SENSA YA WATU NA MAKAZI, 2012: NILICHOKIONA MIMI.
Na Festo Mukerebe
Yapata mwezi Machi au Aprili hivi mwaka huu, niliandika makala nikitoa hoja kwa nini mimi binafsi nilikuwa sijihisi kushiriki Sensa ya mwaka huu, 2012. Lakini baadaye, niliingiwa na woga kidogo, nikihofia maandishi yangu kuhusishwa na misimamo ya vikundi vya kidini, hasa vya Kiislamu, vilivyoazimia na kutishia kuisusia Sensa hiyo kabisa.
Hata hivyo, nilikuwa nimezitaja kwa uwazi na ukweli sababu zangu kadhaa za kutopenda kushiriki Sensa hiyo. Nilieleza katika makala ile kwamba kimsingi mimi ni muumini wa manufaa ya Sensa; na wala sikuhitaji ushawishi au elimu zaidi kutoka kwa mtu yeyote kuhusu jambo hilo.
Katika maisha yangu ya miaka 60, mimi nilikuwa nimeshiriki katika Sensa zote zilizowahi kufanyika nchini mwetu, nikiijumuisha hata ile iliyofanyika mwaka 1957, enzi za ukoloni, japo sitaki kuongopa kwamba nina kumbukumbu ya kutosha kuhusu uzoefu wangu katika Sensa ile. Umri wa miaka minne niliokuwa nao wakati ule, hauniwezeshi kukumbuka nini kilijiri wakati makarani wa zoezi hilo walipozuru kaya ya Baba yangu siku hiyo, kuendesha Sensa ile. Hivyo, sina hata uhakika kama watu hao kweli waliwahi kufika nyumbani kwetu. La msingi hapa ni kwamba nilikuwa tayari nipo duniani wakati huo.
Sensa zilizofanyika baada ya uhuru, hususan 1967, 1978, 1988, 1998 na 2002, nilizishuhudia na kushiriki nikiwa tayari na uelewa wa kutosha. Utaona hapo kwamba Sensa ya mwaka huu, 2012, ilikuwa ni Sensa ya sita kwangu.
Isitoshe, kazi yangu Serikalini, kati ya mwaka 1977 hadi mwaka 1986, ilihusiana moja kwa moja na ukusanyaji wa torwi na takwimu. Pengine ndio maana nautambua fika umuhimu wa zoezi la Sensa na dhima yake katika mipango ya maendeleo ya nchi yetu.
Inaweza kuhojiwa kwa nini sasa sikujisikia kushiriki Sensa ya mwaka huu! Ni hoja nzuri na halali kabisa kujibiwa. Kwa hiyo, japo sipendi au kukusudia kuirejea kwa ukamilifu wake makala niliyoitaja hapo awali mintarafu hisia zangu, itoshe tu kutaja hapa, japo kwa kifupi sana, sababu hizo.
Nilianza shule Januari 1961, nikiwa natembea peku maili kadhaa kila siku, liwake jua au inyeshe mvua. Miavuli tuliyoijua enzi zile ni majani ya migomba. Njia niliyoitembea ilipitia pori moja lenye nyasi ndefu la Mayoga, na ilikuwa na upana wa inchi zisizozidi sita. Hata kuendesha baiskeli katika hicho kinjia ilikuwa ni changamoto ya aina yake. Lakini tulikuwa nazo hizo baiskeli? Na enzi zile, wadudu hatarishi kama nyoka na nge walitamalaki. Neno ‘daraja’ lilikuwa msamiati mgumu kijijini kwetu. Sasa fikiria jinsi, kwa umri wetu mdogo, tulivyoweza kuvuka mito kama Njumbelo, iliyofurika maji pomoni, hasa majira ya masika.
Kijishule cha msingi nilichoanza kusomea, Kashumbililo, kilikuwa ni cha gredi ya chini (lower primary school), kikiwa na majengo ya madarasa yasiyozidi matatu. Nyumba ya pekee ya mwalimu, ilijengwa baadaye kwa nguvu kazi ya sisi wanafunzi na michango ya wazazi wetu masikini. Hata baada ya miongo mingi kupita sasa, taswira ya shule hiyo haijabadilika sana, japo ilikwishapandishwa hadhi kuwa shule ya msingi kamili.
Njia ya kutoka nyumbani Kimbugu kwa wazazi wangu, hadi shule yangu ile ya zamani, imebaki kama ilivyokuwa enzi zangu, ingawa haja ya kuwepo miundombinu ya madaraja ya kuvukia mito, sasa imepungua kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, yaliyosaidia kupunguza kiwango cha mvua zinazonyesha kwetu, maji yanayotiririka mitoni, uoto wa asili na wadudu hatarishi.
Wala hakuna nafuu katika sekta nyingine za kijamii. Kwa mfano, zahanati ya Izigo niliyoshiriki mimi ufunguzi wake mwaka 1964, nikiwa katika kwaya ya shule, haijabadilika sana hadi leo; na siwezi kushangaa kukuta huduma zinazotolewa ndani ya zahanati ile, ni hafifu zaidi kuliko ilivyokuwa wakati inafunguliwa, kwa sababu idadi ya watu wanaotegemea huduma yake, imeongezeka mara dufu, wakati miundombinu yake haijaongezeka na kuboreshwa vya kutosha. Liturgia ya mambo kama haya huko vijijini, inaweza kuwa ndefu sana.
Lakini sio vijijini tu. Hata katika sehemu nyingi za miji yetu, mambo si shwari kabisa. Hatuhitaji hata kutoka mbali ya jiji letu hili la Dar es Salaam ili kulitambua au kulithibitisha jambo hili. Katika makala yangu ya awali niliyoitaja, nilieleza visa na matukio kadhaa ambayo ndiyo hasa almanusura yasababishe nighairi Sensa inayoendelea hivi sasa wakati naandika makala hii.
Mapema mwaka huu, tuliambiwa kwamba Serikali ilikuwa inaendesha mpango wa kugawa vyandarua, kama sehemu ya kampeni ya Taifa ya kutokomeza ugonjwa hatarishi wa maralia. Tulitakiwa tujiandikishe ili kuwezesha kupatikana kwa takwimu sahihi za mahitaji halisi ya vyandarua katika kaya zetu. Tukafanya hivyo. Lakini kichekesho cha mwaka ni kwamba vyandarua hivyo vilipoanza kutolewa, kaya yangu, yenye wanafamilia wanane, ikaishia kuambulia chandarua kimoja tu! Nikigawe vipi chandarua kile chembamba ili kitosheleze mahitaji ya familia yangu, ni swali ambalo Serikali (au watendaji wake?) haikuwa na habari nalo.
Baada ya malalamiko makali, nikiwa mgonjwa kitandani, niliweza kuongezewa chandarua kingine kimoja kidogo chenye matundu yanayoruhusu mbu kupenya! Zoezi hilo la kitaifa likawa limeishia hapo, likituacha baadhi yetu tukijiuliza mantiki na sababu za usumbufu wote wa makarani kupita awali kutuandikisha na kukusanya takwimu za watu katika makazi yetu. Lakini tukaelewa kwamba posho zililiwa. Tukachoka.
Mwishoni mwa mwaka jana, 2011, eneo ninaloishi, lilikumbwa na mkondo wa maji uliotokana na mvua kali za msimu wa vuli. Barabara ya mtaa ninaoishi mimi mwenyewe, ilizolewa kabisa na mkondo huo. Badala ya ‘miundombinu’ na ‘barabara’, tukabaki na msamiati wa ‘makorongo’ na ‘maandaki’ mbele tu ya nyumba zetu.
Pamoja na hali yangu niliyoitaja ya ugonjwa na ulemavu wa viungo, nilifanya jitihada za kuwasiliana na viongozi mtaani kwetu. ‘Wallahi’ hakuna kiongozi hata mmoja, wakati ule hata sasa, aliyefika kunijulia hali (na hapa sizungumzii msaada wa huduma ya matibabu, kama raia mwema) au kukagua uharibifu uliotokea mbele kabisa ya mlango wa nyumba yangu, na kusaidia kuchukua hatua zozote za kuurekebisha.
Aidha, sisi wakazi wa eneo langu, tumekuwa na mgogoro wa muda mrefu, mintarafu hali na hadhi ya viwanja vyetu vya makazi. Inadaiwa kwamba miongo mingi iliyopita, eneo letu liligawiwa kwa mwekezaji mmoja wa Kihindi, kwa mradi wa ujenzi wa viwanda. Lakini Mhindi huyo alishindwa kuliendeleza eneo hili, ambapo baada ya miaka yote hiyo, Waswahili tukawa tumemegeana na kuuziana viwanja vya makazi. Tukajenga nyumba na kuishi, raha mstarehe, bila taarifa za kutosha za ‘mtafaruku’ ambao ungaliweza kutukabili.
Tunasikia kwamba mwekezaji aliporejea miaka ya karibuni na kupewa na serikali sharti la kutoa fidia kwa wakazi na makazi yao, akaghairi kusonga mbele na mradi wake wa ujenzi wa viwanda. Kisa, idadi kubwa mno ya wakazi. Lakini tukagutuka kugundua kwamba eneo letu hili, sasa linatambuliwa, katika kumbukumbu za kiutawala, kwa jina baya la ‘hazard’!
Inaelezwa kwamba katika mazingira hayo, Rais Kikwete wakati akipita eneo hili kwa kampeni zake za awamu ya pili, aliombwa kufuta umiliki wa mwekezaji yule wa Kihindi, na kuturasmishia ukazi sisi wazawa. Na kwa tetesi kwamba Rais aliruhusu uhamisho huo kutekelezwa, mchakato wa kufanya hivyo ukawa umeanza, japo tulio wengi, bado tuliendelea kutokuwa na taarifa za uhakika kuhusu ‘mabadiliko’ hayo.
Hatimaye, kikaitishwa kikao cha mtaa wetu, ambapo kila kaya yetu ilitakiwa kuchangia Sh. 200,000/- katika mfuko fulani ili kuwezesha eneo letu kupimwa, kama sehemu ya urasmishaji tajwa. Namba ya akaunti ya benki ya mfuko huo ilitajwa.
Lakini inavyoelekea, wakazi wenzangu waliohudhuria mkutano ule uliowataarifu kuhusu mchakato wa upimaji , hawakupewa maelezo yenye mashiko ya kutosheleza kiu yao ya kutaka kujua, hasa ikitiliwa maanani kwamba Sh. 200,000/- sio kiasi kidogo mno kwa mwananchi wa kawaida kutoa kwa urahisi, hasa kama maelezo yenyewe ni mepesi mepesi kiasi hicho.
Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, hadi leo, hatujawaona viongozi wetu wa Mtaa wakitupitia au kuonekana kulifuatilia zoezi hilo, kwa shabaha ya kulipatia uongozi stahiki. Matokeo ya hali hiyo ya mashaka, ni kwamba wakazi wamekuwa wazito kujitokeza kutoa (bila dhamana au kauli yoyote ya uhakika) fedha zilizotakiwa kutolewa, licha ya kwamba sisi wananchi tunapenda, na tuko tayari kupimiwa rasmi viwanja vyetu. Mtanzania gani asiyejua uwepo wa ufisadi na mafisadi, ambao wakati wote wanachuruzika udenda wa utajirisho, kwa kutumia migongo ya ‘wajinga ndio waliwao’? Ombwe la uongozi!
Jana, tarehe 27 Augosti, 2012, nilithibitisha ombwe la uongozi ambalo tumekuwa tukitahadharishwa kwamba tunalo katika nchi yetu, toka ngazi ya Taifa hadi ngazi zetu hizi za chini, mitaani. Nilikuwa nimewasubiri makarani wa Sensa tangu jana yake, tarehe 26 Augosti, 2012, ambayo ndiyo ilikuwa siku ya kuanza kwa zoezi hilo la kitaifa. Mimi na wenzangu katika mtaa wetu, tulikuwa tunajiuliza mengi kuhusu ratiba ya makarani kutupitia. Kwa vyovyote vile, sio utawala bora au uungwana, kuwaacha watu wakisubiri kwa kipindi cha wiki nzima, bila kujua ni siku gani hasa watafikiwa katika kipindi hicho cha siku saba za zoezi hilo.
Ndio maana hiyo jana, mimi binafsi sikuwashangaa wapangaji wangu kukutwa hawapo katika vyumba vyao, karani wa Sensa alipowasili kutuhesabu! Wangalifanyaje na ‘mishemishe’ zao, ili kujihakikishia mkono unakwenda kinywani, wao na familia zao?
Kwamba tunalo ombwe la uongozi, ilithibitika zaidi wakati wa mazungumzo yangu na karani huyo wa Sensa kwa eneo letu. Kwanza, karani mwenyewe, alikuwa amenishangaza kwa kufika nyumbani kwangu akiwa yeye peke yake.
Nilikumbuka jinsi enzi zetu sisi, tusingethubutu kuingia ndani ya jamii (kwa mfano kijiji) bila kupitia au kuambatana na kiongozi wa eneo husika. Ilinisikitisha mno Karani huyo wa Sensa aliponijulisha kwamba hata kuonyeshwa tu eneo lake la kushughulikia na mipaka yake, kulifanyika kwa kuonyeshwa kwa kidole kutokea mbali: “Mgeni (Karani), eneo lako linaanzia kwenye nyumba ile pale, hadi barabara ile kule, kisha unakata kulia kuelekea mtaa ule kule, na kuzungukia nyumba yenye geti jekundu kule….bla bla bla” Uongozi gani huo?
Hatuna budi kukubali kwamba Watanzania tumeshiba sana uungwana. Vinginevyo, kwa nini hatukuwatimua kwa mishale makarani wale wa Sensa tusiowafahamu, walioingia katika miji yetu bila utambulisho wowote?
Hali hiyo ilinikumbusha mambo mengi niliyoyatambua katika safari yangu ya maisha. Zamani za Kale, Wamasai walikuwa na ngoma yao ya mashujaa, iliyochezwa usiku wa manane. Ngoma hiyo iliwapa fursa vijana (morani) kujipatia wachumba na zawadi mbalimbali, hasa ng’ombe, zilizotolewa na chifu wa eneo husika. Maleba yaliyomtambulisha kijana kama shujaa na jasiri, yalikuwa ni pamoja na mikia ya simba na korodani zilizokaushwa, yaliyoning’inia shingoni mwa morani wale wakati ngoma hiyo ikichezwa. Idadi ya makolokolo hayo ndiyo iliwajengea heshima washiriki miongoni mwa umma na jumuiya ya mabinti (ndito) waliokuwa nao wakisaka wachumba.
Wakati mikia ilipatikana kwa kupambana na kuwaua simba, korodani zilipatikana kwa mauaji ya watu wa makabila mengine walioonekana wakikatisha nchi ya Wamasai. Kwa mtazamo wa Wamasai, watu hao, sawa na simba, walikuwa wanasaka ng’ombe; hivyo, wote walihesabiwa kuwa maadui (mang’ati) waliopaswa kuuliwa na vijana jasiri na shujaa. Ushujaa huo ulithibitika katika ‘ngoma ya mashujaa’ na kutambuliwa kupitia mavazi na maleba waliyovaa.
Niliikumbuka mila hiyo ya Kimasai siku Karani wa Sensa alipoingia katika mji wangu, bila kiongozi yeyote wa mtaa wetu wa kumtambulisha. Sielewi ni vipi Serikali ilijiaminisha kwamba, katika mazingira hayo, Karani huyo angekuwa salama? Kwa maneno mengine, hivi mimi ningalikuwa naendekeza mila na desturi za asili ya Kimasai kama hizo, usalama wa karani yule ungelihakikishwa namna gani siku ile?
Mtu aliyesoma makala yangu ya awali kuhusu Sensa ya mwaka huu, hatakosa kunishangaa kwamba nilivunja vipi nadhiri yangu ya awali ya kutoshiriki zoezi hilo? Nimweleze mtu huyo kwamba nililazimika kuchukua mtazamo tofauti kwa sababu kadhaa. Kwanza, sikupenda itokee nihusishwe na misimamo mikali ya kidini, ilhali mimi nilikuwa na sababu zangu binafsi zinazojitosheleza.
Lakini pia nilizidiwa na vitisho vya Serikali kwamba mwananchi ambaye atagomea au kususia Sensa mwaka huu, ama atakabiliana na kifungo cha miezi sita jela, au faini ya Sh. 500,000/-. Nilijikuta nasalimu amri na kukubaliana na mwananchi mmoja, aliyesikika katika Wapo Radio akiomba kwamba kero ya Sensa ije na kupita haraka , ili wananchi sasa tupumue.
Aidha, nilivutiwa na Wahadzabe wa Yaeda Chini, Bonde la Ufa, walioshinikiza kuwindiwa nyani na pundamilia, ndipo waridhie kuhesabiwa. Na kweli Serikali hatimaye iliwatimizia watu hao mahitaji yao hayo, nao wakajitokeza kwa wingi kuhesabiwa. Nawafahamu sana Wahadzabe na mapenzi yao makubwa ya nyama pori (manako). Lakini wakati wao walifanikiwa kuwasilisha matatizo yao Serikalini na kutimiziwa haja zao, mimi naendelea na msoto wangu wa enzi na enzi. Wahadzabe hoyee!
Sensa imepita na mimi nimehesabiwa. Lakini ni maoni yangu kwamba ni muhimu wananchi wanaposhiriki Sensa zetu hizi, hatimaye waone manufaa yake - maendeleo ya kweli. Na wala sidhani kama wananchi kuihoji Serikali kuhusu jambo hili, ni uhaini au jinai kwa namna yoyote ile.
Sensa na mipango mingine ya Serikali, haina budi isaidie kujibu kero na kuinua hali za maisha ya wananchi. Ni lazima watu waanze kuona mabadiliko ya maisha, mara baada ya Sensa zenyewe kumalizika, ndipo watahisi kuzichangamkia kikamilifu Sensa za miongo ijayo. Vinginevyo, huko tuendako, tusishangae kuona ongezeko la wananchi wanaojitenga au kususia, sio tu Sensa, bali hata mipango mizuri mingine ya Serikali.
Lakini lipo jambo moja kuhusiana na dodoso la Sensa ambalo nililibaini mimi. Kimsingi, tangu awali, nilikuwa nimetarajia kwamba mahojiano yangu na karani yasingalichukua muda pungufu ya masaa mawili. Nilishangaa kumalizana naye ndani ya muda usiozidi dakika 45 hivi. Ili nijiridhishe kama kweli na vipi jambo hilo lilikuwa limewezekana, nilimuuliza Karani mara mbili mbili anithibitishie kama alikuwa amehitimisha zoezi.
Hata baada ya kuondoka kwake, niliendelea kujisaili moyoni kuhusu jambo hilo. Kwa bahati nzuri, siku ya kwanza ya Sensa yenyewe, nilikuwa nimeshuhudia kupitia luninga, kipindi kilichorushwa na TBC kutokea Ikulu, ambako ilionekana kumchukua muda kama huo huo Rais Jakaya Kikwete mwenyewe hadi kurejea ukumbini, akitokea chumba cha mahojiano kama hayo.
Tatizo langu hasa sio muda uliotumika kwa mahojiano hayo. Tatizo linalonisumbua kichwani, ni kama dodoso lililotumika kutuhoji lilibeba maswali yote muhimu ya kidemografia yaliyohitaji kujibiwa nasi wananchi.
Bado nadadisi kwa nini sikuhojiwa kuhusu mambo ya maendeleo ya makazi, kwa mfano. Katika nyanja hiyo, nilitazamia kuulizwa kama nilikuwa naimiliki nyumba ninayoishi na familia yangu, au ilikuwa ni ya kupanga tu? Nilitarajia kuulizwa nyumba yangu ina vyumba vingapi na kwa matumizi gani? Nilitarajia kuulizwa kama kiwanja changu kilikuwa kimepimwa, na hati yake ninayo? Nilitarajia kuulizwa huduma za kijamii na kiuchumi zinazonizunguka, kama shule, zahanati, barabara, soko, kituo cha usalama, maduka, maji, n.k., na jinsi ninavyozipata na kuzifikia? Kwangu mimi, swali hilo ni muhimu sana kwa sababu makazi bora ni pamoja na huduma hizo. Si wanasema kuwa ni Sensa ya Watu na Makazi? Kwa mantiki hiyo, Makazi yako wapi sasa?
Aidha, kama mzee mstaafu na mlemavu, sikutazamia nikose kuulizwa swali lolote kuhusu huduma za hifadhi ninazozipata kutoka serikalini na katika jamii inayonizunguka, ikiwa ni pamoja na ubora au utoshelevu wake. Sasa nitajitambulisha vipi na Sensa yenyewe, bila kuiona Sensa hiyo inalenga kuniondolea vikwazo vya maisha yangu mimi mwenyewe? Niharakishe kutamka hapa kwamba hakika mke wa muasisi wa Taifa letu, Mama Maria Nyerere, hawezi kuwa alikosea katika suala hili.
Mama huyo amenukuliwa na vyombo vya habari akinadi, kutokea nyumbani kwake Butiama, kwamba kadhia nzima tuliyoishuhudia ya watu kususia Sensa mwaka huu, haitokani na elimu duni kuhusu manufaa ya zoezi hilo kitaifa, bali ari ya kutaka kuiadhibu Serikali kwa uongozi wake dhaifu uliowatelekeza na kero lukuki zinazowakabili, ambazo wananchi hawaoni juhudi za dhati ambazo Serikali hiyo inafanya kuzitatua. ‘Like wife like husband, ee?’ Long live, Mama Maria Nyerere!
Nikirejea katika mada, nasema nilishtuka kuulizwa maswali ya abracadabra kama vile nilikuwa na ndugu zangu wanaoishi na kuendesha shughuli za kiuchumi ughaibuni (diaspora). Jambo hilo lilinikumbusha mkakati wa chini kwa chini wa baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara nchini mwetu ambao wala hawafichi uchu wao wa kujijengea uhalali wa kutaka kumiliki pasi za kusafiria (passport) zinazowatambua kuwa na uraia wa nchi zaidi ya moja! Nani asiyejua kwamba washabiki hawa wa sera za dual citizenship, wanalenga kuchuma kutoka ‘shamba la bibi’ kinyemela, na mwisho wa siku, kulia kivulini ughaibuni, bila kubugudhiwa na mtu yeyote?
Kwa kuzingatia suala hilo, sasa nilianza kuona msingi wa misuri kutunishwa na vitisho lukuki kutolewa na dola, dhidi ya baadhi ya Watanzania waliotaka Sensa hii ituwezeshe kupata uelewa wa muundo wa kijamii (social structure) wa nchi yetu. Mambo ya ughaibu yana manufaa gani kwetu kama Taifa, kushinda elimu ya muundo na mfumo wa maisha ya Watanzania?
Hivi kweli demographic data za makabila (120?) au hata mgawanyiko wetu katika madhehebu ya dini, kwa mfano, zimekosa manufaa yoyote chanya kwa nchi yetu? Madhara yanayohofiwa, ni nini hasa? Mbona huwa tunawaona, hata katika hafla za Kitaifa, viongozi wa madhehebu ya dini, wanaalikwa kuliombea amani, utulivu na utangamano Taifa letu? Mbona kabila dogo la Wazanaki, limewahi kutupatia kiongozi ambaye hana mfano wa ubora katika nchi yetu? Sasa takwimu za madhehebu na makabila zitakuwaje tishio kwa siha njema, ustawi na maendeleo yaTaifa, hata katika karne hii ya 21?
Mimi bado siamini kama kweli tumeitumia fursa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu, 2012, kwa manufaa ya kiwango cha juu kabisa cha ufanisi (optimal use, benefit and utility) ilivyowezekana.
No comments:
Post a Comment