Tuesday, October 23, 2012

“SIZITAKI, MBICHI HIZI” NA UTALII WA NDANI TANZANIA

                           Na  Festo  Mukerebe

Wiki hii ninapoandika makala hii, nimeona vipindi vitatu vya luninga ambavyo naamini vililenga kufanya promosheni ya Utalii wa Ndani nchini. Sijui kwa nini vipindi hivyo  vimerushwa kwa mfuatano katika wiki moja hii; na wala sihitaji sana kujua sababu yake.
Jambo moja limenipa msukumo wa kuandika makala hii. Siku nilipoyafuatilia mahojiano katika mojawapo ya vipindi hivyo, Uchumi Leo, nilijikuta naishirikisha familia yangu kujibu swali muhimu lililojitokeza: kwa nini Watanzania hatupendi kutoka kwa ziara za utalii ndani ya nchi yetu? Sikupata jibu la hakika kwa swali hilo.
Hata hivyo, nilibaini wazi kwamba utalii si jambo la kipaumbele katika familia yangu. Na kwa namna fulani, nilijikuta hofu niliyokuwa nayo awali inayeyuka kama barafu iliyoachwa nje kwenye jua la kiangazi. Nilikuwa nimetarajia kwamba baada ya hamasa nzito iliyokuwa ikitolewa na CEO wa taasisi ya Dar Tourism, pengine familia ingalinisakama na kutaka niiandalie ziara ya utalii wa ndani.
Nilishangaa kusikia wanayabeza mengi yaliyozungumzwa na kuelezwa na CEO kama manufaa ya ziara kama hizo. Mke wangu, kwa mfano, alieleza wazi wazi jinsi ambavyo hayuko tayari kutumia muda wake kwa shughuli za kitalii hapa jijini Dar es Salaam. Ni dhahiri kwamba CEO wa Dar Tourism, alikuwa hakumkonga moyo pale alipohimiza watu watoke kwenda kutembelea sehemu kama vile Mnazi Mmoja ili kuona miti iliyopandwa na viongozi mashuhuri wa bara la Afrika, kama vile Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda na Hayati Samora Machel, Rais wa zamani wa Msumbiji. Sikuwaona kuvutiwa kabisa na wazo lile.
Mwanangu mmoja ndiye alitia fora. Yeye hakuwa na imani hasa na utalii wa maeneo ya kihistoria. Alielekea kuyaona maeneo hayo kama mambo ya uongo na ya kuunda tu, kwa sababu za kibiashara na kiuchumi tu.
Japo na mimi sina shauku kubwa katika nyanja ya utalii, nilijitoa mhanga kuweka sawa mambo mbalimbali kuhusu utalii, na kujibu hoja za wenzangu nilizoziona zimepogoka kupitiliza.
Nianze na hoja ya kutembelea miti iliyopandwa na watu mashuhuri kihistoria. Niliwaeleza, kwa mfano, jinsi wenzetu wa mataifa yaliyoendelea wanavyoenzi viongozi wao wa zamani, kwa kutunza na kuhifadhi vielelezo vinavyogusa maisha yao (viongozi). Ikiwa waliwahi kupanda miti, miti hiyo itatunzwa kwa miaka mingi iwezekanavyo, hata karne kadhaa. Labda sio watu wengi wanaoweza kuamini kwamba ipo miti inayoweza kudumu hata kwa zaidi ya miaka elfu. Mfano mmoja ni miti aina ya mizeituni aliyoishuhudia muasisi wa Ukristo, Bwana Yesu Kristo katika bustani alimofanyia maombi yake ya mwisho, zaidi ya miaka 2,000 iliyopita!
Tulipokuwa katika ziara ya kiserikali nchini Finland, mwaka 1978 (nikiwa nimefuatana na kina Anne Semamba Makinda, Anselm Odhiambo Anacleti, Andrew Kiondo, Mama Mariam Abubakar na mwingine ninayemsahau), tulitembezwa jijini Helsinki na kuonyeshwa vielelezo vya kihistoria na kiutalii vya jiji hilo. Miongoni mwa vielelezo hivyo, ni miti iliyopandwa enzi za kale na viongozi mashuhuri wa nchi hiyo (kama vile Jemedari Mannelheim). Namkumbuka mama wa makamo (professional guide) aliyekuwa akitutembeza na kutupa maelezo fasaha  kuhusu kila kitu unachoweza kukifikiria - jengo, mti, sanamu, mtaa - alivyokuwa akituhamasisha kwa kauli-mbiu aliyopenda kuitamka: “look at thisthis is wonderful, absolutely wonderful”.
Aidha, niliwaeleza habari za vielelezo na vivutio vya kitalii na kihistoria vya Bagamoyo. Niliwajuza kuhusu Profesa Kajeli na uwezo wake mkubwa aliokuwa nao wa kuidadavua na kuielezea kwa ufasaha historia ya mji wa Bagamoyo. (Nimepata kumfananisha Kajeli na marehemu baba yangu mdogo, Ta Erasto, kwa maana ya sura na uwezo wa kueleza mambo na matukio).
Niliwaeleza pia kuhusu vituo vya makumbusho ambamo kumbukumbu mbalimbali za kihisoria na kiutamaduni zinahifadhiwa. Kwa kutoa mfano, nilitaja makumbusho ya Kalenga, Iringa, niliyopata kuitembelea miaka ya nyuma. Katika makumbusho ile, fuvu la shujaa, Mtwa Mkwawa Mkwavinyika linahifadhiwa, ikiwa ni sehemu ya historia ya kutukuka ya mapambano ya kabila la Wahehe dhidi ya Wajerumani.
Mwanangu mwenye imani haba na usahihi wa vielelezo vya kihistoria, hakuwa mwepesi kuamini kwamba fuvu lile lilikuwa la Mtwa Mkwavinyika Mkwawa. Nililazimika kumpatia historia ya fuvu lile, tangu kukatwa kwa kichwa cha Mkwawa mwaka 1898, ambapo  kilipelekwa Ujerumani, hadi mwaka 1954, liliporejeshwa Kalenga, Iringa, kufuatia madai ya Wahehe kutaka warejeshewe fuvu hilo la mtawala shujaa wao.
Nihitimishe kwa kujadili kidogo sababu za Waafrika kuwa wazito wa kufanya ziara za kitalii katika nchi yetu. Inawezekana zikawapo  sababu nyingi, lakini tatu ni dhahiri zaidi.
Moja ni elimu haba katika nyanja za historia na utalii. Sio watu wengi walio na uelewa wa kutosha kuwawezesha kuelewa na kupembua historia ya jamii na nchi zetu. Bila elimu ya namna hiyo, sio rahisi kwa watu walio wengi ku-appreciate matukio mbalimbali ya kihistoria. Tumeona hapo juu, kwa mfano, kwamba baadhi ya visiki vya miti ya mizeituni aliyoishuhudia Bwana Yesu Kristo, bado vinaweza kuonekana hadi leo nchini Israel. Lakini ni waumini wazuri wa Kikristo (kina Askofu Sylvester Gamanywa wa Wapo Mission International) na wanataaluma wa fani ya historia, wanaoweza kujenga imani isiyotetereka kuhusu maelezo kama hayo.
Nililishuhudia jambo hili nilipowaambia wanafamilia yangu kwamba sayansi ya maandishi, inalo chimbuko lake katika Misri ya kale (ancient Egypt). Aidha, mimi mwenyewe nimeweza kusadiki zaidi uwezo mkubwa wa  ustaarabu wa China ya Kale ( Ancient Chinese Civilization), baada ya kuutembelea na kuupanda Ukuta Mkuu wa China (The Great Wall of China) mara mbili katika maisha yangu. Sio rahisi kwa watu wengine wengi, hususan wale ambao hawakujaliwa kuiona milango ya shule au kuzuru vivutio husika, kuwa na keen interest and sense of appreciation kuhusu matukio na vielelezo vyake, kiasi hicho.
Pili, ni malezi na makuzi tuliyoyapata katika mazingira tulimozaliwa na kukulia. Asili ya Waafrika tulio wengi, ni vijijini. Na kabla ya utamaduni na maisha ya mijini kuenea na kutamalaki, tulikuwa karibu sana na mazingira. Huko vijijini, tuliweza kukurupushana mara nyingi na wanyama wa porini kama ngedere, sungura, swala, ndege na wadudu wa aina mbalimbali, wakiwemo wale hatarishi kama nyoka.
Karibu kila mtoto wa Kiafrika, alijihusisha maishani mwake na uwindaji au utegaji wa wanyama na ndege. Na wengi wetu tulisimuliwa na wahenga wetu hadithi za kale kuhusu wanyama mbalimbali kama vile sungura, tembo, chui na wengineo, kiasi kwamba tuliwazoea (sio kuwapenda) hata bila kuwaona wanyama hao. Kila tulipokutana na mnyama pori au ndege, tulikuwa na kazi moja: kumuangamiza kwa kumuwinda kwa mshale, kumtega au kumpopoa kwa manati! Dhana ya utalii wa leo, ni kujenga urafiki na wanyama, ndege, n.k. Katika mazingira tulimokulia, dhana hiyo haikujengeka vya kutosha ndani mwetu mapema.
Lakini kubwa zaidi, ni umaskini uliokithiri wa watu walio wengi. Katika mazingira ya umaskini wetu, hakuna namna ambapo utalii na ziara za burudani zinaweza kuwa ni kipaumbele chetu. Vipaumbele vyetu ni mambo yanayojielekeza katika kutuwezesha kupata mlo wetu wa kila siku na familia zetu (kubangaiza). Maisha nje ya ulingo huo, ni changamoto kubwa kwetu.
Tumekuwa tukishuhudia watalii wa kizungu wakimiminika katika nchi zetu kuwaona wanyama wa porini pamoja na vivutio vingine mbali mbali. Mara nyingi, watalii huwa ni watu ambao walijiwekea nadhiri  kwamba baada ya kustaafu kazi huko makwao, watatembelea nchi zetu hizi ili kula burudani na kufaidi matunda ya jasho lao enzi za ujana wao.
Baada ya mzungu kuwa amehitimu na kufanya kazi kwa miongo kadhaa, atakuwa amelimbikiza akiba kubwa ya fedha, kutokana na ujira wake minono.  Na anapostaafu, analipwa fedha nyingi kama terminal benefits na gratuities. Isitoshe, mstaafu huyu anakuwa hana majukumu makubwa aliyobaki nayo kuyatekeleza katika maisha yake.
Watoto wake (ambao kwa kawaida sio zaidi ya wawili) watakuwa tayari wameajiriwa na kuanza maisha ya kujitegemea. Na kama yupo ambaye bado angali chuoni, si ajabu atakuwa anasoma kwa gharama za serikali au taasisi nyingine ya huduma za kijamii. Mwisho, kama wazazi bado wako hai, bila shaka watakuwa wamekula chumvi nyingi, na watakuwa wanatunzwa na kuhudumiwa katika makambi ya wazee ya serikali. Kazi iliyobaki ya kuwafanyia wazazi hao, itakuwa ni kuwatembelea japo mara moja kwa mwaka na kuwapa maua, kama kielelezo cha mapenzi yake kwao.
Sasa mstaafu huyu, mwenye mapesa kedekede benki, atayafanyia nini mapesa hayo katika kipindi cha maisha yake yaliyosalia? Kwa bahati nzuri, sehemu ya jibu la swali hili, niliwahi kulipata mwaka, 2000 kutoka kwa bosi (wangu wakati ule), Muu wa Mkoa wa Shinyanga, Mohamed Babu. Kama Katibu wake Msaidizi (DPS), nilikuwa nimemsindikiza kwenye safari ya kikazi huko Seronela, Serengeti. Yeye ndiye aliyenifumbua macho kuhusu dhana ya ku-offload.
Tukiwa tunaendelea na vinywaji katika hoteli ile ya kitalii, nilikuwa nimeeleza kushangazwa na uamuzi wa wageni (baadhi wakiwa ni Waswahili wenzetu) kutoonekana kujali bei kubwa ya vinywaji ya pale hotelini, wakati vinywaji sawa na vile, vilikuwa vinapatikana kwa ‘bei che’ katika kijiji jirani na hoteli ile.  Ndipo bosi wangu yule aliponijuza kwamba wenzetu wazungu huwa wamesafiri kwa gharama kubwa kutoka kwao ili wapate fursa ya ku-offload mikoba yao iliyojaa pomoni midola waliyoikusanya kwa miaka mingi kama akiba. Vinginevyo, watu hao waifanyie nini hiyo midola wakati tatizo lao sio umiliki wa fedha, bali namna ya kuzitumia (their problem is not to so much as to earn it, but to spend it).
Tatizo kubwa sisi Waafrika, tulio bado makazini au tuliostaafu tayari, ni umasikini uliokithiri unaotuzonga. Mazungumzo yangu na bosi wangu niliyoyaeleza hapo juu, ni ushahidi tosha wa hali zetu sisi Waswahili. Mazungumzo yale yalinikumbusha jinsi miaka mingi ya utumishi wakina sisi serikalini, tulivyokuwa tunahaha kujinyima lishe na malazi ya viwango bora  tukiwa safarini, kusudi tuweze kuokoa vijisenti kidogo vya kurejea navyo nyumbani, kwa ajili ya kukidhi mahitaji yetu mengine mengi. Ndio kina sisi ambao tulikuwa tayari kuinywa bia yetu katika  vijiji jirani na mahoteli yenye hadhi ya kitalii kama Seronela. Na hali hiyo (ya kubana matumizi) haikubadilika hata baada ya kustaafu kazi, kutokana na malipo duni ya malupulupu ya kustaafu.
Ni katika mazingira kama hayo, inapokuwa ngumu mno kwa Mswahili wa kawaida kutenga kiasi cha maana cha fedha ndogo aliyo nayo katika akiba yake kwa ajili ya yeye na familia yake eti kutoka kwa safari za kitalii. Safari hizo, kwa Mswahili huyu, haziwezi kuwa kitu kingine bali burudani tu, starehe na anasa zisizokuwa za lazima katika maisha yake.
Kimsingi, sipendi kuamini  kwamba Waswahili hawazipendi safari za kitalii. Maana ni nani asiyependa kutoka na kuburudika kwa vivutio mbalimbali, hasa kama vinafikika kwa urahisi na kwa gharama anazoweza kuzimudu? Mbona ni watu wengi tu hawajawahi kuwaona viumbe, mandhari mbalimbali za kimazingira na maeneo ya kihitoria na kijiografia, ambako wangalipelekwa kuzuru, ingaliwapa elimu yenye thamani na kumbukumbu isiyosahaulika katika maisha yao.
Mbona mimi, kwa mfano, siwezi kusahau uzoefu wangu katika mambo kama haya huko ughaibuni (Finland, Uingereza na China) na hata mbuga za wanyama hapa nchini, kama vile Serengeti, Mikumi pamoja na maeneo ya kihistoria ya Bagamoyo, Zanzibar, Arusha, Tabora  Kigoma na Dar es Salaam? Kama siwezi kupanua wigo nilio nao tayari au kurudi kuzitembelea  sehemu zile, sio kwa sababu sikufurahia au kuelimika kwa mambo mengi yenye manufaa katika ziara zangu za awali. Hapana; ni kwa sababu sina mikoba ya ku-offload.
Na pengine tusijifanye Sungura wa simulizi za kale. Sungura aliuona mzabibu uliokuwa umesheheni na kupamba zabibu zilizokuwa zimeiva vizuri na kutamanisha sana. Sungura aliuendea ule mti akinuia kuzichuma na kuzifaidi zile zabibu . Kwa vile maumbile yake hayamruhusu  kukwea miti, Sungura alikuwa na mbinu moja tu ya kuzichuma: kuzirukia kwa juu. Akaruka mara ya kwanza, bila kuzifikia zabibu zile. Mara ya pili, ya tatu, ya nne na ya tano… lakini bado hakuweza kuzifikia.
Hatimaye, Sungura alikata tamaa na kuondoka bila lengo lake kutimia, huku akisonya na kulaani kimoyo moyo, akidai kwamba wala hakuwa na haja nazo zile zabibu, maana zilikuwa ni mbichi: “Za kazi gani hizi?. Wala sizitaki. Zabibu zenyewe ni mbichi; ukakasi mtupu!”


No comments:

Post a Comment