Tuesday, October 23, 2012

SIKU  SUNGURA  ALIPOKUTANA  NA  MBABE  WAKE
                            
                                 Na  Festo   Mukerebe

‘Muosha huoshwa’. Hii ni methali  fupi ya Kiswahili yenye maana kubwa – kwamba hata mtu awe mjanja au mjuzi kiasi gani, hutokea siku naye akazidiwa kete na wajuzi zaidi
Takribani asilimia 90 ya hadithi za kale nilizopata kusimuliwa na wazee wangu enzi nikiwa mtoto mdogo, miaka ya 50 na 60, hususan zile za wanyama, zilimtweza na  kumuinua sungura, mnyama mdogo tu, na kumpa dhima kubwa mno miongoni mwa wanyama wengine mbalimbali, wakiwemo kina tembo, faru, nyati, kiboko na wengine wengi.  Maguvu ya misuri na manyama tipwatipwa, hatimaye hayakuwawezesha kufua dafu au kuwa na tija chanya mbele ya changamoto za nyakati.
Ni sungura, pamoja na udogo wake kimaumbile, ambaye daima aliibuka kidedea kwa  akili, ujanja, hekima na busara zilizosaidia kupatikana kwa suluhu muafaka za changamoto hizo. Kwa maneno mengine, sungura aliweza kuivunjilia mbali mifupa iliyowashinda kuitafuna kina fisi na mbwa mwitu wenye uchu.
Lakini kwa mujibu wa kisa kifuatacho, inadhihirika kwamba katika maisha, kamwe siku hazilingani, na kwamba hata yule bwana aoshaye na kutayarisha maiti kwa mazishi, hutokea siku naye akajikuta anakufa, anaoshwa na kuandaliwa na watu wengine tayari kwa mazishi. Ni hali hiyo, japo sio ya kifo halisi, iliyomtokea Sungura mjanja siku moja katika maisha yake. Na tusisahau msemo mwingine kwamba hata kinyozi naye hunyolewa pia.
Zamani za kale, Mfalme wa himaya ya wanyama pori, alitambua kwamba alikuwa anazeeka na nguvu kumuishia kwa kasi. Na kwa kutambua kwamba kifo kilikuwa kinamjongelea, alihisi hamu ya kumuona mjukuu kabla maisha yake duniani hayajayoyoma. Kwa hiyo, kwa vile Mfalme alijaliwa kumzaa mtoto mmoja tu, na mtoto mwenyewe ni binti, aliamua kumuoza haraka iwezekanavyo ili amzalie mjukuu kipenzi.
Ilani ilitolewa nchini kote kwamba vijana waliohitaji kumchumbia binti wa Mfalme, wajiweke tayari kwa shindano la mbio maalum za kifalme lililokuwa mbioni kutimua vumbi. Ilikusudiwa kwamba mshindi wa pambano hilo ndiye angalikuwa mume wa binti wa Mfalme.
Basi kwa ilani hiyo, vijana wengi wa himaya ya Mfalme na hata himaya nyingine za falme jirani walianza kujiwinda vikali kwa mbio za kishindo za masafa ya kati zilizokuwa zinakaribia. Sungura alikuwa ni mmoja wa vijana waliojitokeza kujisajili kwa shindano lile la kihistoria. Watu wengi waliomfahamu Sungura walimpa asilimia kubwa ya ushindi.
Hata hivyo, kwa vile shindano lenyewe lilikuwa la wazi, ‘watu’ hawakushangaa kuwaona hata kina Tembo, Swala, Kobe, Konokono, Chura, Kinyonga na wengine wakiwasili Ikulu kujiandikisha, kila mmoja akijigamba kwa namna yake jinsi atakavyoibuka mshindi siku ile na hatimaye kumtwaa binti wa Mfalme. Himaya nzima ilirindima kadiri ‘siku ya siku’ ilivyozidi kukaribia.
Mashabiki wengi walidiriki kuwawekea madau mazito baadhi ya washindani. Madau makubwa zaidi yaliwaangukia kina Duma na Sungura, kwa jinsi walivyotambulika kwa mwendokasi wao wa asili. Baadhi ya wanyama, hasa Sungura, waliongezea utamu kwenye utabiri wa wengi, kwa kujigamba kuibuka na ushindi wa kishindo, inyeshe mvua ya masika au liangaze jua kali la kiangazi. Sungura alidai kwamba alikuwa haoni mpinzani wa dhati, hasa baada ya habari kuenea kwamba Duma asingaliweza kushiriki mashindano yale kutokana na msiba wa mama yake kipenzi, uliokuwa umemtokea siku si nyingi zilizopita.
Wakati huo huo, baadhi ya washindani walibaki kuwa gumzo katika vijiwe na makazi. Tembo, Nyati, Kobe,  Kiboko na Konokono, kwa mfano, walizungumzwa kwa dhihaka na kebehi za kila namna.  Miili tipwatipwa ya baadhi yao ilitajwa kama changamoto na kichekesho kuu katika mbio zozote, achilia za kifalme kama hizi. Tembo, kwa mfano, hakufanikiwa kupunguza hata chembe uzito wake, licha ya mazoezi ya kukata na shoka aliyokuwa akiyafanya kila siku. Kwa upande mwingine, mwendokasi wa Kobe na Konokono, uliendelea kuwatia mashaka wengi. Na labda ni shauku ya kuona hatma ya sakata hilo, iliyowavuta wengi kujiwekea nadhiri ya kuhakikisha wanashuhudia mbio hizo za wazi za karne.
Katika washindani wote, Kinyonga alionekana (wakati wote wa maandalizi) kuwa mchache wa maneno na mwingi wa fikra. Hali hiyo iliwachochea watu wengi kumpuuza na kutomtilia maanani kabisa. Alikuwa kama vile hayupo, licha ya kushuhudiwa akipiga jaramba za nguvu kila siku.
Katika jaramba zake, Kinyonga alionekana akifanya mazoezi maalum ya kunyosha misuli ya vidole vya mikono na miguu yake, mithili ya mtu anayenuia kuboresha uwezo wake wa kukamata au kudaka kitu kiganjani. Wengi walijisemea kwamba alikuwa amepoteza mwelekeo. Wengine walichelea kwamba alikuwa amechanganyikiwa na kudhani kuwa shindano lijalo lilikuwa linahusiana na kudaka au kukamata vitu mkononi.
 Hatimaye, ‘Siku ya siku’ iliwadia. Maelfu kwa maelfu ya wananchi walifurika uwanja wa taifa kushuhudia kinyang’anyiro cha karne. Hakuna aliyekubali kubaki nyumbani  akisubiri kusimuliwa na wengine hitimisho la tukio lile, ambalo hata wahenga hawakuwahi kulishuhudia. Hiyo ilikuwa na maana kwamba tukio kama hilo halikuwahi kutokea katika himaya ile tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
Wageni wa heshima walikuwa wamechukua nafasi zao katika viti vyao, na milango ya uwanja ilikuwa imefunguliwa tangu alfajiri, ili kuhakikisha kwamba kila raia aliyejihimu kwenda anapata fursa ya kuingia na kushuhudia kila jambo lililokuwa linaendelea uwanjani pale.
Kipyenga kilipulizwa kuashiria washindani wanaelekea na kujipanga katika msitari wa kuanzia mbio. Shughuli hiyo ilichukua muda kitambo kutokana na idadi kubwa ya washiriki. Na kwa sababu hiyo pia, msomgamano na mbanano, usingaliweza kuepukika.
Ni katika mazingira hayo Kinyonga alipopata mwanya wa kupenya na kuwa jirani kabisa na Sungura. Alitumia fursa hiyo kujishikiza imara kwenye manyoya ya mkia wa Sungura. Na kwa sababu za msongamano na mgusano wa washindani, Sungura hakuweza kuhisi maungoni mwake jambo lolote lisilokuwa la kawaida.
Kipyenga cha kuashiria mbio kuanza sasa kilipulizwa, na umati mkubwa wa washindani sasa uliondoka, huku kila mshiriki akijitahidi kujinasua na kusonga mbele kwa nafasi. Lakini baadhi ya washiriki walijikuta wakipoteza mwelekeo na kudondoka katika hatua za awali za mbio hizo, kutokana na kuteleza au kukanyagana.
Hatimaye, Sungura alifanikiwa kujinasua na kuchomoka mbele ya washiriki wenzake, huku akishangiliwa kwa nguvu na umati wa watu wote waliokuwa wamejazana pale uwanjani kiasi cha ‘mtu’ kukosa nafasi ya kutema mate. Kila mtazamaji, ikiwa ni pamoja na Mfalme mwenyewe na ‘watu’ wa ukoo wake, alikuwa akilifuatilia shindano kwa umakini mkubwa, furaha na shauku tele, vifijo na vigelegele, ambavyo mwangwi wake uliweza kusikika mamia ya kilomita kutoka pale uwanjani.
Wakati mzunguko wa mwisho unakaribia, viti viwili vilivyoundwa kwa dhahabu na kupambwa   na vito lukuki vya thamani, viliwekwa jukwaa kuu. Kiti kimoja kilikuwa ni mahsusi kwa ajili ya mwali (binti wa Mfalme), ambaye aliingia kwa chereko na vifijo, akiwa anasindikizwa na kundi la watu wa familia ya Mfalme. Kiti cha pili kilikuwa cha kuketi mshindi mtarajiwa wa shindano la mbio zilizokuwa zinaelekea ukingoni. Huyu ndiye alikuwa awe Bwana Harusi wa binti wa Mfalme, yaani mkwe mtarajiwa wa Mfalme.
Sasa Sungura alikuwa akipiga matambo kwa madaha na mbwembwe kuelekea jukwaani, akiwa amemaliza mzunguko wa mwisho, kichwani akiwa hana hisi za jambo lolote zaidi ya kutawazwa kuwa mkwe wa Mfalme.  Kwa majivuno na maringo ya kila aina, huku akisindikizwa na kila jicho, alielekea kwenye kiti cha enzi kando na Bibi Harusi. Na wakati uwanja wa taifa unalipuka kwa kumshangilia, alichupa kwa kasi na kuketi juu ya kiti cha bwana harusi mtarajiwa, sambamba kabisa na binti Mfalme, ambaye muda mchache tu ujao angelikuwa mke wake mpendwa.
Lakini nuktahiyo, jambo la ajabu likatokea. Kwani wakati tako lake linagusana na kiti cha enzi, ghafla ikasikika sauti ndogo ikifoka na kulalama kutokea  juu ya kiti kile alichoelekea kukikalia. Sauti ilikemea kwa utulivu:
“ Wewe Sungura vipi? Kwa nini unanikalia kichwani na kuniumiza namna hii?  Unajidai hunioni, ee? Umekumbwa na kiwewe gani hiki hadi kuishiwa staha na ustaarabu kwa kiwango hiki? Mbona mimi niliwasili mapema na kukalia kiti hiki si chini ya dakika kumi zilizopita kabla yako? Sasa unatafuta nini hapa? Mbona viti vingi bado ni vitupu tu? Unataka kutuaminisha kwamba huvioni kabisa? Umechanganyikiwa nini? Tuheshimiane, bwana, tafadhali!”
Kila ushahidi ulimshadidia Kinyonga na kumuangusha Sungura. Kwa mfano, kama ilivyokuwa kwa washindani wote waliojisajili kwa shindano lile, Kinyonga alikuwa na lebo rasmi ya namba mgongoni mwake iliyothibitisha,  pasipo utata wowote, uhalali wa ushiriki wake katika shindano lile. Pili, kila mtu aliiafiki mantiki  kwamba ni yule aliyetangulia kuwasili kwenye kiti ndiye anayeweza kukaliwa kichwani au mgongoni na mtu anayekuja baadaye. Isitoshe, Kinyonga alithibitika kutangulia kuwasili muda mrefu kutokana na mwili wake kuonekana kutokuwa na jasho lolote, tofauti na Sungura ambaye alikuwa bado anatweta na kuhema, huku akiendelea kububujikwa na jasho chapachapa mwilini.
Aidha, iliyumkinika kwamba watu wengi walikuwa wameweka madau yao kwa washindani wa chaguo lao, yaani kina Tembo, Kobe, Konokono na Sungura - kwa maana ya kushinda au kushindwa shindano. Kwa hiyo, macho yote yalielekezwa kwa wadau wale, na hawakuwa makini kubaini Kinyonga aliwasili jukwaani muda gani na kwa staili gani.
Kwa sababu hizo, Kamati ya Maandalizi na Usimamizi wa Shindano lile ilikuwa haina budi kumthibitisha na kumtangaza Kinyonga mshindi wa Mbio za Mfalme. Na kwa msingi huo, Mfalme mwenyewe alichukua nafasi hiyo kumvisha Kinyonga taji la heshima ya Prince na kumtawaza rasmi kuwa mkwe wake (mume wa binti yake), huku Sungura akibaki ameduwaa, asitambue ni kitu gani kilichomsibu na kumnyakua tonge mdomoni! Ilikuwa ni lift ya aina yake.

No comments:

Post a Comment