu, kumcha na kumtukuza Mungu, nasi Waafrika tulikuwa na taratibu zetu za kuwaenzi miungu yetu.
Okuhonga, kulikuwa ni utaratibu wa kuwatolea miungu sadaka na zawadi mbalimbali ili iwapendeze kututunuku baraka na kutujalia neema na rehema tele katika maisha yetu ya kila siku. Na katika jambo hili, Waafrika hatukutofautiana sana na Wazungu wa Ulaya, karne za kale (eila lya kalanda).
 Miungu ya Wahaya, ilikuwa ni pamoja na kasi (mungu wa ardhi na kilimo), ilungu (mungu wa nyika na wanyamapori), lyangombe (mungu wa mifugo, hasa ng’ombe), mugasha (mungu wa Ziwa Lweru- Victoria), nyakalembe, (mungu wa ustawi wa wanawake na mambo ya uzazi), n.k.
Katika Agano la Kale, tunasoma sana habari za dhabihu na matambiko ya kuchoma na kuteketeza kwa ajili ya Mungu? Wahenga wetu nao hawakuwa mbali katika kuwatambikia miungu yao ili iwajalie neema walizozihitaji ili kukidhi shida zao lukuki maishani mwao na kuondokana na maangamizi yaliyowazinga? Na ndiyo tunavyofanya hata sisi leo, chini ya madhehebu yetu mbalimbali - kwa kutoa zaka na sadaka kwa ajili ya kusifu na kushukuru ? Kimsingi, ni dhana ile ile?
Kwa kuhitimisha maelezo haya ya utoaji na upaji kwa ajili ya miungu, okuhonga, Wahaya hawakukosa kukiri imani yao katika uweza wa miungu hao.  Kila walipobanwa na matatizo na kuelekea kukosa suluhu ya kutokea, walisikika wakiungama na kujinyenyekeza: “ tubihongele mukama mungu”.   
                Maelezo ya mifano hiyo hapo juu, yatoshe kuonyesha jinsi utamaduni wa Kihaya ulivyosheheni  utajiri mkubwa katika nyanja ya ukarimu na upaji, okuha.

“SIZITAKI, MBICHI HIZI” NA UTALII WA NDANI TANZANIA

                           Na  Festo  Mukerebe

Wiki hii ninapoandika makala hii, nimeona vipindi vitatu vya luninga ambavyo naamini vililenga kufanya promosheni ya Utalii wa Ndani nchini. Sijui kwa nini vipindi hivyo  vimerushwa kwa mfuatano katika wiki moja hii; na wala sihitaji sana kujua sababu yake.
Jambo moja limenipa msukumo wa kuandika makala hii. Siku nilipoyafuatilia mahojiano katika mojawapo ya vipindi hivyo, Uchumi Leo, nilijikuta naishirikisha familia yangu kujibu swali muhimu lililojitokeza: kwa nini Watanzania hatupendi kutoka kwa ziara za utalii ndani ya nchi yetu? Sikupata jibu la hakika kwa swali hilo.
Hata hivyo, nilibaini wazi kwamba utalii si jambo la kipaumbele katika familia yangu. Na kwa namna fulani, nilijikuta hofu niliyokuwa nayo awali inayeyuka kama barafu iliyoachwa nje kwenye jua la kiangazi. Nilikuwa nimetarajia kwamba baada ya hamasa nzito iliyokuwa ikitolewa na CEO wa taasisi ya Dar Tourism, pengine familia ingalinisakama na kutaka niiandalie ziara ya utalii wa ndani.
Nilishangaa kusikia wanayabeza mengi yaliyozungumzwa na kuelezwa na CEO kama manufaa ya ziara kama hizo. Mke wangu, kwa mfano, alieleza wazi wazi jinsi ambavyo hayuko tayari kutumia muda wake kwa shughuli za kitalii hapa jijini Dar es Salaam. Ni dhahiri kwamba CEO wa Dar Tourism, alikuwa hakumkonga moyo pale alipohimiza watu watoke kwenda kutembelea sehemu kama vile Mnazi Mmoja ili kuona miti iliyopandwa na viongozi mashuhuri wa bara la Afrika, kama vile Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda na Hayati Samora Machel, Rais wa zamani wa Msumbiji. Sikuwaona kuvutiwa kabisa na wazo lile.
Mwanangu mmoja ndiye alitia fora. Yeye hakuwa na imani hasa na utalii wa maeneo ya kihistoria. Alielekea kuyaona maeneo hayo kama mambo ya uongo na ya kuunda tu, kwa sababu za kibiashara na kiuchumi tu.
Japo na mimi sina shauku kubwa katika nyanja ya utalii, nilijitoa mhanga kuweka sawa mambo mbalimbali kuhusu utalii, na kujibu hoja za wenzangu nilizoziona zimepogoka kupitiliza.
Nianze na hoja ya kutembelea miti iliyopandwa na watu mashuhuri kihistoria. Niliwaeleza, kwa mfano, jinsi wenzetu wa mataifa yaliyoendelea wanavyoenzi viongozi wao wa zamani, kwa kutunza na kuhifadhi vielelezo vinavyogusa maisha yao (viongozi). Ikiwa waliwahi kupanda miti, miti hiyo itatunzwa kwa miaka mingi iwezekanavyo, hata karne kadhaa. Labda sio watu wengi wanaoweza kuamini kwamba ipo miti inayoweza kudumu hata kwa zaidi ya miaka elfu. Mfano mmoja ni miti aina ya mizeituni aliyoishuhudia muasisi wa Ukristo, Bwana Yesu Kristo katika bustani alimofanyia maombi yake ya mwisho, zaidi ya miaka 2,000 iliyopita!
Tulipokuwa katika ziara ya kiserikali nchini Finland, mwaka 1978 (nikiwa nimefuatana na kina Anne Semamba Makinda, Anselm Odhiambo Anacleti, Andrew Kiondo, Mama Mariam Abubakar na mwingine ninayemsahau), tulitembezwa jijini Helsinki na kuonyeshwa vielelezo vya kihistoria na kiutalii vya jiji hilo. Miongoni mwa vielelezo hivyo, ni miti iliyopandwa enzi za kale na viongozi mashuhuri wa nchi hiyo (kama vile Jemedari Mannelheim). Namkumbuka mama wa makamo (professional guide) aliyekuwa akitutembeza na kutupa maelezo fasaha  kuhusu kila kitu unachoweza kukifikiria - jengo, mti, sanamu, mtaa - alivyokuwa akituhamasisha kwa kauli-mbiu aliyopenda kuitamka: “look at thisthis is wonderful, absolutely wonderful”.
Aidha, niliwaeleza habari za vielelezo na vivutio vya kitalii na kihistoria vya Bagamoyo. Niliwajuza kuhusu Profesa Kajeli na uwezo wake mkubwa aliokuwa nao wa kuidadavua na kuielezea kwa ufasaha historia ya mji wa Bagamoyo. (Nimepata kumfananisha Kajeli na marehemu baba yangu mdogo, Ta Erasto, kwa maana ya sura na uwezo wa kueleza mambo na matukio).
Niliwaeleza pia kuhusu vituo vya makumbusho ambamo kumbukumbu mbalimbali za kihisoria na kiutamaduni zinahifadhiwa. Kwa kutoa mfano, nilitaja makumbusho ya Kalenga, Iringa, niliyopata kuitembelea miaka ya nyuma. Katika makumbusho ile, fuvu la shujaa, Mtwa Mkwawa Mkwavinyika linahifadhiwa, ikiwa ni sehemu ya historia ya kutukuka ya mapambano ya kabila la Wahehe dhidi ya Wajerumani.
Mwanangu mwenye imani haba na usahihi wa vielelezo vya kihistoria, hakuwa mwepesi kuamini kwamba fuvu lile lilikuwa la Mtwa Mkwavinyika Mkwawa. Nililazimika kumpatia historia ya fuvu lile, tangu kukatwa kwa kichwa cha Mkwawa mwaka 1898, ambapo  kilipelekwa Ujerumani, hadi mwaka 1954, liliporejeshwa Kalenga, Iringa, kufuatia madai ya Wahehe kutaka warejeshewe fuvu hilo la mtawala shujaa wao.
Nihitimishe kwa kujadili kidogo sababu za Waafrika kuwa wazito wa kufanya ziara za kitalii katika nchi yetu. Inawezekana zikawapo  sababu nyingi, lakini tatu ni dhahiri zaidi.
Moja ni elimu haba katika nyanja za historia na utalii. Sio watu wengi walio na uelewa wa kutosha kuwawezesha kuelewa na kupembua historia ya jamii na nchi zetu. Bila elimu ya namna hiyo, sio rahisi kwa watu walio wengi ku-appreciate matukio mbalimbali ya kihistoria. Tumeona hapo juu, kwa mfano, kwamba baadhi ya visiki vya miti ya mizeituni aliyoishuhudia Bwana Yesu Kristo, bado vinaweza kuonekana hadi leo nchini Israel. Lakini ni waumini wazuri wa Kikristo (kina Askofu Sylvester Gamanywa wa Wapo Mission International) na wanataaluma wa fani ya historia, wanaoweza kujenga imani isiyotetereka kuhusu maelezo kama hayo.
Nililishuhudia jambo hili nilipowaambia wanafamilia yangu kwamba sayansi ya maandishi, inalo chimbuko lake katika Misri ya kale (ancient Egypt). Aidha, mimi mwenyewe nimeweza kusadiki zaidi uwezo mkubwa wa  ustaarabu wa China ya Kale ( Ancient Chinese Civilization), baada ya kuutembelea na kuupanda Ukuta Mkuu wa China (The Great Wall of China) mara mbili katika maisha yangu. Sio rahisi kwa watu wengine wengi, hususan wale ambao hawakujaliwa kuiona milango ya shule au kuzuru vivutio husika, kuwa na keen interest and sense of appreciation kuhusu matukio na vielelezo vyake, kiasi hicho.
Pili, ni malezi na makuzi tuliyoyapata katika mazingira tulimozaliwa na kukulia. Asili ya Waafrika tulio wengi, ni vijijini. Na kabla ya utamaduni na maisha ya mijini kuenea na kutamalaki, tulikuwa karibu sana na mazingira. Huko vijijini, tuliweza kukurupushana mara nyingi na wanyama wa porini kama ngedere, sungura, swala, ndege na wadudu wa aina mbalimbali, wakiwemo wale hatarishi kama nyoka.
Karibu kila mtoto wa Kiafrika, alijihusisha maishani mwake na uwindaji au utegaji wa wanyama na ndege. Na wengi wetu tulisimuliwa na wahenga wetu hadithi za kale kuhusu wanyama mbalimbali kama vile sungura, tembo, chui na wengineo, kiasi kwamba tuliwazoea (sio kuwapenda) hata bila kuwaona wanyama hao. Kila tulipokutana na mnyama pori au ndege, tulikuwa na kazi moja: kumuangamiza kwa kumuwinda kwa mshale, kumtega au kumpopoa kwa manati! Dhana ya utalii wa leo, ni kujenga urafiki na wanyama, ndege, n.k. Katika mazingira tulimokulia, dhana hiyo haikujengeka vya kutosha ndani mwetu mapema.
Lakini kubwa zaidi, ni umaskini uliokithiri wa watu walio wengi. Katika mazingira ya umaskini wetu, hakuna namna ambapo utalii na ziara za burudani zinaweza kuwa ni kipaumbele chetu. Vipaumbele vyetu ni mambo yanayojielekeza katika kutuwezesha kupata mlo wetu wa kila siku na familia zetu (kubangaiza). Maisha nje ya ulingo huo, ni changamoto kubwa kwetu.
Tumekuwa tukishuhudia watalii wa kizungu wakimiminika katika nchi zetu kuwaona wanyama wa porini pamoja na vivutio vingine mbali mbali. Mara nyingi, watalii huwa ni watu ambao walijiwekea nadhiri  kwamba baada ya kustaafu kazi huko makwao, watatembelea nchi zetu hizi ili kula burudani na kufaidi matunda ya jasho lao enzi za ujana wao.
Baada ya mzungu kuwa amehitimu na kufanya kazi kwa miongo kadhaa, atakuwa amelimbikiza akiba kubwa ya fedha, kutokana na ujira wake minono.  Na anapostaafu, analipwa fedha nyingi kama terminal benefits na gratuities. Isitoshe, mstaafu huyu anakuwa hana majukumu makubwa aliyobaki nayo kuyatekeleza katika maisha yake.
Watoto wake (ambao kwa kawaida sio zaidi ya wawili) watakuwa tayari wameajiriwa na kuanza maisha ya kujitegemea. Na kama yupo ambaye bado angali chuoni, si ajabu atakuwa anasoma kwa gharama za serikali au taasisi nyingine ya huduma za kijamii. Mwisho, kama wazazi bado wako hai, bila shaka watakuwa wamekula chumvi nyingi, na watakuwa wanatunzwa na kuhudumiwa katika makambi ya wazee ya serikali. Kazi iliyobaki ya kuwafanyia wazazi hao, itakuwa ni kuwatembelea japo mara moja kwa mwaka na kuwapa maua, kama kielelezo cha mapenzi yake kwao.
Sasa mstaafu huyu, mwenye mapesa kedekede benki, atayafanyia nini mapesa hayo katika kipindi cha maisha yake yaliyosalia? Kwa bahati nzuri, sehemu ya jibu la swali hili, niliwahi kulipata mwaka, 2000 kutoka kwa bosi (wangu wakati ule), Muu wa Mkoa wa Shinyanga, Mohamed Babu. Kama Katibu wake Msaidizi (DPS), nilikuwa nimemsindikiza kwenye safari ya kikazi huko Seronela, Serengeti. Yeye ndiye aliyenifumbua macho kuhusu dhana ya ku-offload.
Tukiwa tunaendelea na vinywaji katika hoteli ile ya kitalii, nilikuwa nimeeleza kushangazwa na uamuzi wa wageni (baadhi wakiwa ni Waswahili wenzetu) kutoonekana kujali bei kubwa ya vinywaji ya pale hotelini, wakati vinywaji sawa na vile, vilikuwa vinapatikana kwa ‘bei che’ katika kijiji jirani na hoteli ile.  Ndipo bosi wangu yule aliponijuza kwamba wenzetu wazungu huwa wamesafiri kwa gharama kubwa kutoka kwao ili wapate fursa ya ku-offload mikoba yao iliyojaa pomoni midola waliyoikusanya kwa miaka mingi kama akiba. Vinginevyo, watu hao waifanyie nini hiyo midola wakati tatizo lao sio umiliki wa fedha, bali namna ya kuzitumia (their problem is not to so much as to earn it, but to spend it).
Tatizo kubwa sisi Waafrika, tulio bado makazini au tuliostaafu tayari, ni umasikini uliokithiri unaotuzonga. Mazungumzo yangu na bosi wangu niliyoyaeleza hapo juu, ni ushahidi tosha wa hali zetu sisi Waswahili. Mazungumzo yale yalinikumbusha jinsi miaka mingi ya utumishi wakina sisi serikalini, tulivyokuwa tunahaha kujinyima lishe na malazi ya viwango bora  tukiwa safarini, kusudi tuweze kuokoa vijisenti kidogo vya kurejea navyo nyumbani, kwa ajili ya kukidhi mahitaji yetu mengine mengi. Ndio kina sisi ambao tulikuwa tayari kuinywa bia yetu katika  vijiji jirani na mahoteli yenye hadhi ya kitalii kama Seronela. Na hali hiyo (ya kubana matumizi) haikubadilika hata baada ya kustaafu kazi, kutokana na malipo duni ya malupulupu ya kustaafu.
Ni katika mazingira kama hayo, inapokuwa ngumu mno kwa Mswahili wa kawaida kutenga kiasi cha maana cha fedha ndogo aliyo nayo katika akiba yake kwa ajili ya yeye na familia yake eti kutoka kwa safari za kitalii. Safari hizo, kwa Mswahili huyu, haziwezi kuwa kitu kingine bali burudani tu, starehe na anasa zisizokuwa za lazima katika maisha yake.
Kimsingi, sipendi kuamini  kwamba Waswahili hawazipendi safari za kitalii. Maana ni nani asiyependa kutoka na kuburudika kwa vivutio mbalimbali, hasa kama vinafikika kwa urahisi na kwa gharama anazoweza kuzimudu? Mbona ni watu wengi tu hawajawahi kuwaona viumbe, mandhari mbalimbali za kimazingira na maeneo ya kihitoria na kijiografia, ambako wangalipelekwa kuzuru, ingaliwapa elimu yenye thamani na kumbukumbu isiyosahaulika katika maisha yao.
Mbona mimi, kwa mfano, siwezi kusahau uzoefu wangu katika mambo kama haya huko ughaibuni (Finland, Uingereza na China) na hata mbuga za wanyama hapa nchini, kama vile Serengeti, Mikumi pamoja na maeneo ya kihistoria ya Bagamoyo, Zanzibar, Arusha, Tabora  Kigoma na Dar es Salaam? Kama siwezi kupanua wigo nilio nao tayari au kurudi kuzitembelea  sehemu zile, sio kwa sababu sikufurahia au kuelimika kwa mambo mengi yenye manufaa katika ziara zangu za awali. Hapana; ni kwa sababu sina mikoba ya ku-offload.
Na pengine tusijifanye Sungura wa simulizi za kale. Sungura aliuona mzabibu uliokuwa umesheheni na kupamba zabibu zilizokuwa zimeiva vizuri na kutamanisha sana. Sungura aliuendea ule mti akinuia kuzichuma na kuzifaidi zile zabibu . Kwa vile maumbile yake hayamruhusu  kukwea miti, Sungura alikuwa na mbinu moja tu ya kuzichuma: kuzirukia kwa juu. Akaruka mara ya kwanza, bila kuzifikia zabibu zile. Mara ya pili, ya tatu, ya nne na ya tano… lakini bado hakuweza kuzifikia.
Hatimaye, Sungura alikata tamaa na kuondoka bila lengo lake kutimia, huku akisonya na kulaani kimoyo moyo, akidai kwamba wala hakuwa na haja nazo zile zabibu, maana zilikuwa ni mbichi: “Za kazi gani hizi?. Wala sizitaki. Zabibu zenyewe ni mbichi; ukakasi mtupu!”