JINSI WANASIASA WETU WALIVYOITUNISHIA MISULI MALAWI.
Na Festo Mukerebe
Miaka michache baada ya uhuru, Tanzania na Malawi almanusura zitiane maungoni. Wakati ule, tulizitambua sababu mbili za msingi, ikiwa ni pamoja na mzozo wa mpaka baina ya nchi zetu mbili. Lakini sababu nyingine ilikuwa ni tofauti zetu za kisiasa. Tanzania, tangu mwanzoni kabisa, ilijipambanua kwa kuunga mkono msimamo ulioasisiwa awali na Rais wa Ghana, Osagyefo Kwame Nkrumah, kwamba uhuru wa nchi zetu moja moja barani Afrika hauwezi kuwa kamili na endelevu hadi hapo nchi zote za bara letu zitakapokombolewa kutokana na utawala wa kikoloni.
Kwa bahati mbaya, wenzetu Malawi wao walijiweka kando na msimamo huo wa kimapinduzi. Kwani sisi tukiwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi kusini mwa bara la Afrika (na Afrika kwa jumla), Rais wao alijenga mahusiano ya kirafiki na mahasimu wa harakati zetu za ukombozi, makaburu wa Afrika ya Kusini, waliopepea siasa za ubaguzi wa rangi . Isitoshe, Rais Ngwazi Hastings Kamuzu Banda siku zote alituangalia jicho baya, hasa tulipowapokea wapinzani wake kisiasa walioafikiana na msimamo wetu na kupenda kushirikiana nasi kutimiza ndoto na malengo ya ukombozi kamili wa bara la Afrika. Tokea miaka hiyo, Marais wetu hawakuwahi kupikika na kuiva katika chungu kimoja.
Ni chuki hiyo, iliyotufanya tuishi katika wasiwasi mkubwa miaka hiyo, tukihofia kushambuliwa na Makaburu moja kwa moja au kupitia kwa vibaraka wao, kina Rais Banda wa Malawi.
Nakumbuka mbio za mchakamchaka tulizokimbia kila alfajiri mnamo miaka ya 1960 na 1970, tukiwa tunajiweka katika siha njema kuweza kuzikabili changamoto za kusini, kama lingalikuja kutokea jambo la kutokea! Haukupita muda ikalazimu Watanzania tuongeze juhudi hizo kutokana na tishio jingine la usalama kwa nchi yetu kutokea kaskazini, ambako Dikteta Nduli Idi Amin alikuwa ameipindua kwa mabavu serikali ya muasisi wa Taifa la Uganda, Rais Milton Obote, mwaka 1971.
Hapo nako, tulikuwa tumemkaribisha na kumpa hifadhi mwana wa Afrika, Milton Obote, ambaye - akiwa na wenzake, kina Nyerere na Rais Kaunda wa Zambia huko Singapore, Malaysia, kutetea msimamo wa harakati za ukombozi wa Afrika, katika mkutano wa Jumuiya ya Madola, nyumbani kwake jeshi likachukua madaraka yauongoziwa Taifa kwa mabavu.
Kwa miaka minane, tulilazimika kuvumilia choko choko za Dikteta Amin, mpaka aliporogwa kuvuka mpaka na kuliteka eneo letu la Missenyi mwaka 1978 na kulitangaza kuwa sehemu ya Uganda. Kwa kufanya hivyo, Amin alikuwa ametutangazia vita Watanzania na sasa hatukuwa na kazi nyingine, bali kumpiga! Na katika harakati za kumpiga huko, tulifanikiwa kumuondoa ndani ya nchi yetu, kuikomboa nchi ya Uganda na kuukabidhi utawala wa nchi hiyo kwa wazalendo na wapenda maendeleo.
Wakati wote huo, mahusiano yetu na Malawi yaliendelea kuwa lukewarm, ingawa uhasama halisi ulielekea kumalizika pale Rais wa Maisha, Kamuzu Banda, alipofariki dunia.
Kumbe mzozo wa mpaka ulikuwa haujesha kabisa, kama tulivyokuja kubaini mwaka huu, mzozo huo ulipolipuka tena na kuwafanya baadhi ya watawala wetu watunishe misuri, watambe na nusura watangaze vita kamili dhidi ya Malawi, kwa namna yao. Hakuna awezaye kufahamu kama waliwasiliana na Amiri Jeshi Mkuu wa nchi yetu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kabla ya kutoa kauli zao za majigambo kwa umma. Labda walifanya hivyo, wakati kiongozi wa nchi yetu akiwa katika safari zake ng’ambo au likizo. Na kama hawakufanya hivyo, mbona mwenyewe hajawahi kusikika akiwakemea hata mara moja? Au ndilo ombwe lenyewe la uongozi linalosemekana kuizonga nchi yetu kwa miaka mingi sasa? Mimi binafsi sijui.
Lakini turejee kilichojiri mwaka huu. Zilianza kusikika tetesi kwamba Malawi ilikuwa imeyapa leseni za uwekezaji makampuni kadhaa ya nchi za magharibi kufanya utafiti katika Ziwa Nyassa (?) ili kubaini kuwepo kwa raslimali za mafuta na gesi. Ni wazi kwamba Tanzania haikushirikishwa katika mipango hiyo. Ndiyo maana ilishituka mno ndege za uchunguzi huo zilipoonekana zikirandaranda katika anga za eneo zima la Ziwa Nyassa (?) kwa minajiri hiyo.
Tangu enzi zile za Rais Kamuzu Banda, hoja ya Malawi ilikuwa ni kwamba Ziwa lote lile lilikuwa ni mali ya Malawi kwa asilimia 100%. Hoja hiyo inashadidiwa na ukweli kwamba, bila hata kuzishirikisha nchi nyingine mbili zinazopakana na ziwa hilo, Tanzania na Msumbiji, Malawi walilibatiza ziwa hilo kwa jina la Malawi, ambalo ni sawa na jina la la baadaye la nchi yao.
Hatua hiyo inashangaza, kwa sababu tangu enzi za ukoloni, ziwa hilo lilitambulika kama Ziwa Nyassa, wakati huo bado Malawi inaitwa Nothern Nyassaland. Hatuna ugomvi na nchi hiyo huru kubadilisha jina lake au la ziwa lile.
Na zipo nchi nyingi barani Afrika zilizofanya hivyo. Mifano michache ya nchi zilizojipa majina mapya, ni pamoja na Zimbabwe, DR Congo, Tanzania, n.k.
Pamoja na utashi wa nchi husika katika suala hilo, sisi hatudhani kwamba ni sahihi kwa nchi moja peke yake kubadili jina la raslimali inayotandaa mpaka, bila mashauriano na jirani wengine wanaohusika.
Najiuliza, Kwa mfano, kama sisi Tanzania (baada ya kuachana na jina la Tanganyika), tunaweza kudiriki kulibadili Ziwa Tanganyika na kuliita Ziwa Tanzania (au jingine lile) bila mashauriano yoyote na jirani zetu, DR Congo, ambao tunashirikiana na kugawana ziwa hilo?. Vivyo hivyo, Ziwa Viktoria. Je, hivi kweli inawezekana sisi Tanzania tuamue kulibatiza ziwa hilo kwa jina tofauti, bila mashauriano yoyote na majirani zetu, Kenya na Uganda, ambao mipaka yetu inakutana katikati ya rasilimali hiyo? Hiyo kweli itakuwa diplomasia ya ujirani mwema? Ni wazi kwamba jibu ni hapana!
Kwa hoja hiyo, baadhi yetu tunashangazwa na kitendo cha nchi yetu kukaa kimya miaka mingi tokea jirani yetu Malawi aanze kuliita ziwa hilo kwa jina la Malawi, badala ya Ziwa Nyassa, jina lake la enzi! Haieleweki; wala haikubaliki. Mbona hata OAU iliazimia mapema kabisa kuendelea kuitambua mipaka iliyowekwa na kuachwa na wakoloni, japo kimsingi hatuipendi? Au tuseme kwamba OAU haikuona mantiki ya kuazimia juu ya majina ya raslimali zinazotandaa na kukatiza mipaka?
Malawi inapojihalalisha kumiliki ziwa lote la Malawi, kama yenyewe inavyoliita, inanukuu Mkataba wa Kimataifa wa Heligoland (Anglo-German Treaty) wa mwaka 1890 baina ya Ujerumani na Uingereza, ambazo ndizo zilizitawala nchi zetu jirani (Tanzania na Malawi) kwa mujibu wa Mkataba wa Mkutano Mkuu wa Berlin (Berlin Conference) wa mwaka 1884-85, ambao ndio uliweka misingi na vigezo vya kuligawa bara la Afrika katika maeneo ya kikoloni. Mkataba huo unaainisha mpaka wa Tanzania na Malawi kuambaa ziwa Nyassa ufukweni na Tanganyika.
Lakini Tanzania, kwa upande wake, nayo inanukuu mkataba wa Waingereza wa miaka ya 1930 kuhusu mpaka huo, ambao uliwekwa katikati ya Ziwa Nyassa. Na kwa lugha ya wenyeji wa makabila yanayoishi katika mwambao wa ziwa hilo, neno nyassa linabeba maana ya ‘maji mengi’.
Tusisahau hapa kwamba Tanganyika ilianza kutawaliwa na Uingereza kama mdhamini wa umoja wa mataifa wa kale (League of Nations) , baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita ya Kwanza ya Dunia, 1914-1918, ambapo Ujerumani iliadhibiwa kwa kunyang’anywa makoloni yake, ikiwamo Tanganyika.
Pamoja na maelezo hayo hapo juu, inabainika wazi kwamba yapo mambo kadhaa ambayo yanaweza kuendelea kuzua utata kama hayakujadiliwa na kuwekwa sawa kidiplomasia kwa uwazi na ukweli, baina ya nchi hizi mbili huru, kwa maslahi ya pande zote mbili.
Ingawa hatuna taarifa za kutosha juu ya matokeo ya mazungumzo ambayo inaelekea yameanza kwa ngazi ya mawaziri na marais, Kikwete wa Tanzania na Joyce Banda wa Malawi, tunaamini kwamba muafaka wa amani utafikiwa sio muda mrefu ujao. (Wakati makala hii inaandikwa, zimesikika habari kwamba kwa sasa mazungumzo hayo yameahirishwa hadi tarehe 10 Septemba 2012 ili kuwapa wataalamu wa masuala ya migogoro hii kuwasilisha kile ambacho Waziri Membe amekiita options za utatuzi.
Jambo linalokera na kutia mashaka hadi sasa, ni hawa wanasiasa wetu ‘waheshimiwa’. Wakati wa mawasilisho ya Hotuba ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika Bunge la Bajeti la mwaka huu 2012/13, suala la mgogoro wa mpaka baina ya Tanzania na Malawi juu ya Ziwa Nyassa, limeibuka upya. Mbele ya Bunge hilo, baadhi ya viongozi waandamizi, ikiwa ni pamoja na Waziri huyo mwenye dhamana, Bernard Membe, walisikika wakitamka kwa matambo kuwa Tanzania ilikuwa tayari kwenda vitani kama Malawi ingekaidi amri halali ya Tanzania ya kuwataka kusitisha mara moja shughuli zake za uchunguzi wa mafuta na gesi katika ziwa hilo, hadi suluhu juu ya mgogoro uliodumu kwa miongo mitano sasa, ipatikane kwanza.
Waziri Membe alielekea kufungulia bomba la maji pale Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akiwa anakaimu nafasi ya Waziri Mkuu, naye alipopigilia msumari huo huo wa kuitia adabukijeshi Malawi kwa madai yake ya kujihalalishia umiliki wa Ziwa lote la Nyassa.
Naye Edward Lowassa, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, hakuwa tayari kubaki nyuma katika mbio za kutoa kauli zinazoashiria kwenda vitani dhidi ya Malawi.
Wachunguzi wa mambo ya siasa za Tanzania, tayari wamewashitukia viongozi wanaoshabikia vita dhidi ya Malawi. Inatambulika kwamba viongozi hawa wako mstari wa mbele wa mbio (zisizoanza rasmi bado) za kusaka tiketi ya kugombea urais wa Tanzania mwaka 2015. Inayumkinika kwamba wanasiasa hawa wanalenga kujinasibu kama viongozi jasiri wanaofaa kukabidhiwa hatamu za uongozi wa nchi wakati ukiwadia, 2015.
Lakini Watanzania wengi walioshuhudia vita ya Kagera dhidi ya Nduli Idi Amin wa Uganda mwaka 1978-79, hatuelekei kuvutiwa na misimamo ya kibabe ya viongozi hawa wasaka madaraka.
Ziwa Nyassa, kwa akili na mantiki ya kawaida, ni mali ya urithi wa watu wote wanaozunguka ziwa hilo. Isitoshe, tafiti zilizopo, zinabainisha kwamba makabila ya eneo la Ziwa Nyassa, yameenea katika nchi zote tatu zinazoshirikiana mipaka yake katika ziwa hilo, yaani Tanzania, Malawi na Msumbiji. Kwa manufaa ya kumbukumbu, makabila hayo ni Wanyassa, Wanyakyusa, Wangoni, Wamatengo, Wandali, Wanyanja, Wanyiha, Wayao, n.k.
Makabila haya ya bonde la Ziwa Nyassa, yana asili, utamaduni na shughuli zinazofanana. Na kwa miaka lukuki, watu wote hao wameendesha maisha yao kwa kutegemea ziwa hilo, kwa namna moja au nyingine. Ni mipaka iliyowekwa na wakoloni kwa maslahi yasiyowahusu wao (wakazi wa bonde la Ziwa nyassa) inayowatenganisha hadi leo.
Sisi tunaochelea mkakati wa vita kama suluhisho sahihi na lenye busara la kumaliza mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi, licha ya uzoefu wetu wa kutisha wa Vita vya Kagera, tunayo sababu ya ziada, ambayo (bahati mbaya) wanasiasa wetu wasiokuwa na mzio na umwagikaji wa damu, hawaioni.
Ni kweli kwamba nchi yetu ni Taifa jasiri, ambalo baada ya ushindi wa kishindo wa Vita ya Kagera, sio rahisi kufyata mkia mbele ya nchi ndogo kama Malawi. Lakini tunatambua kwamba katika enzi za vita vya kileo, ukubwa wa nchi na idadi ya watu wake sio vigezo pekee vya kuamua ushindi.
Hilo ni jambo moja. Lakini lipo jingine, ambalo baadhi yetu tunaliona kama tatizo la msingi kabisa. Tulipokusanya nguvu kitaifa na kupambana na Nduli Amin hadi kumtia adabu kijeshi katika uwanja wa vita, mwaka 1978-79, tulikuwa na amali zilizotusaidia katika mapambano hayo. Tunaona mantiki ya kujiuliza sasa kama hizo amali bado tunazo hadi leo, kabla ya kufakamia wazo la kukabiliana na Malawi katika medani ya kijeshi.
Amali ya kwanza, iliyochangia mafanikio yetu nchini Uganda ni haiba ya adui wetu. Idi Amin alikuwa amechukua madaraka ya nchi kwa mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais wa nchi hiyo, Dk. Milton Obote. Kwa vyovyote vile, wapo Waganda ambao hawakupenda utawala wa Obote, na pengine ndio hao kina Amin waliomuondoa madarakani kwa mtutu wa bunduki. Lakini kama tulivyothibitisha wakati majeshi yetu yalipoingia nchini Uganda, raia wengi wa nchi hiyo hawakuunga mkono utawala wa kidikteta huyo. Hawa waliunganisha nguvu zao nasi hadi ushindi kupatikana. Ndio hawa kina Yoweri Kaguta Mseveni, Rais wa sasa wa nchi hiyo.
Malawi inaongozwa na mwana mama, Joyce Banda, ambaye amechukua hatamu za uongozi wa nchi yake hivi karibuni, kufuatia kifo cha Rais aliyemtangulia, Bingu wa Muthalika. Tuna sababu ya kudai kwamba Joyce Banda aliingia madarakani nchini Malawi kwa misingi ya kidemokrasia. Japokuwa mama huyo hawezi kukosa mahasimu wa kisiasa nchini mwake, ni mapema mno kudhani kwamba utawala wake umekwishawachusha sana wanananchi wake kiasi kwamba wapiganaji wetu wanaweza kutarajia kuingia nchini humo kwa vigelegele na vifijo, kama tulivyopokelewa nchini Uganda. Tunahitaji muda mrefu zaidi kuisoma political landscape ya Malawi.
Pili, ni uongozi wa pekee wa Baba wa Taifa, Rais Julius Kambarage Nyerere. Hatudhani kwa dhati kwamba wapo watanzania wanaoweza kubeza vipaji vya uongozi alivyokuwa navyo Baba wa Taifa. Wote tulishuhudia hekima, busara na ujasiri wake kipindi chote cha Vita ya Kagera. Kwamba sifa hizo zilimfanya apendwe, aaminiwe na kukubaliwa kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu, ni ukweli usiokuwa na ubishi miongoni mwa Watanzania. Wako wapi leo, Watanzania tujiulize, viongozi wa ‘kaliba’ ya Nyerere wenye uwezo wa kutuongoza nadi ushindi wa hakika vitani?
Natamani Watanzania waitafakari hali ya uongozi tulio nao nchini hivi sasa, ili hasa tujiridhishe kuhusu uwezo wake wa kutushawishi tujitoe muhanga kumwaga damu yetu na hata kulifia Taifa. Kwa lipi la mno? Ukiona Watanzania wanadiriki kugomea zoezi la kawaida tu la Sensa ya Watu na Makazi, 2012, kwa mfano, utatarajia nini katika ushiriki wao katika zoezi hatarishi la Vita? Kwa uzalendo upi na kwa maslahi ya nani?
Tuhitimishe hoja hii kwa kuitupia jicho zaidi hali ya uzalendo tuliyo nayo nchini hivi sasa. Uongo mbaya, uzalendo wetu miaka hii, ni wa kiwango cha chini mno. Baba wa Taifa alipolihakikishia na kulitangazia Taifa kwamba uwezo wa kumpiga Amin tulikuwa nao; na kwamba sababu na nia ya kufanya hivyo tulikuwa nayo pia, tulimuamini sana. Kama alivyozoea kusema yeye mwenyewe, ‘imani huzaa imani’. Nasi hatukuutilia mashaka uchambuzi wake wa mwenendo wa mapambano ya kumung’oa na kumtokomeza Nduli Amin.
Mtanzania aliyekuwa na afya njema alihamasika kwenda mstari wa mbele - kama ni kufa ni kufa. Na yule ambaye hakuwa na uwezo wa kwenda mstari wa mbele, alichangia juhudi za vita kwa hali na mali.
Michango ya hiari ilikuwa ya aina kedekede. Wakulima, kwa mfano, walichanga vyakula mbalimbali vilivyohitajiwa na wapiganaji wetu wa mstari wa mbele. Wamiliki wa vyombo vya usafiri na usafirishaji walijitolea vyombo vyao kusafirisha wapiganaji, vyakula, zana na mahitaji mengine. Na wafugaji nchini hawakusita kutoa mifugo kwa ajili ya kuimarisha lishe ya wapiganaji wetu. Watanzania wengine walijitolea damu kwa ajili ya wapiganaji waliopata dhoruba vitani. Nakumbuka jinsi hata sisi wafanyakazi wakati ule, tulivyoridhia kwa hiari kukatwa mishahara yetu kwa ajili ya kuchangia juhudi hizo. Orodha ya michango, kwa hakika, ni ndefu sana.
Miaka hii, Watanzania tumeshuhudia kila uoza, ufisadi, ubinafsi na ulafi katika nchi yetu. Kwa bahati mbaya, uoza na ufisadi huo umeachwa kutamalaki bila dalili zozote za kujali au kuudhibiti. Nani sasa, katika mazingira haya, anaweza kujiaminisha kwamba michango kama hiyo, ikitolewa, itafika salama kwa walengwa? Nina hakika siwezi kukosea sana nikihisi kwamba viongozi wetu walipoanza kutoa kauli za vita, wapo wajanja walioanza kuchuruzika udenda wa utajirisho!
Hapana, sisi Watanzania hatuko tayari kwa vita na Malawi. Tunaiweka kete yetu katika option ya mazungumzo ya kidiplomasia, ujirani mwema na ushirikiano wa kimataifa. Huko ndiko tunakotaka watawala wetu watuelekeze.
No comments:
Post a Comment