Tuesday, October 23, 2012

‘OKUKYALA N’OKUKUKYALILANA’: MILA YA WAHAYA
INAYOHITAJI MTAZAMO MPYA.

                       Na  Festo Mukerebe

Okukyala n’okukyalilana’, ni maneno ya Kihaya ambayo, kwa tafsiri sisisi, ni ‘kutembea na kutembeleana’. Ni sahihi pia kutumia neno okulebangana. Ni moja ya mila za jamii  ya Kihaya, ambazo, kimsingi, nazikubali na kuzienzi sana.
Kutembeleana ni tabia ya kiungwana na kielelezo cha upendo wa wanandugu  katika jamii. Na methali ya Kihaya isemayo: obukwatane kagulu, inathibitisha jinsi Wahaya walivyothamini tabia ya wana ndugu na jamaa kutembeleana mara kwa mara, kama mkakati madhubuti wa kujenga na kustawisha mahusiano ya kidugu ndani ya jamii.
Hata hivyo, leo nimeanza kuiangalia mila hii kwa ‘jicho la mashaka’. Yalianza lini hayo na kwa nini? Nitaeleza.
Kama mfuasi mwaminifu wa mila na desturi mbalimbali za jamii yangu, nilijenga mazoea ya kwenda nyumbani kwa likizo kila mwaka wa maisha yangu ya ajira serikalini. Ni rekodi ambayo sitaishi niisahau maishani mwangu kwamba, kati ya mwaka 1977 nilipoajiriwa kazi, hadi nastaafu kwa maradhi mwaka 2004 ( kipindi cha takriban miaka 30), ni mwaka mmoja tu ambapo niliitumia likizo yangu nzima kwa kubaki kwenye kituo changu cha kazi, Dar es Salaam. Ilikuwa miaka ya 1980. Lakini kutokana na sononeko nililolipata moyoni (nolstagia) kwa kuwamiss wazazi wangu wapendwa, ndugu na jamaa, sikupata kuthubutu au kujaribu tena ‘kuua’ mwaka mzima, bila kwenda nyumbani Muleba, Kagera.
Kusema kweli, kwa miaka mingi tu, niliweza kwenda nyumbani hata zaidi ya mara moja kwa mwaka. Kwa mantiki hiyo, basi, mimi nilikuwa muumini mzuri na mtekelezaji mwaminifu wa falsafa ya msemo niliounukuu hapo awali wa: obukwatane kagulu.
Na wala isidhaniwe kwamba na mimi nilikuwa narejeshewa (au hadi sasa narejeshewa) kwa vitendo fadhila hiyo na wale wote niliokuwa nawazuru kiasi hicho! Hata nilipoanza kuugua sana, hadi miaka minane sasa, sijapata kushuhudia ndugu na jamaa zangu wakija kunitembelea na kunijulia hali au kunisaidia. Ni ukweli mchungu ambao nimelazimika kuuzoea na kudumu nao sasa! Sina hakika tena kama kweli katika maisha,  wema hulipwa kwa wema! Lakini niliache hilo na kurejea kwenye mada halisi ya makala hii.
Mbali na kwenda nyumbani mara kwa mara, nilizoea kuzitumia fursa hizo kusukuma kazi nilizokuta Wazazi wangu wakiangaika nazo, hasa za kilimo. Nadiriki kudai kwamba sikupata kwenda likizo nyumbani ili niweze kupumzika au kustarehe, baada ya kuhenya kazini serikalini kwa vipindi virefu. Kwangu, likizo ilikuwa ni fursa ya kubadilisha aina ya kazi tu na kuwazuru jamaa zangu popote walipoishi. Na jambo hilo halikupata kunisononesha au kunikera kwa namna yoyote ile. Kwangu, safari za likizo, zilikuwa ni safari za Hija!
Miaka michache baadaye, baada ya kujiimarisha vya kutosha kielimu na kikazi, nilianza kujijengea misingi binafsi ya maisha  yangu kifamilia. Nilinunua shamba (ekibanja) kijijini Itoju. Nikajenga nyumba. Nikaoa mke na kuanza kuzaa watoto. Kwa kifupi, nikawa nimeianza safari ya utu uzima ya kujitegemea, hadi hivi sasa.
Nimejifunza nini katika uzoefu wangu na mila hii ya Wahaya, mila ya kutembeleana (okukyalilana au okulebangana)? Nadiriki kusema kwamba nimejifunza mambo mengi. Baadhi yake ni chanya na yanafaa kuendelezwa, lakini yapo mengine hasi, tusiyostahili kuendelea nayo bila kuyahoji kuyafanyia ukarabati.
Tangu nikiwa sijatokomea katika safari yangu ya kusaka elimu na maisha, nilizoea kuona wazee na watu wazima kijijini kwetu wakidamka asubuhi na kupita ujiranini kujulia hali. Siku nyingine, majirani hao nao walipita nyumbani kwetu, kufanya vivyo hivyo. Kauli kama: Waitu mwalozile?, Mwaimukayoge?, Waitu kyabalembaki?, n.k., zilikuwa za kawaida kusikika asubuhi kutoka kwa wazee waliofika mapema kwetu hivyo kutujulia hali. Kauli nyingine ambazo ilikuwa ni kawaida kuzisikia, ni kama vile: Gaya nkaa mbwenu?, Twakililaha?, n.k.
 Aidha, swali kama: Mbele Wagamanyile…?, lilijenga mazingira ya kujulishana matukio yaliyojiri kijijini. Wakati fulani, ilikuwa ni mlipuko wa magonjwa ya binadamu na mifugo, hata vifo. Wakati mwingine, ilikuwa ni matukio ya wizi na ujambazi. Wakati mwingine yalikuwa ni  umbea kidogo kuhusu migongano au mifarakano katika ndoa za baadhi ya wanakijiji, fumanizi, n.k. Na wakati mwingine (kama nilivyowahi kuandika katika mfululizo wa kumbukumbu zangu hizi), ilikuwa ni kuhusu msichana gani alitoroshwa usiku ule. Au ilikuwa ni kuhabarishana tu kuhusu matukio ya uhasama na mapigano ya vijana, hasa siku za sherehe za kijamii na kidini. Lakini mara nyingi, ilikuwa ni kupeana habari ni wapi na nani alikuwa ameleta ‘neema’ kijijini, kwa kugema pombe, lubisi.
Ninachosisitiza hapa ni kwamba wazee walijijengea utaratibu maalum na madhubuti wa kupashana habari zenye manufaa na ustawi kwa jamii yao na makando kando yake. Kwangu mimi,  ni wazee hawa ambao waliasisi dhana nzima ya Daily News. Awali, nilipokuwa  sijaibaini falsafa hii ya ‘Daily News’, sikutambua jinsi wazee, hasa wa sehemu za mbali, walivyojua, kwa mfano, kwamba siku fulani pale nyumbani kwetu au kwingine, kulikuwa kunagemwa pombe, kiasi cha kumiminika kwa wingi siku hiyo kutembelea, tangu asubuhi na mapema kabisa!
Pili, ni matembezi yangu kwa Bibi na Shangazi zangu. Matembezi  ya sehemu za mbali, hujulikana kama okuzinduka. Bibi mzaa Mama, (Ma Paulina Mukabanjabi), aliishi Muyenje, na Bibi mzaa Baba (Ma ‘Zabeti’ Kyompailwe), aliishi Mafumbo, kwa mwanaye, Ta Phillemon. Shangazi yangu, (Ma Alfredina), aliishi Mafumbo; na mwingine, (Ma Vedastina), aliishi Itoju. Kwangu, ilikuwa kama sheria (isiyoandikwa) kuwazungukia jamaa zangu hao (na wengineo) kila likizo niliyokwenda nyumbani. Karibu wote walikuwa ni wajane, wakiishi peke yao.
Kila nilipowazuru makwao jamaa zangu hao, sikukosa kustaajabia furaha na shauku kuu waliyokuwa nayo kwa ujio wangu. Hawakukosa kuniambia,  wakati wa mlo, kwa mfano, jinsi walivyofurahia na kushiba kweli chakula siku ile. Japo walijitahidi kunielewesha nini walikuwa wanamaanisha kwa kauli zao hizo, sikupata kuing’amua mapema maana yake kwa undani wa kutosha.
Leo naelewa maana halisi ya kauli zile.  Nimetambua, kutokana na uzoefu wangu mwenyewe, jinsi inavyokuwa vigumu kwa mtu, hasa aliyewahi kuishi katika mtangamano wa umoja wa kifamilia, kufurahia chakula, bila kukila chakula hicho katika ushirika na watu wengine, hasa jamaa zake. Si Wahaya wenyewe husema: akake okalya na abawe?
Sasa naelewa jinsi inavyowezekana kwa mtu mpweke na mkiwa kupitisha hata siku nzima bila kutia tumboni mlo kamili. Hajisikii njaa wala motisha wa kuingia jikoni na kujishughulisha. Na hata akifanya hivyo, hatakuwa na ‘apetaiti’ ya kutosha kwa chakula hicho atakacholazimika kukila katika mazingira ya ukimya, upweke na ukiwa. Sasa kwa nini asifurahie ujio wako kwake, ujio uliomuwezesha hata yeye mwenyewe kufaidi mkungu bora wa ndizi, alioutenga siku nyingi shambani, kwa matarajio ya ujio wa mgeni maarufu kama ‘wewe’? Si ndiyo siku ambayo alijisikia ari ya kutumia amana ya pato lake kununua kitoweo kizuri au pombe? Hilo nililipata zaidi kwa Shangazi yangu wa Itoju na Bibi yangu wa Muyenje.
Lakini lipo jambo jingine nililolipata zaidi kwa Bibi yangu huyo na Shangazi yangu wa Mafumbo. Bibi yangu, alihakikisha ananitembeza kwa watu mbalimbali kijijini, ikiwa ni pamoja na sehemu ambako pombe zilikuwa zimegemwa na kunywewa. Wakati wote alikuwa anajigamba na kutamba kwamba wakati wa midume ya kijiji  kufyata mikia ulikuwa umewadia!
Alidai kuwa ile ‘midume’ iliyozoea kujipitisha na kumnyanyasa kwa upweke na ukiwa wake, ilipaswa sasa kutambua kuwa yeye hakuwa mwanamke wa hivi hivi tu, kama walivyofikiri kwa kujidanganya. Kwani si sasa walikuwa wamemshuhudia kwa macho yao wenyewe mume wake wa ‘shoka’, aliyekuwa amerejea kutoka mjini? Changamoto yake kwa watu hao ilikuwa: ‘mwenye wivu sasa ajinyonge!’
Vivyo hivyo, Mafumbo kwa Shangazi yangu mwingine. Yeye aliikoga na kuionya ‘mibabe’ iliyokuwa   ikitishia usalama wake, kwa namna mbali mbali, sasa kufikiria mara mbili mbili. Si walikuwa sasa wamemuona ‘kiboko yao’, yaani mtoto wake mwenyewe, aliyekuwa akifanya kazi serikali kuu?’. Sasa na wathubutu tena hata kumgusa tu, kama hawatakiona kilichomtoa  kanga manyoya!
Sasa nihitimishe sehemu hii kwa jambo moja chanya la jumla. Mwaka 1995, kulitokea msiba mkubwa wa Dada yangu, Severina. Msiba ule uliitikisa na kuiumiza sana familia yetu.  Jamaa na ndugu zetu wengi kutoka sehemu mbali mbali walifika nyumbani kuhani. Miongoni mwao, walikuwa ni mabinti wawili, ambao sura zao zilikuwa ni ngeni kabisa machoni mwangu.
Sikuwa mwepesi kuulizia utambulisho wao (identity). Lakini Shangazi yangu mmoja, kama vile alitambua mashaka na udadisi niliokuwa nao kichwani , akaniita pamoja na wale mabinti. Akaanza kutuhoji sote (mbele ya kadamnasi) kama tulikuwa tunafahamiana. Jibu letu sote lilikuwa ni ‘hapana’. Hali hiyo iliwafadhaisha jamaa wote walioshiriki mazungumzo yale. Maana wale mabinti walikuwa ni dada zangu kutoka kijiji cha Kashule, wala si kilomita nyingi sana kutoka kwetu, Kimbugu; nami nilikuwa kaka yao.
Asili yetu ya pamoja ni wahenga wetu, Tilwilukwa na Kagasheki waliohamia kwetu (Kimbugu na Kashule) wakitokea Kihanja Butorogo, takriban miaka 400 iliyopita. Kwa makadirio yangu hayo (yaliyotokana na utafiti wa awali niliopata kuufanya kuhusu historia ya Abasimba ba Butorogo, vimetimu vizazi vinane tangu kuwasili Kimbugu kwa Abasimba hao wa kale. (Kwa takwimu zangu, kizazi kimoja kilidumu kwa wastani wa miaka 50). Lakini kutokana na pande zetu kutotembeleana kwa miongo na miongo, tulikuwa sasa tumeanza kutofahamiana!
 Kila mwanandugu aliyechangia mjadala ule, hakukosa kugusia hatari ya ‘maumbu’ katika ukoo wetu, kuingia katika mahusiano ya kimapenzi au kuoana kabisa, kutokana na kutotembeleana na kufahamiana, kama ndugu wa damu na asili moja. Na sote tunajua jinsi lilivyo jambo la laana, mkosi na hatari kubwa kwa kizazi husika, endapo jambo kama hilo likitokea.    
Hadi hapa, kutembeleana kutakuwa kumejenga taswira wazi jinsi kulivyo sehemu muhimu ya utamaduni wa Wahaya. Lakini, kama zilivyo mila na desturi nyingi, uzuri na umuhimu wa mila hizo, usitufanye tukaendelea kuzishikilia na kuzitumia tu kama zilivyo (intact), bila kuzifanyia tathmini na maboresho, kwa manufaa zaidi na maendeleo ya kijamii kwa nyakati tulizo nazo sasa. Nitaeleza kidogo kwa nini naona hivyo.
Baada ya kuwa nimemaliza kujenga nyumba yangu Kijijini, Itoju, nilikuwa napenda zaidi kuzitumia fursa za likizo zangu kuendeleza shamba langu. Kufanya hivyo, kulijumuisha kupalilia magugu (kulim’omwata) na kuhudumia migomba  (kushalila), kazi ambazo hufanikiwa zaidi zikifanyika asubuhi sana, kabla jua halijachemka.
Kwa bahati mbaya, mimi ni mzito wa kudamka alfajiri kwa kazi hizo, hata nyingine. Na wala sikujishinikiza kuirekebisha tabia hiyo, kwa vile nilihisi kwamba kuwa kwangu likizo, kulinipa uhalalisho wa kupitiliza usingizi kidogo! Sina hakika kama nilikuwa sahihi katika kuendekeza katabia hako ka ‘uvivu kidogo’.
Lakini pamoja na udhaifu huo niliokuwa nao, ilipotokea siku mazingira yakaniruhusu, nikafanikiwa kuamka mapema (saa moja au mbili), nikapiga mswaki na kuelekea kwenye kiunga cha magugu, hadi saa saba hivi, kazi ya maana iliweza kuwa imefanyika, bila ajizi yoyote.
Sasa alikuwepo rafiki na jirani yangu (sasa marehemu), Bwana Philbert. Phil, kama tulivyozoea kumuita kwa kifupi, hakuwa rafiki yangu wa kawaida tu. Ni yeye ambaye, kwa sehemu kubwa, alinisaidia kusimamia ujenzi wa nyumba yangu hapo kijijini.  Haijalishi kwamba naye binafsi alinufaika, kwa namna moja au nyingine, na ujenzi ule. Alikuwa mtu wa karibu.
Kama walivyo baadhi ya watu, ikiwa ni pamoja na Marehemu Baba yangu, Phil alikuwa na uwezo mkubwa wa kudamka alfajiri kabisa. Katika maisha yake, inaelekea kwamba alikuwa ‘ametangaza vita’ dhidi ya magugu shambani mwake.
Kwa hiyo, kila alipoamka alfajiri, alijijitoma shambani kwake na kuchapa kazi kwa bidii hadi saa nne asubuhi, ambapo jua linakuwa linaanza kuchemka. Yeye ndipo aliporejea ndani na kwenda bafuni kukoga. Nusu saa baadaye, aliweza kupiga ‘suti’ na kiatu,  na akatoka kuanza kuwazuru majirani na maswahiba zake, akiwemo mimi.
 Kipindi hicho, mimi ndiyo kwanza shughuli ya shambani kwangu ilikuwa inaanza kunoga na kijasho chembamba kunitoka.  Ghafla, niliweza kusikia: “Olimu waitu?”. Na nilipotaharuki, hakuwa mwingine bali shoga yangu, Phil, aliyekuwa amefika kunitembelea (kunkyalila).
Sasa kwa mila yetu, mtu hawezi kuendelea na kazi yoyote ile wakati anapotembelewa na jamaa, jirani au rafiki. Inalazimu asitishe kila shughuli anayokuwa akiifanya wakati ule na kunyanyuka mara ili kumlaki kindakindaki mgeni wake. Utazisikia “nyegera”, “nyegera”, (“karibu”, “karibu”…) zisizo na idadi zikimtoka mwenyeji, wakati  anahaha kumuelekeza ndani mgeni wake ili kusalimiana, okushulana, na shumalamu waitu zake nyingi   kuchukua mkondo wake . Kwa mila hiyo, ni tabia mbaya na utovu wa heshima kwa mwenyeji kuendelea na kazi katika mazingira ya ujio wa mgeni.
Kwa bahati mbaya, hakuna alama yoyote itakayokujulisha kwamba mgeni wako alikwishakamilisha malengo yake ya kazi shambani kwake. Na kwa vile naye hasemi lolote kuhusu ukweli huo, mwenyeji hatatokea kulitambua mapema jambo hilo. Ni rahisi kubashiri athari za mila hiyo kwa maendeleo!
Lakini mimi niliathirika zaidi. Kwani baada ya maongezi marefu ndani ya nyumba, yakiwa wakati mwingine yanaambatana na okutangilila vinywaji, hasa enkonyagi, kahawa za kutafuna (emwani), n.k., nitashauriwa jioni hiyo tutoke kidogo ili yeye anitembeze kijijini, kusudi nipate kufahamiana na watu mbali mbali wenyeji. Nami, kama mkazi mgeni kijijini, nilihitaji kufahamiana na wenyeji wengi kadiri ilivyowezekana. Kwa utaratibu huo, basi, haikuwa ni ajabu kujikuta nashindwa kutimiza malengo au kuzitumia siku zangu za likizo kwa manufaa ya maendeleo niliyokusudia.
Tarehe 1 Septemba, 2012, nilijikuta naitafakari mila hiyo kongwe ya Wahaya. Siku hiyo asubuhi, mwanangu Elford, akiwa likizoni, alikuwa ameanza na kuendelea na kazi ya kupaka rangi. Ghafla, nikasikia rafiki yake fulani amewasili kumtembelea. Kwa hisia zangu za mila ya kwetu,  ya okukyala n’okukyalilana, nikafadhahika kwa kudhani kwamba kazi hiyo sasa ingalibidi kusimama, pengine hadi siku nyingine. Nilitarajia kumuona mwanangu anamkaribisha (kunyegeza) mgeni wake sebuleni kwa soga na michapo.
Lakini haikuwa hivyo; kwani hata saa nzima baadaye, nilisikia kazi inaendelea kurindima, na wakati huo huo, michapo na maongezi yakiwa yamepamba moto mtindo mmoja baina ya marafiki wawili.
Ndipo nilipotambua kwamba kumbe mila ya kutembeleana inaweza kutekelezwa vizuri tu sambamba na kazi. Nikawa nashangaa kwa nini huko nyumbani haikuwezekana mgeni aliyekukuta katika eneo fulani la kazi, hakuketi pembeni na mazungumzo yakaendelea; au pale ambapo aina ya kazi iliyokuwa ikifanyika iliruhusu, mgeni hakushiriki kwa vitendo kazi ile aliyokukuta unaendelea nayo (kuhwela).
Nilianza kuhisi kwamba mtazamo mpya  wa kutembeleana na kazi ungalikuwa chachu ya maendeleo na tija katika jamii. Lakini pia, ungalipunguza matembezi yasiyokuwa na malengo au tija, matembezi ambayo ni sahihi zaidi kuyaita uzururaji. Uzoefu wangu wa tarehe 1 Septemba, 2012, ulidhihirisha kwamba kutembeleana na kazi, inawezekana!
Labda nihitimishe kwa kutoa changamoto na wito kwa jamii kuzifanyia tathmini mila na desturi nyingi ambazo awali tulizitohoa bila kuhoji manufaa yake kwetu na jamii zetu leo. Mfano mmoja hapa ni  mila nyingine ya Kihaya ya kusindikizana, okushendekelezangana. Nimekuwa nikiwabeza kina mama wengi walioizamia kwa kupitiliza mila na desturi hiyo. Utakuta mwanamke anamtembelea shoga yake. Kwa muda wa saa mbili, wataongea sebuleni. Baadaye watahamia kibarazani au nje, chini ya mti, kusukana nywele. Na wakati wote huo, maongezi yao yataendelea mtindo mmoja.  Utaamini kwamba wameongea mengi hadi yakaisha.
Ukiamini hivyo, utakuwa umekosea sana.  Maana baada ya hapo, utamuona mgeni anaaga kuondoka, na mwenzake ananyanyuka kumtoa, kumsindikiza. Ndipo utakapotambua jinsi mila ya kusindikizana nayo ilivyo kikwazo kwa matumizi ya muda kwa manufaa.
Mchakato wa kusindikizana unaweza kuchukua zaidi ya saa nzima. Mwenyeji anaweza kumsindikiza jirani yake hadi nyumbani kwake kabisa. Na huko maongezi yakawa yameanza upya, hadi pale inapolazimu yule aliyesindikizwa sasa ageuke kuwa msindikizaji.
Kama hamasa ya ushoga wa wawili hao bado inachemka, usishangae kuwaona  wawili hao wanasindikizana na kurejea tena nyumbani kwako, walipoanzia. Hapo, sasa tujiulize kama kweli mila ya namna hiyo, mila yenye kuendekeza maongezi yasiyokuwa na mwisho (umbea?), inaweza kutufikisha mbali!  Mimi sidhani.
Pamoja na hayo, hatuna budi tukubali na kukiri kwamba mila na desturi zetu nyingi zilikuwa na mantiki na manufaa makubwa. Katika uchambuzi wa mila ya okukyala n’okukyalina, kwa mfano, tulijadili dhana ya Daily News, na kuona jinsi mila hiyo ilivyoweza kutumika kama chombo maridhawa cha kueneza habari vijijini. Hatuhitaji kukumbushwa kwamba enzi za kale, wakati mila na desturi hizi zinaasisiwa, hapakuwapo na media kama tulizo nazo leo hii, yaani magazeti, radio, TV, n.k. Wala hapakuwapo na simu kwa ajili ya mawasiliano ya masafa.
Hapo katikati, wenzetu wa mataifa yaliyotutangulia katika elimu ya sayansi na teknolojia, walivumbua aina mbali mbali za mawasiliano kwa maandishi: barua, telegram, telex na fax. Kabla ya uvumbuzi huo, ilikuwa ni lazima watu wawasiliane kwa kutembeleana na kuongeleshana. Waliweza kupelekeana zawadi mbalimbali kwa kutumia mila zao nyingine, kama vile okuzilima,  okutwela, okukulata, okuganuza, okubisila, okutangilila, okubegela, okubegana, okugabila, okugemula, n.k. Hata watu waliotenganishwa na masafa marefu, walifikishiana taarifa kwa midomo yao wenyewe, au kwa kutumia matarishi (entumwa) na wajumbe.
Na tarishi, mjumbe au mtu aliyerejea kutoka kukyala au kuzinduka, kukulata, n.k., aliwajibika kusimulia kwa kituo kila jambo aliloshuhudia safarini, okubaluhla au okutebya . Msimuliaji mzuri, omubaluzi, aliwawezesha wale ambao hawakwenda, kujisikia sawa na wale waliokuwa kwenye msafara. Ni bahati mbaya, kwamba okubaluhla, ni mila ambayo nayo inayoyoma kwa kasi.
Hadi miaka ya karibuni, njia mbalimbali za mawasiliano zilitumia muda mrefu. Enzi mimi nikiwa nasoma sekondari, kwa mfano, barua ya kawaida kutoka Tabora hadi Kagera, ilichukua wiki mbili, tatu, au hata zaidi.
Japokuwa sina takwimu za kunisaidia kuthibitisha rai yangu, mawasiliano kwa njia ya barua leo, yamepoteza mvuto kwa kiasi kikubwa, kufuatia uvumbuzi wa electronic media, hasa simu za mezani na hasa za kiganjani. Gunduzi nyingine za teknolojia ya mawasiliano zinaangukia katika nyanja ya mitandao, networks, kama vile e-mails, face book, twitter, you tube, jamii forums, you name it! Katikanyanja hii, nina hakika na msemo wa Waingereza, kwamba: ‘the sky is the limit’.
Kadiri gunduzi hizi za teknolojia ya mawasiliano zinavyozidi kushamiri, kuenea na kuwafikia watu wengi, hata vijijini, ndivyo mila na desturi zetu za jadi za mawasiliano, zinavyozidi kupoteza nafasi na umuhimu. Na sioni kama jambo hili  linahitaji usomi wowote kulimaizi. Kwani, licha ya kuenea kwa simu za kiganjani, kwa mfano, watu wenyewe, hata ndugu na jamaa,  hawaonyeshi ari ya kuwasiliana na kutembeleana, kama ilivyokuwa enzi zilizopita.
Binafsi, nakumbuka jinsi ilivyokuwa haiwezekani kwangu kupitisha wiki nzima bila kuijibu barua aliyonitumia ndugu, jamaa au rafiki yangu, licha ya kwamba nilihitaji kujiandaa kwa karatasi, bahasha, stempu na muda wa kuiandika na kuipeleka posta barua yangu ya majibu.
Siku hizi, licha ya kuenea kwa umiliki wa simu za kiganjani (na kuibuka kwa mitandao mingine lukuki), inayorahisisha na kuharakisha mawasiliano baina ya watu, jamaa, ndugu na marafiki, hatuoni mawasiliano hayo kutumika kwa kishindo na vuguvugu kama ambavyo ingalitarajiwa.
Kama huu sio uzoefu wangu binafsi tu, ni muhimu wachambuzi na watafiti katika taaluma hii, wakabashiri na kutujuza hatma na athari za muda mrefu za mazingira yote haya, kwa maendeleo ya teknolojia za mawasiliano, na kinyume chake (vice versa).  Ni changamoto tu!

No comments:

Post a Comment