Tuesday, October 23, 2012

MDAHALO WA NELSON WA CHANYA NA HASI YA MATUMIZI YA SIMU ZA KIGANJANI NA UZOEFU WANGU KATIKA KILIMO NA BIASHARA YA ZAO LA NYANYA ENZI ZA MAREHEMU BABA YANGU BUKOBA

                                 Na  Festo  Mukerebe
Tarehe 21 Septemba, 2012 ilikuwa ni siku ya Jumamosi. Ilikuwa ni mara yangu ya pili au ya tatu kubaini mwanangu Nelson akiondoka nyumbani asubuhi na kurejea jioni. Kwa vile hiyo haikuwa ni kawaida yake tangu miaka ya awali, kuhudhuria masomo shuleni siku za Jumamosi, nilikuwa nimekwishahojiana naye kuhusu mabadiliko hayo. Naye alikuwa tayari amenipatia maelezo ya kuridhisha mintarafu mabadiliko hayo.
Hata hivyo, siku tajwa hapo juu, nilirudia kumhoji kuhusu jambo hilo hilo. Naye akanieleza kwamba kwa siku hiyo, yeye na wanafunzi wenzake wa Kidato cha Tatu na Nne, walikuwa wamealikwa kushuhudia (na kushiriki?) mdahalo wa Kidato cha Tano na Sita shuleni kwao – mdahalo uliohusu faida na hasara za kumiliki simu za mkononi. Bila shaka hoja hiyo iliwahusu na kuwalenga wanafunzi wenyewe.
Nilihisi kutaka kujua jinsi wachangiaji wa mjadala ule walivyodadavua na kujenga hoja na misimamo yao. Kwa bahati mbaya, hapa sikuambulia maelezo ya kukidhi. Maana Nelson aliishia kukumbuka mchangiaji mmoja tu aliyedai kwamba simu zina matokeo ya kuwatia umasikini wamiliki wake, kutokana na ununuzi wa kila mara wa vocha za muda wa kuwa hewani.
Maelezo hayo kiduchu yaliniongezea kiu ya kutaka kujua zaidi. Lakini kwa vile Nelson hakuelekea kuwa na cha maana zaidi kutosheleza kiu yangu, nilijikuta mimi mwenyewe sasa nashindwa kudhibiti hamu yangu ya  kuchangia mdahalo nisioalikwa, Nelson akiwa ndiyo hadhira yangu ya pekee!
Uchu wangu ulinipeleka takriban mwaka 1965. Kadiri ya kumbukumbu zangu, ambazo zimekataa kufutika kichwani hadi sasa, ni kipindi hicho Marehemu Baba yangu, kwa kushirikiana na wanaume wengine wachache kijijini kwetu, Kimbugu - Bulwani, waliasisi kilimo cha mboga mboga, hususan nyanya na kabeji – kilimo ambacho kilileta mabadiliko makubwa katika uchumi na maisha ya wanaume wale wa shoka walioshiriki kilimo kile na (sisi) familia zao.
Kwa kusema hayo, sina maana kwamba wazee wale walitajirika sana kutokana na mabadiliko hayo. Lakini naweza kusema kwa kujiamini kabisa kwamba kuanzia wakati huo, maisha ya familia zetu hayakurejea nyuma.
Mwaka ule wa 1965, kwa mfano, Baba aliweza kuboresha makazi yetu kwa kufanikiwa kujenga nyumba aina ya banda yenye kuezekwa kwa bati, badala ya tetei aliyoijenga miaka mimi nazaliwa, 1952 - 1953. Nakumbuka jinsi nilivyoshirikiana naye kusomba nguzo, mabati na maji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ile ya banda (wengi hawaelekei kulijua hilo), ambayo bado ipo hadi hii leo.
Mwaka 1966, Baba aliinyanyua juu hadhi ya familia yetu kwa kuanza kufuga ng’ombe wachache aliowamiliki mwenyewe kutokana na mapato ya biashara ya nyanya. Nakumbuka jinsi nilivyoshirikiana naye kuwaswaga ndama wawili (na wengine walioongezeka baadaye) kuwaleta nyumbani. Ndugu na jamaa zangu wengi hawaelekei kulitambua jambo hilo la kihistoria. (Au labda wanalipuuza tu kwa nia mbaya!)  
Idadi ya ng’ombe wa Baba iliongezeka taratibu sana kwa sababu ya maradhi ambayo hayakuepukika kutokana na uhaba wa taaluma stahiki katika nyanja ya ufugaji na huduma zinazohusika nayo. Wakati anaitwa kutangulia mbele ya haki, Baba yangu hakuweza kuvuka idadi ya ng’ombe 15 ambao wote waliishia mikononi mwa survivors wachache mafisadi  . Lakini ni ukweli usiopingika kwamba ng’ombe hao walimjengea hadhi kubwa (yeye na hata sisi) katika jamii, na kutupa  sisi ‘wasomi’, uhakika wa kusonga mbele shuleni.
                Lakini, kilimo cha nyanya ndicho pengine kilichotujenga zaidi kuliko kitu kingine chochote katika maisha. Huwa napenda kuamini kwamba kama kilimo hicho kingalitendeka mnamo mazingira ya miaka tuliyo nayo, basi Baba yangu asingalifariki au tukiwa masikini. Na hili hasa ndilo linaloniunganisha na mdahalo wa Nelson kuhusu hasi na chanya ya simu za kiganjani shuleni kwake.
Tangu nikiwa darasa la Tano, mwaka 1965, ‘tulilima na kulimaga… tulipanda na kupandaga’. Misitu mikubwa ya kiasili kama Nkomelo, Kyakatoto, Lubezi, Kyente, Kamusholelwa na mingineyo, iliangamia kwa mapanga, mashoka na majembe ya familia za wazee waliokuwa serious farmers (Baba yangu, Mzee Frederick Kalumuna, Mzee Paulo Bitambi, Mzee Mwamudu Hassan Kagengele, Mzee Bayubi, Mzee Celestin Lubunu, Kijana Abubakar Mwamudu na wengine wachache ambao nimewasahau). Sina hakika na hukumu ya wanaharakati wa hifadhi ya mazingira! Lakini katika hili, siwatarajii waibuke na nishani kwa ajili yetu!
Mchakato wa kilimo kile ulianza na wazee kukagua msitu unaolengwa kushughulikiwa na kufikia muafaka na wamiliki wake. Baada ya hapo, mapanga na mashoka makali yalinolewa na kufanya kazi, kabla ya familia zetu hazijapinda migongo kuutifua udongo wenye rutuba nyingi na pengine usiopata kulimwa tangu enzi za kale. Ndipo mbegu za money maker, drum head na nyinginezo ziliposihiwa katika vitalu na miche kupandwa. (Kwa bahati mbaya, sikuwahi kuona mistari inazingatiwa!). Hatua hiyo ilifuatiwa na umwagiliaji kwa kutumia keni, vidumu, karai, sufuria, vibuyu na vyombo vingine vilivyoweza kupatikana katika kaya zetu. Ilikuwa ni lazima mashamba (emisiri) yawe jirani kabisa na vyanzo vya maji (chemichemi, mito na ziwa) ili kuwezesha kazi hiyo (iliyofanyika majira ya kihangazi) kufanyika kwa ufanisi.
Mchakato wa umwagiliaji na palizi (mbili) ulifuatiwa na kazi ngumu kadhaa. Moja ya kazi hizo ilifanyika usiku, ikihusu ulinzi dhidi ya wanyama waharibifu, hasa viboko. Kazi hii ilifanywa na wazee na vijana waliokuwa na umri mkubwa. Kazi yingine ilikuwa ni kuchuma na kusomba nyanya hadi nyumbani. Pengine hii ndiyo kazi iliyotutoa jasho jingi zaidi kuliko kazi nyinginezo. Kwa maana, kama ilivyokwishadokezwa, nyumbani kwetu (pakiwa mwanzoni mwa plateau ya kwanza kutoka Ziwa Viktoria) panatenganishwa na ukanda wa pwani na safu ya  mlima mkali ambao ilibidi tuupande tukiwa na matenga mazito ya nyanya vichwani mwetu. Kwa kawaida, kazi ya kuvuna na kusomba nyanya hizo kutoka ufukweni mwa Ziwa Viktoria, ilifanyika mara mbili kwa siku.
Na hata hadi hapo, kazi ilikuwa bado ni mbichi kabisa. Maana baada ya siku kama mbili hivi, ililazimu tupakie upya nyanya hizo katika matenga na kuyabeba matenga hayo hadi barabarani Kibahoni, ambapo tuliyasetiri msituni kwa usalama. Alfajiri kesho yake, tulidamka mapema na kuyapanga barabarani, kusubiri usafiri wa mabasi yaendayo Bukoba Mjini kwa mauzo.
Kabla sijatokomea Kahororo mwaka 1968 kwa elimu ya Sekondari, niliweza kusafirisha nyanya za Baba mara mbili au tatu hivi, hivyo kuwa na uzoefu na uelewa wa kutosha kuhusu yaliyojiri baada ya basi tulilosafiria kuwasili stendi ya mabasi mjini Bukoba.
Tuliweza kuipima hali ya soko mara baada ya kuwasili stendi na kuanza kuyateremsha matenga yetu. Iwapo ulilakiwa kwa kuzongwa na umati wa wafanyabiashara ya nyanya kutoka soko kuu la mji, basi ulikuwa na kila sababu ya kuwa na faraja kwamba kulikuwa na uhaba mkubwa wa zao hilo huko sokoni na hivyo kwamba bei kwa siku hiyo ilikuwa ni nzuri. Kwa mujibu wa Marehemu Baba yangu, sasa uliweza kuiwasha sigara yako na kuivuta kwa matumaini na madaha, ukiwaachia wafanyabiashara kazi ya kushughulika na uteremshaji wa matenga.
Lakini endapo ulijikuta ukiandamwa na watoza ushuru wa halmashauri ya mji tu, basi ulilazimika kubwaga moyo kwamba siku ile soko lilikuwa tayari limefurika nyanya, hali ambayo ilikuwa na athari ya kushusha bei ya zao hilo siku hiyo. Na siku kama hiyo, wafanya biashara walicheza mchezo mchafu. Bila huruma yoyote kwa wakulima waliosafirisha mazao yao kwa gharama kubwa, walibana kutoa bei hadi jioni wakati mabasi yanaanza kurejea vijijini. Ndipo katika kiwewe cha kuachwa na mabasi hayo, wakulima hawakuwa na jinsi yoyote ile bali kuuza mazao yao kwa bei ya kutupa! (Sikuona waliokuwa na ndugu au jamaa wa kufikia mjini Bukoba).
Kinasimuliwa kisa cha mzee Celestin Lubunu ( huyu aliwahi kupigana vita ya pili ya dunia, akiwa askari katika jeshi la kikoloni la Waingereza nchini, King’s African Rifles, ambaye hakuwa tayari kuzikubali kirahisi nyanyaso za wafanya biashara wa sokoni. Tofauti na baadhi ya wakulima wenzake waliolazimika kuzimwaga jalalani nyanya zao zilizokosa soko, Mzee Celestin alifanya hivyo baada ya kuzipondaponda na kuzichanganya na uchafu. Alikuwa amegundua kwamba baada yawaokuondoka, wafanya biashara wajanja walikuwa wanachakura majalala na kuziokota nyanya zilizotupwa humo, na kisha kuziosha kwa maji,  ili kesho yake wazifanyie biashara safi kama kawaida, bila kugharamika nazo kwa lolote!
Endapo mawasiliano ya simu za mkononi yangalikuwa tayari yamevumbuliwa enzi hizo, madhila yote hayo yasingeliwakuta kina Baba na wakulima wenzake masikini. Wangaliweza kuitathmini hali ya soko kila siku kabla ya kusumbuka na usafirishaji wa ‘mzigo’ mzito, hadi hali ya soko itulie au itoe bei yenye tija zaidi. Vyovyote vile, wangaligharamika kidogo kwa kununua vocha za muda wa maongezi hewani. Lakini manufaa ya kufanya hivyo, yangalikuwa makubwa sana kuliko hasara waliyoipata kutokana na ukosefu wa mawasiliano hayo.
Hadi wanaaga dunia, nina hakika kwamba baadhi ya wale wazee, kama sio wote, wangalikuwa wakimiliki hata vyombo vya moto kama vile pick-up au malori na outboard engines kwa ajili ya kusafirisha matenga ya nyanya na magunia ya kabeji hadi masoko makubwa zaidi ya miji ya mbali kama Mwanza, Shinyanga na Tabora. Si ni dhahiri kwamba kwao umasikini ungalikuwa bye bye? And why not?      


No comments:

Post a Comment